1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Homa ya Nguruwe yasambaa hadi Ulaya

28 Aprili 2009

Ulimwengu mzima unajiandaa kuchukua hatua madhubuti za kupambana na kuenea homa ya nguruwe iliyozuka nchini Mexico. Virusi hivyo vinaripotiwa vimesambaa hadi barani Ulaya ambako mtu mmoja ameambukizwa homa hiyo hatari

https://p.dw.com/p/HfZb
Wakazi wa Mexico wajihami kwa vichuja puaPicha: AP


Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya watu 149 wamefariki mpaka sasa Mexico pekee. Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, kwa upande wake, limetangaza kuwa ugonjwa huo umefikia kiwango cha hatari ya maambukizi kati ya binadamu na huenda ukasababisha janga.


Punde baada ya Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, kutoa onyo hilo masoko ya hisa barani Asia yanaripotiwa kutetereka. Mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyeripotiwa kufariki nje ya Mexico, japokuwa watu 50 wameripotiwa kuambukizwa virusi vya homa hiyo katika mataifa ya Marekani, sita huko Canada na barani Ulaya ambako mtu mmoja ameambukizwa nchini Uhispania. Taarifa hizo zimethibitishwa na Kamishna wa Masuala ya Afya wa Umoja wa Ulaya, Androulla Vassilou aliyeeleza kuwa ''Tumepokea thibitisho kutoka kwa idara ya afya nchini Uhispania kuwa kuna mtu mmoja aliyeambukizwa virusi vya homa ya nguruwe katika eneo la Umoja wa Ulaya''


Mexiko Schweinegrippe Schweinehaltung in Xonacatlan, Mexico
Nguruwe wanaosambaza virusi vya homa hiyo hatariPicha: AP

Homa ya nguruwe inaweza kutibiwa kwa haraka kwa kutumia dawa ya kupambana na virusi. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, kwa upande wake limesisitiza umuhimu wa kujizatiti kuzuia virusi hivyo kusambaa zaidi, ila limepinga hatua ya kuifunga mipaka ya Mexico. Naibu Mkurugenzi wa Shirika hilo la WHO, Keiji Fukuda amelielezea hilo,''Mkurugenzi mkuu amependekeza kutofunga mipaka au kupiga marufuku safari zozote zile.Hata hivyo, ni muhimu kwa wagonjwa kutosafiri.''


Kufuatia tangazo la Shirika la WHO serikali kote ulimwenguni zimewashauri raia wao kutoizuru Mexico pasipo sababu za msingi, kadhalika kuimarisha uangalizi katika viwanja vya ndege vya kimataifa. Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Marekani tayari zimewatahadharisha raia wao kutoizuru Mexico inayotegemea pato la fedha za kigeni katika sekta ya Utalii.


Japan imewashauri raia wake walioko Mexico kurejea nyumbani kabla hali haijakuwa mbaya.

China kwa upande wake imeahidi kutangaza taarifa zozote za watu walioambukizwa homa ya nguruwe pindi watakapozipata. Itakumbukwa kuwa mwaka 2003 serikali ya China ilijitahidi kubana maelezo yoyote yale kutangazwa baada ya homa ya mafua makali ya SARS kuzuka.

Ulimwengu ulijifunza kutokana na jaa hilo. Dr Malik Peris ni mmoja wa wanasayansi waliohusika katika vita hivyo.Amesema''Somo moja tulilopata ni kwamba hospitali na vituo vya afya vinaweza kuwa chanzo cha kusambaa kwa virusi. Watu wana ufahamu mkubwa zaidi kwa sasa kwamba usafi ni jambo la msingi na virusi hivyo vinawezwa kusambazwa kwa mikono au kukohoa.''


Mlipuko wa homa kali ya mafua uliotokea mwaka 1968 nchini China ulisababisha vifo vya yapata watu milioni moja kote ulimwenguni. Raia wengi wa Mexico wamelazimika kuvaa vichuja pua katika maeneo mengi nchini humo. Mikahawa,majumba ya sinema,viwanja vya michezo na baadhi ya afisi za serikali vyote vimefungwa ili kuzuia virusi hivyo kusambaa. Shule nazo zimefungwa hadi ifikapo tarehe 6 mwezi ujao wa Mei. Kulingana na maafisa wa afya wa Mexico, virusi vya homa hiyo havisambazwi kwa kula nyama ya nguruwe.


Mwandishi: Thelma Mwadzaya RTRE/AFPE

Mhariri:Othman Miraji