1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huenda matokeo ya mwanzo ya uchaguzi DRC yakacheleweshwa

Amina Mjahid
3 Januari 2019

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo CENI, Corneille Nangaa amesema huenda wakasitisha zoezi la kutoa matokea ya mwanzo katika uchaguzi wa rais uliomalizika hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/3B0C2
Demokratische Republik Kongo - Wahl: Corneille Nangaa Yobeluo
Picha: Getty Images/AFP/L. Tato

Nangaa amesema wanafanya kila wawezalo ili kutoa matokeo ya mwanzo tarehe 6 Januari. Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ni nchi kubwa katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara na nchi ambayo haipo imara kiusalama na iliokumbwa na mgogoro wa kisiasa kwa takriban miaka miwili iliyopita.

Kongo nach der Wahl
Wanachama wa CENI wakihesabu kura baada ya kumalizika zoezi la uchaguzi Picha: Reuters/B. Ratner

Rais Joseph Kabila aliye na miaka 47 alipaswa kuachia madaraka mwaka 2016, muda wake rasmi wa mihula miwili kama rais kulingana na katiba ya Congo ulipaswa kumalizika rasmi mwaka huo. Lakini akatumia kipengee cha kuwa msimamizi wa serikali kuendelea kubakia madarakani hali iliyozua ghasia na kusababisha mauaji ya watu kadhaa.

Baada ya uchaguzi kuahirishwa mara kwa mara, hatimae uchaguzi huo ulifanyika Desemba 30 kumchagua mrithi wa rais Joseph Kabila. Hata hivyo kumekuwa na wasiwasi juu ya namna hesabu za kura zilizopigwa zinavyofanyika huku upinzani ukiwa na hofu kwamba matokeo huenda yakachakachuliwa ili kumpitisha mgombea aliye chaguo la chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary.

Tume ya Uchaguzi CENI imesema huenda ikatoa matokeo ya mwanzo Januari 6  huku matokeo rasmi yakitarajiwa kutolewa tarehe 15 mwezi huo huo na rais mpya akitarajiwa kuapishwa siku tatu baadae.

Upinzani unadai kura huenda zikaibwa kwa manufaa ya mgombea wa chama tawala

Corneille Nangaa mwenyekiti wa CENI amesema kuhesabu kura kwa mikono ni jambo lililowapa changamoto kubwa. Kila eneo lililoshiriki katika uchaguzi linajukumu la kuhesabu kura zake kisha kuzipeleka katika eneo linalokusanywa kura zote ili zijumlishwe tayari kwa kutangazwa. Lakini miundo mbinu sio mizuri nchini humo barabara ni mbovu na hatua hiyo imetoa changamoto kwa matokeo kufikishwa kwa wakati.

Kongo hält mit zwei Jahren Verspätung historische Wahlen ab
Mashine za kielektroniki zilizotumika katika uchaguzi wa Congo 2018Picha: Reuters/K. Katombe

CENI ilitumia mfumo wa kielektroniki katika uchaguzi huo, ambako wapiga kura walitumia kijiskrini cha kubovya kumchagua kiongozi wanaemtaka ili baadae mashini ichapishe matokeo hayo ambayo baadaye yangeliwekwa katika masanduku ya kupigia kura.

Amesema mfumo wao baadae ulikataliwa na kwa sasa ni lazima watu wasubiri kura zihesabiwe kwa mikono jambo litakalochelewesha matokeo.

Awali upinzani ulidai mashine hizo huenda zikatumiwa katika wizi wa kura katika uchaguzi huo kupitia mfumo wa kielektroniki.

Baadhi ya wagombea wajitangazia ushindi kabla ya matokeo rasmi

Huku hayo yakiarifiwa tume hiyo ya uchaguzi ilipitia changamoto nyengine ambapo muda mfupi baada ya uchaguzi kufanyika tayari kulikuwepo na wagombea waliojitangazia ushindi.

Kollage von den vier Top-Kandidaten DR Kongo
Baadhi ya wagombea wa urais Emmanuel Ramazani Shadary, Vital Kamerhe, Felix Tshisekedi na Martin Fayulu

Mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary na Felix Tshisekedi mkuu wa chama cha upinzani cha UDPS chama kikongwe na kikubwa cha upinzani walijitangazia kushinda katika uchaguzi huo.

Lakini kulingana na utafiti wa maoni ya wapiga kura uliofanyika kabla ya uchaguzi wa rais Martin Fayulu alionekana kuwa kipenzi cha wengi.

Huku hali ya wasiwasi ikiendelea kuonekana wazi nchini humo serikali ilisitisha huduma zai interneti na kukatiza matangazo ya kituo cha Kimataifa cha Radio France Internationale RFI ikiishutumu kwa kutangaza matokeo madai yanayoendelea kukanushwa na kituo hicho.

Kwa sasa hamu kubwa kwa raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ni kumjua rais wao Januari 15 na kuwepo amani baada ya matokeo hayo kutangazwa rasmi na tume ya uchaguzi CENI.

Mwandishi: Amina Abubakar /AFP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo