1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hosni Mubarak arejea tena Mahakamani

MjahidA25 Agosti 2013

Aliyekuwa rais wa Misri Hosni Mubarak anarejeshwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya waandamanaji mwaka wa 2011 katika maandamano ya umma yaliomuondoa madarakni.

https://p.dw.com/p/19VmB
Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak.
Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak.Picha: picture-alliance/dpa

Kesi hii ni moja kati ya mashitaka mengine dhidi ya rais huyo wa zamani aliyeondolewa kutoka gerezani wiki iliyopita. Mubarak aliwekwa katika kifungo cha nyumbani na waziri mkuu wa serikali ya mpito Misri Hazem el-Beblawi.

Rais huyo wa zamani aliye na umri wa miaka 85 , na aliyefunguliwa mashitaka mwezi wa Juni mwaka jana na kuhukumiwa kifungo cha maisha kwa sasa anazuliwa katika hospitali ya kijeshi mjini Cairo na haijawa wazi iwapo ataweza kuhudhuria kesi yake leo.

Wakati huo huo viongozi wa chama cha Udugu wa Kiislamu Mohamed Badie, Rashad Bayoumi na Khairat al-Shater wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza leo(25.08.2013) ambapo pia wanakabiliwa na makosa ya mauaji na uchochezi.

Kiongozi wa Kidini wa chama cha Udugu wa Kiislamu Mohamed Badie
Kiongozi wa Kidini wa chama cha Udugu wa Kiislamu Mohamed BadiePicha: Mahmud Hams/AFP/Getty Images

Badie alikamatwa wiki iliopita, ambapo ni mara ya kwanza kwa kiongozi mkuu wa kidini wa chama cha udugu wa kiislamu kutiwa nguvuni tangu mwaka 1981.

Badie, Shater na Bayoumi wanadaiwa kuhusika na mauaji ya waandamanaji waliofariki nje ya makao makuu mjini Cairo mnamo Juni 30, ambapo mamilioni ya waandamanaji walishiriki maandamano dhidi ya Mohammed Mursi.

Wanachama wengine watatu pia watajiunga na wenzao katika kusikiliza kesi hiyo. Iwapo wote sita watapatikana na hatia huenda wakahukumiwa kifo.

Bado kuna wasiwasi wa kutoke ghasia zaidi.

Hata hivyo kusikilizwa kwa kesi hizo mbili katika maeneo tofauti ya mji kunaendeleza hofu nchini humo baada ya kukumbwa na machafuko tangu July 3 ambapo rais wa nchi hiyo Mohammed Mursi aliondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi.

Kesi hizi zinafanyika wakati kukishuhudiwa utulivu kufuatia ghasia baada ya wiki nzima ya umwagikaji wa damu. Ghasia zilianza Agosti 14 wakati vikosi vya serikali viliposhambulia kambi za waandamanaji wanaomuunga mkono Mursi.

Rais aliyepinduliwa madarakani Mohammed Mursi
Rais aliyepinduliwa madarakani Mohammed MursiPicha: imago

Huku hayo yakiarifiwa Mursi ambaye anazuiliwa katika eneo ambalo halijulikani anatarajiwa kufunguliwa mashtaka juu ya kutoroka jela wakati wa maadamano ya kutaka mabadiliko mwaka 2011.

Tangu kuanza kwa ghasia baada ya polisi kuvunja kambi za waandamanaji watu 600 wameuwawa na wengine wengi wamejeruhiwa.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP

Mhariri Sekione Kitojo