1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hujuma za ndege zisizo rubani zachunguzwa

25 Januari 2013

Umoja wa Mataifa umeanzisha uchunguzi wa kutumiwa ndege zisizokuwa na rubani katika operesheni dhidi ya magaidi kufuatia lawama kwamba operesheni hizo zimeangamiza maisha ya raia kadhaa wasiokuwa na hatia.

https://p.dw.com/p/17RFm
Ndege isiyokuwa na rubani chapa General Atomics MQ-1A Predator

Uamuzi huo uliotangazwa mjini London unahusu uchunguzi wa hujuma 25 za ndege zisizoendeshwa na marubani nchini Pakistan, Yemen,S omalia, Afghanistan na katika ardhi za wapalastina.

Nyingi ya hujuma hizo zimefanywa na Marekani. Uingereza na Israel pia wametumia ndege hizo zisizokuwa na rubani na mataifa mengine dazeni kadhaa yanasemekana pia kuitumia teknolojia hiyo.

Akitangaza uamuzi wa kuanzishwa uchunguzi huo, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anaesimamia haki za raia katika mapambano dhidi ya magaidi, Ben Emmerson, amesema lengo kuu la uchunguzi huo "ni kutafuta ushahidi kama mashambulizi ya ndege zisizoendeshwa na marubani na vyombo vyenginevyo vinavyofyetuliwa kutoka mbali yamesababisha hasara iliyokithiri miongoni mwa raia na kutoa mapendekezo kuhusu jukumu la serikali kufanya uchunguzi ulio huru, usiokuwa na mapendeleo kuhusu madai hayo."

Mjumbe huyo maalum wa umoja wa mataifa amesema ni muhimu kuwepo mikakati halali ya opereshini kama hizo na ambayo itaambatana na sheria za kimataifa.

Jenerali mstaafu wa kimarekani Stanley McChristal, aliyebuni mkakati wa kupambana na waasi nchini Afghanistan, ameonya mapema mwezi huu dhidi ya kutumiwa kila kwa mara ndege zisizokuwa na rubani, akisema zinasababisha hasara kubwa ya maisha ya binaadam na kuzusha ghadhabu na maandamano nchini Pakistan.

Matokeo ya uchcunguzi yatarajiwa kabla ya mwisho wa mwaka

Ben Emmerson Pressekonferenz UN Drohnen
Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa Ben Emmerson akizungumza na waandishi habariPicha: C.Court/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa tarakimu za Kituo cha waandishi habari wanaofanya uchunguzi - Bureau of Investigative Journalism - watu kati ya 2600 na zaidi ya 3400 wameuliwa nchini Pakistan kutokana na hujuma za ndege zisizorushwa na rubani-kati ya 473 hadi 889 walikuwa raia wa kawaida.

Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa lilishauri uchunguzi huo ufanywe kutokana na maombi ya nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Pakistan, Urusi na China.

Matokeo ya uchunguzi huo yatawasilishwa mbele ya hadhara ku ya Umoja wa mataifa October mwaka huu mjini New York.

Ndege zisizokuwa na rubani Mashariki ya Kongo

Kämpfe Ost Kongo Rebellen Flüchtlinge
Vikosi vya serikali vikiwasaka waasi mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya KongoPicha: Reuters

Wakatai huo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeruhusu ndege hizo hizo ziisizokuwa na rubani zitumike kuchunguza nyendo za wanamgambo mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Risala ya mwenyekiti wa baraza la usalama kwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ,inazungumzia juu ya kutumiwa-"ikihitajika" ndege hizo, ili kurahisisha shughuli za vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa katika eneo la mashariki la jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman