1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Homa ya nguruwe yaenea katika nchi kadhaa

27 Aprili 2009

Tahadhari yatolewa kuepuesha maambukizi zaidi

https://p.dw.com/p/Herr
Wataalamu wahofia homa hiyo huenda ikawa janga la dunia.Picha: AP

Maafisa wa afya kote duniani wanashirikiana kuidhibiti homa inayosababishwa na nguruwe ambayo inaaminika imeua zaidi ya watu 100 nchini Mexico.

Waziri wa afya Jose Angel Cordova amesema kwamba idadi ya watu wanaoshukiwa kuwa na virusi vya homa hiyo nchini humo imeongezeka na kufikia watu 1,614.

Shirika la afya duniani WHO limefahamisha kuna hatari kwamba mkurupuko wa homa hiyo mpya ambayo kwa sasa imegunduliwa katika nchi za Marekani,Canada pamoja na Mexico ukasambaa na kuwa janga kamili.

Maßnahmen in Zusammenhang mit der Schweinegrippe in Mexiko am Flughafen
Tahadhari zachukuliwa katika viwanja vya ndege nchini Mexico na kwingineko.Picha: AP

Mpaka sasa Marekani imetangaza hali ya dharura katika sekta ya afya ya umma baada ya kugunduliwa visa vya maambukizi ya watu 20 na kutangaza mipango ya kuwafanyia uchunguzi wa kimatibabu wageni wote wanaowasili kutoka nchi zilizoathirika na homa hiyo.

Akitangaza juu ya tahadhari za kuchukuliwa nchini Marekani waziri wa usalama wa ndani Janet Napolitano amesema kwamba inambidi kila mmoja kuhakikisha usafi wa mwili pamoja na mazingira ili kuepuesha maambukizi ya homa hiyo nchini Marekani.

Maafisa nchini Canada wamethibitisha kwamba watu sita wameambukizwa virusi vya homa hiyo.

Barani ulaya watu kadhaa wanafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kutokana na kushikiwa kuwa na homa hiyo pamoja na katika eneo la mashariki ya kati na Asia.

Waziri wa afya nchini Newzealand amesema kwamba watu 40 wanaoshukiwa kuwa na virusi vya homa hiyo inayoambukiza wamewekwa katika karantini wakiwemo wanafunzi 13 ambao hivi karibuni walisafiri kwenda Mexico na kugunduliwa kuwa na virusi vya homa hiyo.

Kwa upande mwingine Australia imesema kwamba raia wake wawili wameonyesha dalili ya kuambukizwa homa hiyo ya nguruwe.

Saumu Mwasimba/AFPE