1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Historia ya ugaidi nchini Ujerumani ni somo kwa leo

5 Septemba 2007

Katika majira ya mapukutiko ya mwaka 1977, Ujerumani ilishuhudia wakati mgumu. Kutoka Septemba tano, siku ya kutekwa nyara aliyekuwa rais wa jumuiya ya waajiri, Hanns Martin Schleyer, hadi kuuliwa kwake, siku 44 baadae, Ujerumani ilijikuta katika hali ya hatari. Magaidi wa Kundi la Jeshi Jekundu, RAF, waliokuwa wamefungwa katika gereza la Stammheim huko Stuttgart waliweka mbinyo waachiliwe huru.

https://p.dw.com/p/CH8Q
Marehemu Hanns martin Schleyer, aliyekuwa rais wa Jumuiya ya Waajiri wa hapa Ujerumani
Marehemu Hanns martin Schleyer, aliyekuwa rais wa Jumuiya ya Waajiri wa hapa UjerumaniPicha: dpa

Maelfu kwa maelfu ya polisi walitafuta wapi alifichwa Bwana Bwana Schleyer, na waliomteka nyara ni nani. Wanasiasa walitaka irejeshwe tena hukumu ya kifo. Wakuu wa sekta ya uchumi, mahakimu na wanasiasa walikuwa hatarini. Kutoka kitisho cha wakati huo hadi mitihani ya sasa inayotokana na ugaidi wa siasa kali za Kiislamu duniani kumepita sio tu miongo mitatu lakini mambo mengi yamejiri. Hebu turejee nyuma katika historia ili tupate somo na kutambua kwamba kitisho hicho- kutokana na kukamatwa karibuni hapa Ujerumani watu wanaoshukiwa kuwa magaidi- kuwa ni cha kweli zaidi kuliko wakati wowote mwengine.

Ugaidi ni njia inayotumiwa pale ushawishi na nguvu za hoja kufikia lengo la kisiasa zinaposhindwa. Hivyo ndivyo ilivokuwa kwa magaidi wa Kundi la Jeshi Jekundu, RAF, au wale wa mtandao wa al-Qaida au Wataliban. Ugaidi ni njia ya mwisho kwa wale wanaojiita wanamapinduzi au wakombozi katika kujipa haki na kupoteza vipimo vyote vya uutu. Hapo tena sio tu mahakimu, wanasiasa au wanamabenki, kama ilivotokea katika majira ya mapukutiko ya mwaka 1977 hapa Ujerumani, wahofie maisha yao, lakini kila mtu ambaye kwa sadfa amekumbwa na vitendo hivyo vya kigaidi. Bila ya kujali kama watu hao ni miongoni wa wafanya biashara katika Jengo la Kituo cha Biashara Duniani mjini New York au watalii waliokuweko siku hiyo ya asubuhi ya Septemba 11 au ni wasafiri katika basi la ghorofa mjini London, miaka michache baadae.

Ugaidi na mabomu ni sawa, bila ya kujali yanaelekezwa kwa nani, maisha yanasababisha fazaa na hofu, na bila ya kujali kama ni dhidi ya ile inayoitwa dola ya kishetani, yaani Marekani, au dhidi ya dola ya nguruwe ambayo hao wanachama wa kundi la RAF walitaka kuipiga vita hapo mwaka 1977.

Bila ya shaka, kuna tafauti kubwa baina ya ugaidi wa wakati huo wa kundi la RAF na hatari ya sasa ya ugaidi wa siasa kali za Kiislamu. Ugaidi wa kundi la Kijerumani la RAF ulikuwa na lengo dhidi ya wale waliotoa sura ya mfumo wa nchi. Kwa lugha ya kudharau uutu ya wananadharia wa wa kundi hilo la RAF, wao waliukusudia mfumo wa kidemokrasia na wa uchumi wa masoko uliokuweko katika Ujerumani Magharibi ya wakati huo kwamba ndio uliokuwa na dhamana, ukiwakilishwa na wanasiasa wakuu, wakuu wa mabenki au mahakimu. Kwa mtizamo wa kundi la Jeshi Jekundu la RAF watu hao pia ni wenye makosa pale risasi za magaidi, kama vile katika mkasa wa Hans Martin Schleyer, zinapompiga dereva na walinzi wake watatu.

Ugaidi wa al-Qaida na washirika wake duniani unawakumba watu wasiokuwa na hatia, kwa vile ugaidi huo unawaweka katika hali ya wasiwasi watu wa Ulimwengu ulio huru, mfano ni kukamatwa washukiwa hao wa ugaidi wa hapa Ujerumani.

Kama ilivokuwa miongo minne iliopita, dola sasa pia isikubali kubinywa. Ujerumami ililipa gharama kubwa kwa kukataa kuwaacha huru kutoka gerezani magaidi wa kundi la RAF, na gharama yenyewe ni kuuliwa Hanns Martin Schleyer. Waliochukuwa uamuzi wakati huo, pia kansela wa zamani Helmut Schmidt, wameomba radhi binafsi kwa familia ya Schleyer. Uamuzi mgumu wa serekali ya wakati huo umelinda heshima ya dola na utawala unaoheshimu sheria, licha ya gharama kubwa iliolipwa. Msimamo mkakamavu kama huo lazima leo uchukuliwe pale watu wenye heshima, kwa masikitiko, wanatekwa nyara na wahalifu huko Iraq. Ugaidi, kama ni wa kuteka nyara watu au wa mashambulio ya kujitolea mhanga, unaweza kukabiliwa tu kwa kutumia nguvu. Kubembeleza na kufanya mashauriano kunawapa nguvu tu magaidi. Somo hilo la majira ya mapukutiko mwaka 1977 hapa Ujerumani lazima watu wajifunze katika kupambana na ugaidi duniani.

Na yule ambaye anataka kutetea thamani za kimsingi za uhuru, lazima pia asimame kidete kuitetea misingi hii, japokuwa kuna machungu ndani yake. Na ni tu pale nguvu za ulinzi za dola zitakapokuwa haziubani uhuru wa mtu binafsi, ndipo raia watakapokuwa tayari kwa muda mrefu kutetea thamani za dola yao za kuwa na dola ya kiliberali yenye kuheshimu sheria na ilio ya kidemokrasia.