1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande Afanya Ziara Marekani

11 Februari 2014

Rais wa Ufaransa Francois Hollande yuko Marekani kwa ziara ya siku 3, ambapo anatarajiwa kuzungumza na mwenyeji wake Barack Obama juu ya masuala kadhaa, yakiwemo Syria, Iran na operesheni za kulinda amani barani Afrika.

https://p.dw.com/p/1B6bH
Rais Francois Hollande aliwasili mjini Washington Jumatatu kuanza ziara rasmi ya siku 3
Rais Francois Hollande aliwasili mjini Washington Jumatatu kuanza ziara rasmi ya siku 3Picha: AFP/Getty Images

Mizinga 21 imewekwa tayari kufyetuliwa kwenye busitani ya Ikulu ya Marekani, kwa heshima ya rais Francois Hollande, atakapowasili kwenye Ikulu hiyo kwa mazungumzo yatakayoangazia masuala kadhaa muhimu duniani, kama vile mpango wa nyuklia wa Iran, mabadiliko ya tabia nchi, na vita dhidi ya makundi ya kiislamu yenye misimamo mikali.

Baadaye Hollande na mwenyeji wake, Barack Obama watanyanyua glass zao za mvinyo, kusherehekea kile ambacho rais wa Ufaransa amekiita urafiki wa milele kati ya nchi yake na Marekani, ambao ulianzishwa enzi za mapinduzi miaka 200 iliyopita. Urafiki huo lakini kwa sasa unrekebishwa baada ya kuvurugika kutokana na tofauti kuhusu vita vya Irak.

Marekani ilitoa msaada wa vifaa kwa jeshi la Ufaransa katika mapambano yake dhidi ya makundi ya kiislamu nchini Mali, na pia nchi hizi mbili ni washirika katika mazungumzo na Iran yanayonuia kupata suluhisho la kisiasa kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo. Marekani na Ufaransa hali kadhalika zina msimamo wa aina moja kuhusu mgogoro wa Syria.

Urafiki wa kihistoria

Mnamo siku ya kwanza ya ziara yake, Hollande akiambatana na mwenyeji wake walitembelea nyumba ya Thomas Jefferson, rais wa tatu wa Marekani ambaye aliwahi kuwa balozi wa nchi yake mjini Paris, na aliyezungumza lugha ya kifaransa.

Marais Hollande na Obama, wanatarajiwa kusisitiza uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi zao.
Marais Hollande na Obama, wanatarajiwa kusisitiza uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi zao.Picha: Reuters

Akizungumza wakati wa kuitembelea nyumba hiyo, rais Obama alisema hiyo ilikuwa fursa ya kukumbusha msingi wa urafiki baina ya nchi mbili.

''Naamini kwa kuanza ziara namna hii, tunaweza kugeuka na kuangalia urafiki kati ya Ufaransa na Marekani tangu vizazi viwili vilivyopita. Katika mazungumzo ya kesho, sio kwamba tutajikita tu juu ya mizozo ya sasa, bali pia jinsi ya kuuendeleza uhusiano wetu siku za usoni.'' Alisema Obama.

Holande aliitumia ziara kwenye nyumba hiyo iliyoko katika jimbo la Virginia kukumbushia historia ya urafiki baina ya Ufaransa na Marekani, akitaja Marquis de Lafayette, mfaransa kutoka familia ya kifalme aliyeshiriki katika vita vya uhuru wa Marekani, na jeshi la Rais wa kwanza wa Marekani George Washington, ambalo kulingana na maelezo ya rais wa Ufaransa, lilikuwa la kimapinduzi.

Mazungumzo rasmi ni leo

Lakini kazi rasmi ya ziara yake itaanza baadaye leo katika chumba cha mikutano cha Ikulu ya White House, wakati marais hao wawili watakapozungumzia masuala magumu, yanayotarajiwa kugusia mzozo wa Syria, mazungumzo na Iran, na mgogoro unaoendelea nchini Ukraine. Masuala yenye utata kama kashfa ya udukuzi wa Marekani juu ya washirika wake, ikiwemo pia Ufaransa, yanatarajiwa kujadiliwa.

Operesheni za kijeshi za Ufaransa barani Afrika ni miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele.
Operesheni za kijeshi za Ufaransa barani Afrika ni miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele.Picha: Getty Images/AFP

Masuala mengine ambayo inaaminika yatakuwa kwenye meza ya mazungumzo ni operesheni za jeshi la Ufaransa nchini Mali na katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambazo Marekani inasaidia kwa kutoa taarifa za kijasusi, na vifaa.

Ziara ya rais Francois Hollande ni ya kwanza rasmi kufanywa na rais wa Ufaransa nchini Marekani tangu mwaka 1996. Vile vile Hollande anatumia ziara hii kuyakwepa kidogo matatizo katika maisha yake binafsi, hasa ya kimapenzi ambayo yamesababisha kutengana kwake na mke aliyekuwa akiishi naye, Valerie Trierweiler.

Baadaye marais wawili, Francois Hollande na Barack Obama watafanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE

Mhariri:Hamidou Oummilkheir