1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu na mashaka kuelekea kura ya maoni Sudan

Saumu Ramadhani Yusuf8 Novemba 2010

Mvutano kuhusu jimbo la Abyei waendelea

https://p.dw.com/p/Q1kr
Rais wa Sudan Omar al-Bashir na rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter, alipotembelea Sudan hivi karibuniPicha: AP

Mvutano juu ya suala la kufanyika kura ya maoni kuhusu hatma ya jimbo la Abyei unaendelea. Hii leo serikali ya Sudan imekataa kubadili msimamo wake wa kutaka kura hiyo isifanyike.

Kura ya maoni itakayoamua hatma ya jimbo la Abyei ilipangwa kufanyika sambamba na kura ya maoni kuhusu suala la kutaka kujitenga kwa Sudan Kusini hapo Januari 9 mwakani. Kura hizo zote mbili za maoni zilikubaliwa kufanyika kwa mujibu wa makubaliano ya amani ya mwaka 2005 yaliyomaliza vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Kusini na Kaskazini.

Sudan Wahlen Kandidat Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: AP

Lakini maandalizi ya kura ya maoni kuhusu  jimbo la Abyei ambalo litaamua ama kujiunga na Kaskazini au upande wa Kusini yamezungukwa na mvutano mkali kutoka pande zote mbili, hali ambayo imeibua hofu kwamba huenda zoezi hilo likaairishwa na kusababisha mzozo mpya katika eneo hilo.

Kiini cha mvutano huo ni suala la watu wa kabila la Missiriya, waarabu ambao ni wafugaji wa kuhama hama ambao husafiri kupitia jimbo hilo la Abyei kwa miezi kadhaa na kuitumia ardhi ya jimbo hilo kulisha mifugo wao.

Chama tawala huko Sudan Kaskazini cha National Congress Party (NCP) kinaamini kwamba watu hao wanastahili  kupewa nafasi ya kupiga kura ya kuamua hatma ya Abyei, mtazamo ambao unapingwa na chama cha Peoples Liberation Movement SPLM kutoka Kusini.

Chama hicho kinasema watu wa kabila la Missiriya sio wakaazi halisi wa Abyei na kwa hivyo hawana haki ya kushiriki kura hiyo  ya maoni.

Flash-Galerie Sudan People's Liberation Army
Jeshi la SPLM sudan KusiniPicha: AP

Marekani imeonekana kuingilia kati mvutano huu na kutoa ahadi kwamba ikiwa serikali ya Khartoum itakubali kura hiyo ya maoni ya Abyei ifanyike kama ilivyopangwa yaani Januari 9 basi itaondolewa katika orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi duniani ifikapo Julai mwaka 2011. Leo lakini serikali ya Khartoum imelikataa pendekezo hilo la Marekani.

Ibrahim Ghandour afisa wa ngazi ya juu katika chama tawala cha NCP ameweka bayana kwamba mkwamo bado uko pale pale ikiwa na maana kwamba kura ya maoni kuhusu jimbo la Abyei huenda isifanyike kama ilivyotarajiwa.

Tukinukulu maneno ya afisa huyo amesema, hakuna zawadi yoyote duniani, iwe ni kufutwa kutoka kwenye orodha ya magaidi au kingine chochote kitakachoweza kukishawishi chama cha NCP kukubali watu wa kabila la Missiriya au watu wengine wowote wa Abyei wanyimwe haki yao ya kupiga kura.

Itakumbukwa kwamba kabila la Missiriya walikusanywa na chama cha NCP kupigana dhidi ya kusini wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, na safari hii pia wengi wanahofia kwamba jimbo la Abyei ndilo litakalokuwa chachu ya vita vipya nchini Sudan ikiwa mvutano huo hautapatiwa ufumbuzi.

Mwandishi Saumu Mwasimba/RTRE

Mhariri Josephat  Charo.