1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hillary Clinton azidi kupeta uchaguzi wa mchujo

18 Mei 2016

Mapambano ya kuwania uteuzi wa mgombea uraisi Marekani yanaendelea ambapo Bernie Sanders ameshinda jimbo la Oregon na Hillary Clinton ametwaa ushindi wa jimbo la Kentucky katika chama cha Demokratic

https://p.dw.com/p/1IpjK
Clinton na Sanders wazidi kutoana jasho katika mbio za mchujo
Clinton na Sanders wazidi kutoana jasho katika mbio za mchujoPicha: Reuters/B. Snyder

Mgombea wa chama cha Republican akinyakua ushindi katika jimbo pekee kulikofanyika uchaguzi huo wa mchujo kwa chama cha Republican la Oregon ambapo inaashiria amefikia kilele chake kuelekea kuwa mgombea wa uchaguzi wa rais wa chama hicho.

Kwa upande mwingine baada ya miezi kadhaa ya harakati za uchaguzi wa mchujo wademokrat wanaonesha ishara kwamba huenda pakaweko matatizo ya kukiunganisha chama hicho kumuunga mkono Clinton kuwa mgombea urais katika wakati ambapo Barnie Sanders ameapa kuendelea kusonga mbele na mapambano ya kuwania uteuzi huo hadi kipyenga cha mwisho mnamo katikati ya mwezi Juni.

Sanders atahitaji kushinda kiasi thuluthi mbili ya wajumbe waliobakia ili kuwa katika nafasi sawa na mpinzani wake kabla ya kukamilisha mchakato huo ingawa mpaka wakati huo hajaonekana kuwa na dalili ya kuachia ngazi.Akizungumza katika jimbo la Carliforni jana jumanne Sanders amesema kwamba kabla ya kupata nafasi ya kummaliza Donald Trump kwanza anahitaji kummaliza Hillary Clinton.

Jumanne hiyo Clinton alipata ushindi kwa kujipatia kura za wajumbe 279 dhidi ya Sanders pamoja na kujipatia uungwaji mkono wa maafisa waliowengi chamani ikiwemo wajumbe maalum au Superdelegates.

Hillary Clinton akiwahutubia wafuasi wake baada ya kushinda Kentucky
Hillary Clinton akiwahutubia wafuasi wake baada ya kushinda KentuckyPicha: Reuters/J. Sommers

Pamoja na kwamba matokeo ya Kuntucky na Oregon hayakubadilisha kwa kiasi kikubwa hesabu ya wajumbe bado waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje Hillary Clinton anaongoza katika mbio za kuelekea kuteuliwa tarehe 7 huko New Jersey kushika bendera ya chama cha Demokratic katika kinyang'anyiro cha urais.

Katika kile ambacho kimeonekana kuwa ni kuzidi kwa mvutano ndani ya chama cha Demokratic kati ya wanaomuunga mkono Sanders na wanaoegemea upande wa Clinton,Sanders ametoa kauli nzito Jumanne akiyapinga malalamiko yanayotolewa na wafuasi wa chama hicho wanaomuunga mkono Clinton katika jimbo la Nevada kwamba walitishia kumuua mwenyekiti wa chama hicho kwa kufanya mizengwe katika matokeo na kumpa ushindi Clinton.

Sanders ameyataja malalamiko hayo kuwa ya kipumbavu na kwamba wafuasi wake hawakutendewa haki na walinyimwa heshima.Kimsingi hadi sasa Clinton anahitaji wajumbe 92 tu kufikisha idadi jumla ya wajumbe 2,383 wanaohitajika kushinda uteuzi wa kugombea urais kwa tiketi ya chama chake.

Mvutano huo wa Sanders na Clinton kwa upande mwingine unatumiwa na mgombea wa chama cha Republican Donald Trump ambaye ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba Hillary hawezi kufikia mwafaka na Barnie Sanders na hiyo ni siku nyingine mbaya sana kwa Clinton.

Hillary Clinton(Democrat) na Donald Trump( Republican)
Hillary Clinton(Democrat) na Donald Trump( Republican)Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Juu ya hilo bilionea huyo wa Marekani anayetoa kauli za ajabu katika mbio zake za kuwania uteuzi katika chama cha Republican amesikika tena mara hii akizungumzia kuhusu Korea Kaskazini ambapo ameweka wazi kwamba endapo atakuwa rais wa Marekani atazungumza na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ,jambo ambalo likitokea itakuwa ni mageuzi makubwa sana katika sera za Marekani.Akihojiwa na shirika la habari la Reuters Trump alisema hatokuwa na tatizo kuzungumza na Kim Jong Un.

Hadi sasa sera ya Marekani imekuwa ya kujaribu kuitenga serikali ya mjini Pyongyang.Trump amekwenda mbali zaidi na kusema kwamba mkakati wa kuzungumza na Korea Kaskazini ni wa kuibinya China kwasababu Marekani ina nguvu kiuchumi kuliko China.Ama kuhusu makubaliano ya tabia nchi ya mjini Paris Trump amesema pindi ataingia madarakani atalifufua upya suala hilo na kutaka makubaliano hayo yajadiliwe tena kwasababu anahisi yanainyonya Marekani na kuzipendelea nchi kama China.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman