1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hukumu ya Karlsruhe juu ya Hartz IV

10 Februari 2010

Mahkama ya katiba ya Ujerumani yadai Hartz IV ifanyiwe marekebisho.

https://p.dw.com/p/Lxlo

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo, hii takriban yote yamechambua hukumu iliopitishwa jana na Mahkama Kuu ya Katiba mjini Karlsruhe, juu ya kesi iliofikishwa mbele yake i kuwa , malipo yanayoitwa "HARTZ IV" kwa familia zenye mapato ya chini, hayatoshi kwa hata ulezi wa watoto wao.

Gazeti la Flensburger Tageblatt kuhusu hukumu hiyo laandika:

Hukumu ya Karlsruhe, inaonesha dhahiri-shahiri ni tatizo gani wanasiasa wanakabiliwa nalo wakati huu.Tatizo hilo, halilingani na ukweli wa maisha yalivyo na hii si haki.Badala ya kutunga mikakati kuipunguzia serikali mzigo na kuvumbua njia mpya za kutia mapato,serikali imekimbilia kutunga sheria kali kama hiyo.Kwa njia hiyo, kunaibuka sheria upande huu na kanuni upande ule.Viraka sasa vinatiwa katika sheria mpaka hakuna nafasio tena .

Na hivyo ndivyo ilivyotokea katika kuhesabu malipo ya HARTZ IV. Kile kinacho takikana sasa, ni kuonesha ujasiri na kutunga mikakati mipya pamoja na kuachana na miko yote: mfano, je, haifai sasa kuzingatia kutoza tena kodi za mali,kuongeza kodi ya urithi,kutoza kodi ya mapato kutoka masoko ya hisa au hata kuanzisha ada za mshikamano na watoto ?

Ama gazeti la Westfalen-Blatt, likiendeleza mada hii ya "Hartz IV "laandika kwamba, Mahkama ya Katiba haikukata hukumu ya kusangaza lakini ni ya busara. "Mambo hayawezi kwenda namna hivyo" ndivyo walivyoamua mahakimu na kudai sheria hiyo idurusiwe tena bungeni na ni barabara kufanya hivyo.Gazeti Laongeza:

"Kwani,sheria hiyo irudi Bungeni kudurusiwa tena.Kwani, mara nyingi wanasiasa huiachia Mahkama ya Karlsruhe, kurekebisha dosari zake.Nasaha njema sasa ni ghali kuipata na wakati unapita na matokeo hayajulikani.Serikali ya muungano ya Ujerumani ya CDU/CSU na FDP inakabiliwa na mzigo mzito ambao inabidi kuthibitisha inaweza kuubeba ."

Dola linalowahurumia wanyonge , linapoteza sasa imani yake hata tu likiruhusu tu kutiliwa shaka kwamba, halijali hali za watoto wa wanyonge. Hivyo ndivyo gazeti la Frankischer Tag linavyosema na kuongeza:

Dhara hii, ina athari kubwa.....kutochukua sasa hatua kurekebisha mambo,kutawapigia upatu wafuasi wenye siasa kali za mrengo wa shoto kutembeza sera zao.Kuonesha dhamana kwa wanyonge katika jamii , kunatoa sura nyengine kabisa na hata busara ya kisiasa.

STUTTGARTER NACHRICHTEN, laandika kwamba, serikali ya muungano ya Ujerumani, inapaswa sasa kuchunga ili mwanya wa mishahara na ujira inayotolewa, isiwe mkubwa zaidi kuliko ilivyo hadi sasa.Vyama vya wafanyikazi,chama cha kijamaa cha SPD na kile cha Linke cha mrengo wa shoto zaidi, hufanya mambo ni rahisi hivyo vinapodai kuwekwa kima cha chini kabisa cha mishahara kote nchini.Kwani, laandika gazeti:

" Spain,Itali na Ugiriki ,ni mifano inayobainisha nini kinatokea pale kima cha mishahara kikipanda bila ya kulingana na uzalishaji viwandani.Viwanda hushindwa kushindana na viwanda vyengine.Kuajiri mfanya kazi, huwa ghali na uchumi katika sehemu mbali mbali za bahari ya Meditteranian umeporomoka chini.Hali kama hiyo, yapaswa kuzuwiwa isitokee Ujerumani."

Mwandishi: Ramadhan Ali/DPA

Uhariri: Abdul-Rahman