1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande na Merkel wakutana kwa mara ya kwanza

Abdu Said Mtullya16 Mei 2012

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, amefanya ziara yake ya kwanza nchini Ujerumani. Wahariri wanatoa maoni yao juu ya ziara hiyo

https://p.dw.com/p/14wMW
Kansela wa Ujerumani Kansela Angela Merkel na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais Francois Hollande wa UfaransaPicha: Reuters

Mhariri wa gazeti la" Badische Zeitung"anasisitiza umuhimu wa mshikamano baina ya Ujerumani na Ufaransa katika muktadha wa mitazamo tofauti baina ya Rais Hollande na Kansela Merkel juu ya njia ya kuutatua mgogoro wa madeni barani Ulaya.

Mhariri huyo anasema kwa kuwa katika siasa za kimataifa mtu hawezi kumchagua mshirika amtakae, Hollande na Merkel wanapaswa kutafuta njia ya kuja pamoja,hasa kutokana na kutambua kwamba bila ya mshikamano baina ya nchi zao hakuna kitakachosonga mbele barani Ulaya.

Mhariri wa gazeti la"Flensburger Tageblatt" anasema kwamba katika uhusiano baina ya Ufaransa na Ujerumani jambo la kipaumbele ni nchi na siyo mwanasiasa. Na kwa hivyo siyo muhimu ni mtu gani ni Rais wa Ufaransa au Kansela wa Ujerumani, jambo muhimu ni kuelewana.

Gazeti la"Stuttgarter"linautilia maanani uwezo wa Ujerumani na Ufaransa wa kuziondoa tofauti baina yao katika uhusiano wao. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa mipango juu ya kuleta ustawi haitauondoa ulazima wa kubana matumizi. Mustakabal wa bara la Ulaya unategemea sana sera za mageuzi.

Mgogoro wa kisiasa nchini Ugiriki unaweza kuwa mtihani mkubwa kwa mshikamo wa Ujerumani na Ufaransa. Lakini hadi sasa,jambo moja limeonekana,kwamba katika mgogoro wa madeni,Ujerumani na Ufaransa zimezidi kusogeleana.

Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linakumbusha kwamba mshikamano wa kirafiki baina ya Kansela Merkel na aliekuwa Rais wa Ufaransa, Sarkozy, haukujengeka katika kipindi cha kufumba na kufumbua. Mhariri wa gazeti hilo anasema mara tu baada ya kuanza kazi,Rais wa Ufaransa Hollande amefanya ziara nchini Ujerumani na amefanya mazungumzo na Kansela Merkel. Lengo la ziara hiyo ni kujuana na kuyaangalia kwa undani mawanda ya kazi ya pamoja. Katika nyanja fulani,ushirikiano baina ya Merkel na Hollande unaweza kuwapo bila ya utata. Kwani ushirikiano wa karibu baina ya Sarkozy na Merkel ulihitaji muda kujengeka.

Gazeti la"Neue Osnabrücker" linasema Rais Hollande ameingia madarakani wakati ambapo nchi yake inakabiliwa na changamoto kadhaa. Ufaransa inakabiliwa na ukosefu wa ajira wa kiwango kikubwa, nchi hiyo ina deni kubwa na uchumi wake umekwama.Na barani Ulaya kwa jumla, mgogoro wa madeni unazidi kuwa mkubwa, na hasa nchini Ugiriki ambako uchaguzi mwingine utafanyika.

Wakati changamoto hizo zinaendelea kuwa kubwa,injini muhimu barani Ulaya, yaani mshikamano baina ya Ufaransa na Ujerumani,inapaswa kutiwa ufunguo upya. Hollande na Merkel hawana muda wa kusubiri. Badala yake wanapaswa kuziondoa tofauti zao haraka. Kauli mbiu haiwezi kuwa kubana matumizi au kutumia fedha ili kuleta ustawi. Kinachotakiwa ni kuleta ustawi, lakini chonde, siyo kwa njia ya kujitumbukiza zaidi katika madeni.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Miraji Othman