1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu yazidi kuongezeka Israel na Palestina

Lilian Mtono
14 Mei 2021

Wakati mzozo kati ya Israel na Palestina ukizidi kutokota, Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litakutana Jumapili kujadili ongezeko la machafuko kati ya majirani hao wa Mashariki ya Kati. 

https://p.dw.com/p/3tNwk
Israel  Ashkelon Iron Dome fängt Raketen aus Gazastreifen ab
Picha: Amir Cohen/REUTERS

Wakati mzozo kati ya Israel na palestina ukizidi kutokota, Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumapili linatarajia kufanya kikao kwa njia ya video kujadili ongezeko la machafuko kati ya majirani hao wa Mashariki ya Kati. 

Kulingana na wanadiplomasia, Marekani ambayo ilizuia kikao hicho ambacho awali kilipangwa kufanyika hii leo na kupendekeza kufanyika mapema wiki ijayo, hatimaye wamekubaliana kukihamishia siku ya Jumapili kufuatia maombi kutoka kwa Tunisia, Norway na China. Marekani ilitaka kwanza kuruhusu njia za kidiplomasia na kusema inaunga mkono majadiliano ya wazi kwenye Umoja wa Mataifa na kwamba haipingani na kikao hicho.

Rais Joe Biden amesema bado anashinikiza kusitishwa kwa mapigano hayo, ingawa maafisa wanakiri  kwamba mzozo huo utaendelea ama kuongezeka kwa siku kadhaa zijazo. Biden amesema kinachotakiwa sasa ni kuangazia namna watakavyoweza kupunguza mashambulizi hususan ya maroketi ambayo huelekezwa kwenye maeneo yenye watu wengi na kuongeza kuwa kazi bado inaendelea.

Wakati miito ikiongezeka kwa Biden kuchukua hatua zaidi za moja kwa moja, bado haiko wazi ni kwa namna gani rais huyo Marekani ambayo ni mshirika muhimu wa Israel atakavyojiingiza kwenye mzozo huo na kuweza kuzishawishi pande zote mbili.

Weltspiegel 11.05.2021 | USA Washington | Joe Biden, Präsident
Rais Joe Biden akabiliwa na shinikizo zaidi la kuuingilia mzozo huo moja kwa moja.Picha: Drew Angerer/Getty Images

Biden ameibadilisha ghafla sera ya Marekani kuelekea Israel kutoka kwa mtangulizi wake mrepublican Donald Trump na kuendelea kusisitizia umuhimu wa suluhu ya mataifa mawili katika mzozo huo.

Mapema leo waziri mkuu Netanyahu amesema Israel itaendeleza kampeni dhidi ya kundi la Hamas iwapo watalazimika kufanya hivyo. Amesema kwenye taarifa iliyorekodiwa kwamba taifa hilo limeahidi kulipiza kisasi, kufuatia mashambulizi ya maroketi ya Hamas dhidi ya taifa la Israel.

Amesema "Narudia kile nilichosema mapema leo. Tunawasaidia kwa asilimia 100 polisi, Polisi wa Mpakani na vikosi vingine vya usalama ili kurejesha sheria na utulivu katika miji ya Israel. Hatutavumilia machafuko. Tunawasaidia polisi kutumia nguvu kamili. Hatua hizi zote ni muhimu, halali na zinahitajika ili kusimamisha uasi huu katika taifa la Israel."

China yaishutumu Marekani kwa kupuuza "mateso" dhidi ya Waislamu wa Palestina.

Katika hatua nyingine, China imeishutumu Marekani kwa kupuuza kile walichoita mateso dhidi ya Waislamu baada ya kukizuia kikao hicho cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Hua Chunying amesema kile wanachohisi ni kwamba Marekani ambayo huwa inajigamba kuwa inajali haki za binaadamu, hivi sasa inapuuzia mateso yanayowakumba Waisalamu wa Palestina.

Amesema, Marekani inatakiwa kutambua kwamba maisha ya Waislamu wa Palestina pia yana thamani.

Katika hatua nyingine, msemaji wa jeshi la Israel Jonathan Conricus amesema wamepeleka ndege 160 kwenye ukanda wa Gaza ili kusambaratisha mtandao wa mahandaki yanayotumiwa na Hamas wanaolidhibiti eneo hilo.

Huku hayo yakiendelea, familia za Wapalestina zimeanza kukimbilia maeneo ya jirani ya viunga vya Gaza hii leo, wakati Israel ikianzisha mashambulizi mazito kwenye mtandao huo.

Pande hizo mbili zimeingia kwenye awamu mpya ya mashambulizi baada ya hali ya wasiwasi kuzidi kuongezeka. Wanamgambo hao wameishambulia Israel kwa takriban maroketi 1,800 tangu siku ya Jumatatu. Hadi sasa Israel imeripoti vifo vinane huku wizara ya afya ya Gaza ikiripoti vifo 119 na majeruhi 830 kufuatia mashambulizi ya kisasi yaliyofanywa na Israel.

Mashirika: DPAE/AFPE/RTRE