1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hoffenheim ina miadi na Berlin

7 Novemba 2008

Katika premier League-Manchester united yakutana leo na Arsenal.

https://p.dw.com/p/FpPr
Majogoo wa HoffenheimPicha: AP

Katika Bundesliga-ligi ya ujerumani,macho yanakodolewa mapambano 2 ya hapo kesho:Chipukizi Hoffenheim wana miadi na Hertha Berlin ,mjini Berlin wakati mabingwa Bayern Munich wanaitembelea Schalke mjini Gelsenkirchen wakipania kutamba na kuparamia zaidi kileleni.

Katika Premier League-ligi ya Uingereza mabingwa Manchester United wamepimana nguvu leo na Arsenal london ambayo imebidi kuteremka uwanjani bila ya jogoo lao la Togo Emmanuel Adebayor. Chelsea ikiongoza ngazi ya ligi inarudi kesho uwanjani kupambana na West Brom.

River Plate ya Argentina yapigwa kumbo nje ya Kombe la klabu bingwa la Amerika kusini-Copa Sudamericana.

Katika ringi ya mabondia,bingwa wa wezani wa juu ulimwenguni Muukraine Vitali Klitchko, aamrishwa kutetea taji lake na mkuba Carlos Gomez aliepiga kambi Ujerumani ama sivyo,atabidi kupambana na mbondia mwengine.

Baada ya FC Cologne na Hannover 96 kufungua duru ya mwishoni mwa wiki hii ya Bundesliga hapo ijumaa ,mashabiki wa Ujerumani wanasubiri kwa hamu kuu changamoto 2 za jumapili:Hoffenheim-timu iliopanda msimu huu tu kutoka daraja ya pili , ina miadi na Hertha Berlin mjini Berlin,ikitazamiwa kutamba katika mpambano wake wa 6 mfululizo.Hoffenheim imewastaajabisha mashabiki wengi nyumbani na ugenini kwa mchezo wao wa kasi na maridadi bila ya kumiliki majina makubwa ya mastadi wa dimba. Swali mara hii ni je: Hoffenheim itatamba tena na kutoroka na ushindi wa 6 mfululizo ?

Changamoto ya pili ya kusisimua zaidi ni kati ya mabingwa Bayern Munich na Schalke.Schalke wanacheza kesho nyumbani lakini, wamepumzika siku moja tu kutoka mpambano wao wa alhamisi wa kombe la UEFA na Racing Santander ya Spain wakati wenzao Bayern Munich walipumua vya kutosha walipomudu sare tu ya bao 1:1 na Fiorentina ya Itali hapo jumaane.

Hamburg imekuwa na miadi na Borussia Dortmund wakati Bremen iliongolewa meno na wagiriki Panathniakos kati ya wiki walipokandikwa mabao 3-0, wanacheza na Bochum.

Changamoto za mwishoni mwa wiki hii za Bundesliga, zitakamilishwa kesho kwa mpambano 3 baina ya Frankfurt na Stuttgart.

Tugeukie sasa Premier League-Ligi ya Uingereza mkisikia zaidi kutoka kwa Kalyango:

Msisimko wa Premier League-Ligi ya uingereza unatuwama katika changamoto ya jumamosi hii baina ya Arsenal London na Manchester United.Arsenal bila ya Mtogo Adebayor na imeshindwa tayari mara 3 msimu huu.Isitoshe wako pointi 6 nyuma ya viongozi Chelsea wenye miadi kesho na West Brom.

Katika dimba kanda ya Amerika Kusini, River Plate ya Argentina imekiona kilichomtoa kanga manyoya ilipozabwa na Guadalajara ya Mexico mabao 4-3 wiki hii na mwishoe, kutolewa nje ya Copa-amerika kusini.

Wamexico kutoka Guadalajara walitoka nyuma baada ya River kuongoza kwa mabao 2 na kuwaambia vishindo vyenu vya darini vitaishia sakafuni.Mechi hiyo ikionekana muhimu sana kwa hatima ya kocha wa River Plate Diego Simeone.Sasa Guadalajara itakumbana na Internacional walioistushja boca junior pia ya Argentina mjini Buenos aires kwa kuwachapa mabao 4-1 kupitia duru zote mbili.

Nje ya dimba, mbabe wa wezani wa juu ulimwenguni wa shirika la WBC muukraine Vitali klitschko ametakiwa na shirika la WBC kuingia haraka ringini na mkuba Carlos Gomez au itawekwa wazi nani wa kupambana nae.Klitchko akiwa na umri wa miaka 37 alirejea ringini baada ya mapumziko ya miaka 4 na alitwaa taji la WBC mwezi uliopita alipomtwanga Mnigeria Samuel Peter.Peter hakurudi ringini baada ya duru ya 8.