1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hotuba ya kansela Merkel bungeni

Oumilkher Hamidou10 Novemba 2009

Kansela Merkel atahadharisha Ujerumani inaweza kukabiliana na wakati mgumu

https://p.dw.com/p/KTKR
Kansela Angela Merkel akihutubia bungeni mjini Berlin leoPicha: AP

Kansela Angela Merkel anapanga kutia njiani mpango wa vifungu vitano kwa lengo la kuikwamua Ujerumani toka mgogoro wa kiuchumi na kuipatia msukumo mpya.Kansela Angela Merkel amefafanua mpango huo ,katika hotuba yake bungeni hii leo.

Katika hotuba yake ya kwanza bungeni kama kiongozi wa serikali ya muungano wa vyama vya CDU/CSU na waliberali wa FDP kansela Angela Merkel amezungumzia juu ya kipindi kigumu kinachowasubiri wajerumani.Kansela Merkel amehakikisha hata hivyo huduma za jamii zitadhaminiwa.Upande wa upinzani unahofia mgawanyiko miongoni mwa jamii.

Katika mhula wake wa pili madarakani,kansela Angela Merkel amepania kusafisha mabaki ya mgogoro wa kiuchumi,kurejesha hali ya kuaminiana kati ya serikali na wananchi,kuufanyia marekebisho mfumo wa jamii,kubuni mkakati madhubuti wa kuhifadhi hali ya hewa kote ulimwenguni na kuhakikisha wezani sawa kati ya uhuru na usalama.

"Ujerumani inakabiliana na changamoto ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu muungano" amesema kansela Angela Merkel,hii leo ,wiki mbili baada ya kukabidhiwa kwa mara ya pili wadhifa huo."Karata zitachanganywa upya.Tukifanya makosa upande huo,basi hayataweza kurekebishika.

Tukifanya vyema,basi Ujerumani itapata nguvu zaidi."Amesisitiza.Kansela Angela Merkel ameahidi uchambuzi wa kina ili mpango wa serikali yake ufanikiwe.Ameutolea mwito upande wa upinzani,sawa na wanauchumi,makanisa na jamii, washirikiane ili kwa pamoja waiongoze Ujerumani katika njia iliyo bora.

Kansela Angela Merkel amesema:

"Jamii inaweza tuu kuimarishwa ikiwa watu wengi zaidi watapatiwa kazi,ikiwa masomo ya maana yatafungua njia ya kupanda daraja,ikiwa urasimu usiokua na maana utabomolewa,kwa maneno mengine ikiwa bidii italeta tija katika nchi hii........"

Kansela Angela Merkel ametetea mipango ya kuufanyia marekebisho mfumo wa afya na kuelezea pia azma ya kushiriki katika mkutano wa kilele wa hali ya hewa mjini Copenhagen.Amezungumzia pia umuhimu wa kuendelezwa mazungumzo pamoja na Urusi akisema anaunga mkono msimamo wa rais Barack Obama wa Marekani wa kuitakasa dunia na silaha za atomiki.

Deutschland Frank-Walter Steinmeier Bundestag Regierungserklärung
Kiongozi wa kundi la SPD bungeni,F-W. Steinmeier akihutubia bungeniPicha: AP

Upande wa upinzani unakosoa mpango wa serikali ya muungano wa vyama vya CDU/CSU na waliberali wa FDP.Kiongozi wa kundi la SPD bungeni,Frank-Walter Steinemeir anamtuhumu kansela Angela Merkel kutaka kuutia hatarini mfumo wa jamii na kuongeza bila ya kiasi madeni ya serikali.Mkuu wa kundi la chama cha mrengo wa shoto Die Linke,Oscar Lafontaine anasema kansela Angela Merkel hakutoa mapendekezo yoyote ya kumaliza mgogoro wa kiuchumi.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou /dpa

Mhariri:Abdul-Rahman