1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Human Right Watch limetoa ripoti yake ya mwaka huu.

14 Desemba 2009

Imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kumaliza ukatili Mashariki ya Kongo

https://p.dw.com/p/L239
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja Mataifa wakisimamia usalama katika moja ya mitaa ya jiji la Kinshasa nchini KongoPicha: AP

Shirika la Haki za Binadamu-Human Rights Watch limetoa ripoti yake juu ya hali ya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyoendelea kushamiri mashariki mwa Kongo, ambapo limelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka za kuwalinda raia wasiathirike zaidi kutokana na ukatili unaofanywa na serikali na vikosi vya waasi, na kuhakikisha kuwa wanajeshi wa kulinda amani hawajiingizi katika vitendo vya uhalifu.

Ripoti hiyo yenye kurasa 183, iliyopewa kichwa cha habari" Mtaadhibiwa: Mashambulio kwa Raia Mashariki ya Kongo," imetoa maelezo ya kina juu ya kuuawa kwa makusudi kwa raia 1,400 kati ya mwezi Januari na Septemba 2009, wakati wa operesheni mbili za kijeshi zilizofuatana dhidi ya wanamgambo wa kihutu wa Rwanda, wa Democratic Forces for Liberation of Rwanda (FDLR).

Ripoti hiyo imetuama zaidi katika mipango 23 ya uchunguzi wa shirika hilo mwaka huu, na kuwahoji waathirika 600, mashahidi na wanafamilia.

Mtafiti wa ngazi ya juu wa shirika hilo Anneke Van Wounderberg, alisema kuwa mauaji na vitendo vya ubakaji vinavyoendelea mashariki ya Kongo, vinaonesha kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linahitaji mkakati mpya wa kuwalinda raia, na akaongeza kuwa Baraza hilo linatakiwa lipeleke kundi la wataalam nchini Kongo na kuanzisha mpango madhubuti wa kuwalinda raia.

Ripoti hiyo imesema jeshi la Kongo na waasi wa FDLR waliwashambulia raia kwa kuwatuhumu kuwa ni wasaliti, wakawaua kwa kuwakata na mapanga.

Wanajeshi na waasi hao waliwafyatulia risasi raia waliokuwa wanajaribu kuyakimbia makaazi yao, au kuwachoma moto wakiwa majumbani mwao.

Kwa mujibu wa mashuhuda, baadhi ya wahanga walifungwa kamba kwa pamoja kabla ya kuchinjwa kama kuku, ambapo sehemu kubwa ya wahanga hao ni wanawake, watoto na wazee.

Human Rights Watch imependekeza kuundwa kwa kitengo cha wataalamu watakaoshughulia masuala ya kuwalinda raia, ambao watachukua hatua mahsusi za kuboresha mbinu za usalama wa raia mashariki ya Kongo.

Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa nchini Kongo Alan Doss, atalihutubia Baraza la Usalama la umoja huo mnamo Desemba 16 mwaka huu, ambapo pia Baraza la Usalama litapiga kura ya kurefushwa muda wa Vikosi vya Umoja wa Mataifa vya Kulinda Usalama, (MONUC), nchini Kongo mnamo Desemba 21.

Pia shirika hilo limevihimiza vikosi vya kulinda amani kuacha kushiriki katika operesheni zote za kijeshi zinazoendelea hivi sasa, hadi pale tathimini ya jinsi ya kutekeleza operesheni hizo bila kuathiri sheria ya kimataifa ya haki za binadamu itakapokuwa tayari.

Human Rights Watch imetaka pia makamanda wanaojulikana kuwa wana rekodi za ukiukaji wa haki za binadamu waondolewe kwenye operesheni.

Katika kipindi cha miezi tisa ya mwanzo ya mwaka huu, Umoja wa Mataifa uliorodhesha zaidi ya kesi 7,500 za unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na wasichana katika maeneo ya Kaskazini na Kusini mwa Kivu, ikiwa karibu kuvuka idadi ya kesi zilizoorodheshwa mwaka mzima uliopita.

Mwandishi:Lazaro Matalange/HRW PRESS

Mhariri:Abdul-Rahman