1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hukumu ya kesi Bemba kutolewa Jumatatu

20 Machi 2016

Jumatatu (21.03.2016) mahakama ya uhalifu ya kimataifa hatimae inatarajiwa kutangaza hukumu kwa kesi inayomkabili Jean Piere Bemba ya uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binaadamu Jamhuri ya Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/1IGfK
Jean-Pierre Bemba akiwa katika mahakama ya uhalifu ya kimataifa mjini The Hague. (29.09.2015)
Jean-Pierre Bemba akiwa katika mahakama ya uhalifu ya kimataifa mjini The Hague. (29.09.2015)Picha: Reuters/P. Dejong

Zaidi ya miaka 14 imepita tokea Jean Pierre Bemba makamo wa rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na vikosi vyake walipoiteremshia balaa Jamhuri ya Afrika ya Kati.Mwishoni mwa mwaka 2002 Bemba aliwatuma wanajeshi wake wanaofikia 1,500 kuvuka mpaka na kuingia Jamhuri ya Afrika ya Kati kumsaidia Rais wa wakati huo Ange-Felix Patasse kuzima jaribio la mapinduzi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka wapiganaji wa Bemba walijihusisha na uhalifu mbaya kabisa wa kivita kwa miezi kadhaa wakati wakiwa nchini humo. Mawakili wa Bemba wanapinga vikali madai hayo. Wanasema mteja wao hakuwa na mamlaka ya moja kwa moja kwa kikosi hicho wakati wa kutendeka kwa uhalifu huo na kwamba wahusika walikuwa ni wanamgambo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kuhakikisha kwamba mashahidi wanakubaliana na maoni hayo Bemba na mawakili wake walitumia ushawishi mkubwa kutaka kusaidiwa.Katika mashtaka ya pili Bemba na mawakili wake wanne wanatuhumiwa kuwahonga mashahidi kwa kutumia ushahidi wa uwongo.Inaelezwa kwamba Bemba akiwa kwenye chumba chake gerezani mjini The Hague Uholanzi ameunda mtandao kamili wa hongo.

Bemba gerezani

Bemba amekuwa kizimbani tokea mwaka 2008. Ubelgiji ndio iliowasilisha katika mahakama ya uhalifu mjini The Hague hati ya kukamatwa kwa Bemba.Miaka miwili baadae jaji alifunguwa kesi hiyo na ushahidi wa mashuhuda kuanza kusikilizwa kwa urefu. Hapo mwaka 2014 mahakama ilikamilisha mchakato huo na tokea wakati huo Bemba amekuwa akisubiri hukumu.

Jean-Pierre Bemba na wafuasi wake mjini Kinshasa 2006.
Jean-Pierre Bemba na wafuasi wake mjini Kinshasa 2006.Picha: AP

Andreas Mehler mkurugenzi wa taasisi ya Arnold Bergstrasser ilioko Freiburg hapa Ujerumani anasema ikiwa mchakato wa kesi hiyo hautafanyika haraka jukwaani ni suali la kutiliwa mashaka iwapo wahanga hao wa zamani watakuwa na muda kuwahi hukumu. Ni mzigo mzito sana kwa wahanga kwa kuzingatia mambo yote mawili kiakili na rasilmali.Katika nchi yenyewe ya Afrika ya Kati wananchi hawakuizingatia sana kesi hiyo.Operesheni hiyo imetokea miaka 14 iliopita na tokea wakati huo kumetokea vita vya wenyewe kwa wenyewe na kwa mara nyengine tena ukiukaji mkubwa sana wa haki za binaadamu.

Kwa kweli mahakama hiyo ya uhalifu ya kimataifa inatakiwa izuwiye ukiukaji mpya wa haki za binaadamu na uhalifu wa kivita. Mehler anasema lakini kwa vyo vyote vile hali hiyo haikujitokeza wakati wa kesi ya Bemba.

Kabila afaidika na kesi ya Bemba

Mtu ambaye wa kufurahia kesi hiyo kuchukuwa muda mrefu kwa hakika ni mpinzani wa Bemba ambaye ni Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.Picha: Reuters

Hapo mwaka 2006 Bemba alichuana na Kabila katika uchaguzi wa rais.Bemba alishindwa katika uchaguzi huo na kwenda kuishi uhamishoni barani Ulaya hapo mwaka 2007 ambapo alikuja kukamatwa mwaka mmoja baadae.Ukweli kwamba Bemba kwa muda mrefu amekuwa hayuko katika siasa za kitaifa kunamweka katika nafasi nzuri sana kwenye wizani Bw. Kabila anasema hayo Mehler.

Wakati wananchi Jamhuri ya Kati takriban hawakushughulishwa kabisa na kesi ya Bemba Wacongomani wanaisubiri kwa shauku kubwa hukumu ya Jumatatu.Mwanasheria wa Congo Eugene Bakama Bope anasema hiyo ni hukumu muhimu kwa kuangalia kilioko mashakani nchini Congo.Hapo mwezi wa Novemba uchaguzi unatarajiwa kufanyika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na ambapo kuachiliwa huru kwa makamo huyo wa zamani wa rais kunaweza kwa mara nyingine tena kutimiza dhima muhimu.Pale tu kutakapokuwa na ushahidi kwamba serikali ya Congo ilikuwa na mkono wake katika kukamatwa kwa Jean Pierre Bemba mtu anaweza kusema Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa inatumika kama zana na wale walioko madarakani.

Mahakama za ndani ya nchi zinaweza kuwa mbadala wa mahakama ya uhalifu ya kimataifa ambapo kesi zake huchukuwa muda mrefu.Wote wawili Mehler na Bope wanakubaliana kwamba wakati umefika kwa mahakama za Afrika kuimarisha mifumo yao ya sheria kushughulikia uhalifu unaotendeka katika ardhi yao.

Mwandishi :Hilke Fischer /Mohamed Dahman

Mhariri : Mohammed Khelef