1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa zamani wa FDLR wahukumiwa

28 Septemba 2015

Mahakama ya Ujerumani, imewahukumu adhabu ya vifungo vya muda mrefu jela, raia wawili wa Rwanda, waliokuwa viongozi wa waasi baada ya kupatikana na hatia ya kupanga mauaji mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/1Gea9
Ignace Murwanashyaka
Ignace MurwanashyakaPicha: picture-alliance/dpa/MDR/Fakt

Jaji wa mahakama hiyo, Juergen Hettich ameiambia mahakama kuwa Ignace Murwanashyaka, kiongozi wa zamani wa kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda-FDLR, amehukumiwa leo kifungo cha miaka 13 jela, huku msaidizi wake Straton Musoni, amehukumiwa kifungo cha miaka minane jela.

Akizungumza na mahakama baada ya kesi hiyo iliyodumu kwa muda wa saa nne, Jaji Hettich amesema viongozi hao wa zamani wa waasi walikuwa wakipanga mauaji hayo wakiwa nchini Ujerumani.

Amesema kesi hiyo sio ya kisiasa, bali kesi ya jinai kwa kuzingatia umuhimu wake. Hata hivyo, hukumu hiyo haijakidhi matakwa ya waendesha mashtaka waliokuwa wanataka Murwanashyaka ahukumiwe kifungo cha maisha gerezani, bila ya kuwepo uwezekano wa kuachiliwa huru baada ya miaka 15, kama ilivyo kawaida kwa mfumo wa kisheria wa Ujerumani. Aidha, walitaka Musoni ahukumiwe kifungo cha miaka 12 jela.

Murwanashyaka na Musoni ambao wameishi Ujerumani kwa zaidi ya miaka 20, walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 26 ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu na makosa 39 ya uhalifu wa kivita uliofanywa na wanamgambo wa FDLR chini ya uongozi wao kati ya Januari 2008 hadi walipokamatwa Novemba mwaka 2009.

Mwanzoni mwa kesi hii, mwendesha mashtaka wa serikali, Christian Ritscher alisema Murwanashyaka aliamuru mauaji ya zaidi ya watu 200 na idadi kubwa ya watu kubakwa na wanajeshi wake na kwamba aliwatumia raia kama ngao ya kujikinga na aliwapeleka wanajeshi watoto katika eneo la mapambano, mashariki mwa Kongo.

Kesi ya aina yake

Kesi hii ni ya kipekee kutokana na kuwa ya kwanza kutumia kanuni za Ujerumani za uhalifu dhidi ya sheria za kimataifa. Tangu ilipoanzishwa mwaka 2002, sheria hiyo inaruhusu kuwahukumu watu kwa makosa ya uhalifu wa kivita na ukiukwaji wa haki za binaadamu wakiwa nje ya nchi zao.

Straton Musoni
Straton MusoniPicha: picture-alliance/dpa/B. Weissbrod

Mwanasheria wa Murwanashyaka, Ricarda Lang, amesema mteja wake hausiki na tuhuma zinazomkabili na anataka aachiliwe huru. Akihojiwa na DW mwezi uliopita, Lang alisema mteja wake hakuwa na namna yoyote ya kuzuia uhalifu huo.

Hadi alipokamatwa mwaka 2009, Murwanashyaka alikuwa akiishi kwenye mji wa Ujerumani wa Mannheim, ambako alikuwa akiepuka sana kujulikana na umma.

Musoni ambaye ni msaidizi wa Murwanashyaka, pia anatuhumiwa kutoa amri kwa kundi la kijeshi la FDLR, akiwa nchini Ujerumani, kwa njia ya simu za satelaiti, ujumbe mfupi wa maandishi pamoja na baruapepe.

Hukumu hiyo imepongezwa na kuonekana kama hatua moja mbele, baada ya Umoja wa Mataifa kurudia wito wake kwa Baraza la Usalama kuwafikisha makamanda wa FDLR kwenye vyombo vya sheria vya nchi za nje.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DW
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman