1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Human Rights Watch: Watu 700 wameuawa Kongo

Jane Nyingi
7 Oktoba 2016

Shirika la Human Rights Watch  limesema wapiganaji wasiofahamika wamewaua karibu raia 700 katika mashambulizi  yaliyoanza  miaka miwili iliyopita wilaya ya Beni mashariki ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/2R1WG
Kongo Afrika Massaker Mann sitzt vor einer ausgebrannten Hütte
Picha: Getty Images/K.Maliro

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human rights Watch  limesema wapiganaji wasiofahamika wamewaua karibu raia 700 katika mfululizo wa mashambulizi  yaliyoanza  miaka miwili  iliyopita wilaya ya Beni  mashariki  mwa jamuhuri ya Kidemocrasi ya Kongo. Mauji  hayo yameendelea  licha ya kuwepo majeshi ya Kongo na walinda amani wa Umoja wa mataifa.

Shambulizi kubwa na la karibuni  lilifanyika mwezi Agosti mwaka huu  ambapo wapiganaji waliua karibu watu 40 na kuteketeza nyumba kadha katika mji wa Rwangoma uliojirani ya mji wa beni. Serikali ya Kongo na  walinda amani wa umoja wa mataifa wametakiwa kuibuka na mikakati mipya  ya kuwalinda wananchi hasa walioko mji wa Beni na kuhakikisha wanaohusika na mashambulizi hayo wanachukuliwa hatua.

Baada ya miaka miwili  ya mauji ya kikatili,wenyeji wa Beni  wanaishi kwa hofu  ya kutokea mashambulizi zaidi  na hata wamepoteza matuamini  kuwa kuna yeyote anaweza kuyamaliza mauji yanayoendelea. Watafiti wa shirika la  kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, wanasema ripoti za kuaminika  kutoka wanaharakati wa Kongo na pia kutoka shirika la Umoja wa mataifa  zinaonyesha kuwa wapiganaji wenye silaha wamewaua karibu raia 680 katika angalau mashambulizi 120 wilaya ya  Beni  tangu mwezi October mwaka 2014.
Waathirika na mashahidi walieleza jinsi washambuliaji hao walivyofanya  mauji hayo kwa kuwakatakata  kwa shoka  au mapanga hadi kufa  wahusika huku wengine wakipigwa risasi. Idadi ya wahanga huenda ikiwa  juu kuliko ilivyo sasa
Kufikia sasa haieleweki  wanaofanya  mashambulizi hayo. Serikali ya Kongo inalilaumu  kundi moja la waasi  ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake katika  eneo hilo, huku vyanzo vingine vikiyahusisha makundi mengine na hata maafisa wa kijeshi na baadhi ya mashambulizi.

DR Kongo Bevölkerung in Goma nach den Angriff der Hutu Rebellen
Watu wa Beni wanaishi kwa hofuPicha: Getty Images/AFP/K. Maliro

Mauaji yaendelea licha ya kuwepo wanajeshi


Ripoti hiyo ya Human Rights Watch  inatokana na tafiti tano zilizofanywa wilaya ya Beni tangu mwezi Novemba mwaka 2014, mahojiano ya zaidi ya waathirika 160 na  mashahidi waliyoyashuhudia mashambulizi hayo. Wengine waliohojiwa ni maafisa wa jeshi la kongo,Umoja wa mataifa,wale wa serikali  ya Kongo miongoni mwa wengine. Wakati wa Mahojiano hayo mvulana mwenye umri wa miaka 10 alieleza jinsi  alivyochukuliwa mateka wakati wa shambulizi la mji wa Rwangoma na alishuhudia mauji kadhaa. Wanajeshi wa Kongo na wale wa Umoja wa mataifa  walipelekwa eneo hilo  baada ya kumalizika mashambulizi na wauji wakiwa tayari wametoroka zamani.

 

Mwandishi:Jane Nyingi/Human Rights Watch Report
Mhariri:Yusuf Saumu