1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hukumu ya "magaidi wa Sauerland"

5 Machi 2010

Je, hukumu iliotolewa imestahiki ?

https://p.dw.com/p/MKmf
Washtakiwa 4 wa kundi la Sauerland.Picha: AP

Ile kesi ya magaidi wanne walioitwa "kundi la Sauerland", ilimalizika jana hapa Ujerumani.Magaidi hao wanne, walipewa adhabu ya vifungo vya muda mrefu korokoroni.Kesi yao ilidumu miezi kumi, ilichukua vikao 65 na ilijumuisha madaftari 600 ya kurasa 1,700.

Kesi hii haikuwa ya kawaida. Washtakiwa ni vijana 4 kutoka Ujerumani ambao walijiunga na vita vya Jihad na ambao walijitolea kupigana na makafiri humu nchini. Jinsi walivyozibwa macho, walivyojaa chuki, walijitolea kuwahilikisha wanadamu wenzao 100-150 na hata zaidi. Yastaajabisha lakini, kuona hawajui mengi juu ya Uislamu wenyewe.

Msako wa Polisi ulikuwa mkubwa, kwni, kiasi cha askari 600 wakiwaandama na kamwe hawakuwapa washtakiwa hao upenu. Katika kipindi hicho ingelikuwa balaa kubwa laiti pangekuwapo kundi jengine la kigaidi lilokuwa likiandaa njama nchini Ujeruimani. Kwani, laiti lingekuwapo,basi uwezo wa vyombo vya usalama usingeweza kulishughulikia.

Hata kesi yenyewe ilichukua muda mrefu ,kinyume na kawaida, mbele ya Mahkama Kuu ya jiji la Dusseldorf. Katika siku ya 15 ya vikao vya kesi hii, washtakiwa waliamua kuungama madhambi yao. maelezo yao yakamurika mapya juu ya muundo wa ugaidi ulimwenguni. Kwani, sasa tunajua vipi chipukizi wapya wa vita vya Jihad wanavyo penyezwa katika kambi za mafunzo na vipi katika kambi hizo wanavyo andaliwa kwa mashambulio.

Ilipojadiliwa Bungeni iwapo kuwapo katika kambi kama hizo yatosha tu kuwa mhalifu wa sheria,kuliibuka wasi wasi iwapo hapo pia ni kumuadhibu mtu kwa mawazo yake. Kesi hii imebainisha baadhi ya mambo dhahiri-shahiri. Imeanika wazi kuwa, yule anaekwenda kwenye kambi hizo na kujipatia mafunzo, haendi kwa darasa. Kwani, huyo amejitolea kufundishwa vipi kuua.

Vijana hao wanne wameelezea jinsi walivyokulia hapa Ujerumani na kuteleza hadi kuingia katika mandhari ya magaidi wa kiislamu. Walikuwa katika misukosuko katika familia zao na hivyo wakapoteza muelekeo. Hawakujua tena nini haki nini dhuluma. Nini sawa nini si sawa.

Mwishowe, hali isio ya kawaida pia, ni jinsi gani washtakiwa hao wanne walivyokuja kubadilika mawazo : watatu kati yao bila ya kuchelewa ,waliikubali hukumu waliopitishiwa. Wanne alitaka kuilalia alao usiku mmoja kabla kuikubali au kuikataa.Walipewa vifungo tofauti vya miaka kadhaa gerezani. Na kwa jicho hilo , jungu walilopika,hukumu waliopitishiwa imestahiki.

Mwandishi: Jöris,Paul-Elmar /WDR

Mtayarishi: Ramadhan Ali

Uhariri: Miraji Othman