1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu ya kura kuharibika yatanda Kenya

25 Julai 2017

Tume ya uchaguzi Kenya inahofia Wakenya wengi hawajapata elimu ya kutosha kabla ya uchaguzi mkuu. Wengi wa wapiga kura ni vijana watakaoshiriki mara ya kwanza na hivyo ipo hatari ya kura nyingi kuharibiwa.

https://p.dw.com/p/2h67Q
Kuhesabu kura Kenya
Picha: DW/ M. Braun

Kamishna wa Tume ya Uchaguzi IEBC, Roslyne Akombe, amekosoa kauli ya upinzani kuwa, wawakilishi wa vyama mbali hawataruhusiwa mita 400 kutoka kituo cha kupigia kura akisema kuwa wanakamilisha maandilizi yao. Upinzani ulikuwa umesema kuwa utawatuma waakilishi wake watano kwa kila kituo cha kupigia kura kulinda kura. 


Asilimia 60 ya wakenya ni vijana, takwimu hiyo ikimaanisha kuwa wengi wa wapiga kura kwenye uchaguzi mkuu ujao watakuwa chini ya umri wa miaka 30 hali ambayo imechangia wanasiasa wa pande zote kuwashawishi vijana kwa kuahidi kubuni nafasi tosha za kazi baada ya uchaguzi. Hata hivyo kwa mujibu wa tume inayosimamia uchaguzi na mipaka nchini Kenya, pana hofu kuwa elimu kwa wapigakura haikutekelezwa vizuri na kuwafikia walengwa. Wasiwasi wa tume hiyo ukijiri siku 13 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika. Daktari Roslyn Akombe ni mmoja wa makamishna wa tume hiyo.

Tume ya IEBC imebainisha kuwa itajaribu mitambo yake kote nchini tarehe 31 mwezi huu. Hata hivyo asilimia tano ya wakenya hawataweza kutambuliwa na mitambo hiyo. Tayari asilimia 90 ya mitambo imefanyiwa majaribu hadi sasa. Ili kukabiliana na changamoto za kimitambo, tume hiyo imesema kuwa wamekodi huduma za kampuni tatu za kutoa huduma za simu za mkononi. Saala ya tume ya mipaka tarehe nane mwezi ujao, ni kuwa mitambo ya kupiga kura haitakuwa na matatizo. 

Vituo vya kupiga kura vitafunguliwa saa kumi na moja asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni siku ya uchaguzi. Wagombea saba wakitarajiwa kutoana jasho kwenye kinyang’anyiro hicho. Hata hivyo ushindani mkubwa unatarajiwa kuwa kati ya rais Uhuru Kenyatta na kinara wa mmungano mkuu wa upinzani Raila Odinga wa NASA. Huku upinzani ukidai kuwa utakuwa na maafisa watano katika kila kituo, tume ya uchaguzi na mipaka imesema kuwa maafisa wake pamoja na walinzi ndio wataruhusiwa kwenye vituo hivyo. 

Matamshi ya tume ya IEBC huenda yakaibua mvutano mwingine kati yake na upinzani ambao tangu mwanzo umekuwa ukidai kuwa inashirikiana na serikali kuiba kura kwenye uchaguzi mkuu. Kinara wa upinzani Raila Odinga anasimama kidete kuhusu msimamo wao. 

Wakenya milioni 19 wanataraiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo ambao kura ya maoni inabashiri kuwa huenda ikaelekea kwa awamu ya pili baada ya rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga kutoshana nguvu kwenye awamu ya kwanza ya kipute hicho.