1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Human Rights watch yazishutumu nchi zenye nguvu duniani kuhusu Syria

Admin.WagnerD21 Januari 2014

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadaamu Human Rights Watch limezishutumu nchi zenye nguvu zaidi duniani kwa kushindwa kushinikiza kumalizika kwa maovu Syria na badala yake zinaangazia zaidi mazungumzo

https://p.dw.com/p/1AuQc
Picha: picture-alliance/dpa

Siku moja tu kabla ya kuanza kwa mkutano wa kimataifa wa kutafuta amani Syria unaofanyika nchini Uswisi,shirika la Human Rights Watch limetoa ripoti inayozishutumu vikali nchi zenye nguvu zaidi duniani ikianza na Marekani.

Ripoti hiyo ya kurasa 667 inasema Marekani imezingatia zaidi kuzileta pande mbili zinazozana pamoja kwa ajili ya mazungumzo ya kutafuta amani na kuyafumbia macho suala la kuubinya utawala wa Rais Bashar al Assad kusitisha mateso na dhiki na kuwachukulia hataua kali wanaofanya maovu hayo.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamau pia limezishutumu Urusi na China kwa kuulinda utawala wa Syria dhidi ya kuchukuliwa hatua madhubuti na umoja wa Mataifa kama kuwekewa vikwazo vya marufuku ya kuuziwa silaha.

Hatua za dharura zichukuliwa Syria

Mkurugenzi mkuu wa Human Rights Watch Ken Roth amesema hawawezi kusubiri hadi kufikiwe kwa mkataba wa amani ambao uwezekano wake unatiliwa shaka huku kiasi ya watu 5,000 wanakufa nchini Syria kila mwezi.

Rais wa Syria Bashar al Assad
Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: AFP/Getty Images

Human Rights watch linasema Marekani ina maslahi yake ya kibinafsi katika mzozo wa Syria katika kupinga kuwasilishwa kesi kwa mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu iliyoko The Hague kwa kuhofia kuwa kwa kufanya hivyo, itaibua athari za kisheria dhidi ya washirika wao Israel.

Roth amesema anatumai ripoti iliyotolewa wiki hii kuhusu mauaji ya wafungwa na jeshi la Assad itamshinikiza waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, kutangaza kukomeshwa mara moja kwa mateso kama alivyoshughulikia suala la matumizi ya silaha za kemikali mwaka jana karibu na mji wa Damascus iliyosababisha kuchukuliwa kwa hatua za haraka na jumuiya ya kimataifa.

Utawala wa Assad washutumiwa

Ripoti nyingine iliyotolewa hapo jana ambayo iliandikwa na waliokuwa waendesha watatu wa mashitaka ya uhalifu wa kivita inayojumuisha picha zinazothibitisha kuwa utawala wa Assad ulitumia mbinu ya mateso na mauaji dhidi ya wapinzani wao katika mzozo unaoendelea.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture alliance/Zumapress.com

Katika ripoti ya Human Rights Watch,kundi hilo linaoonyesha utofauti ulioko ya jinsi jumuiya ya kimataifa ilivyo wepesi kushughulikia mizozo barani Afrika kama wa Jamhuri ya Afrika ya Kati,Sudan Kusini na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo lakini haiupi uzingati huo huo mzozo wa Syria, ambao umedumu kwa miaka mitatu sasa.

Jumuiya ya kimataifa imekuwa ikifanya maamuzi ya dharura ili kutimiza wajibu wake wa kulinda maisha ili kuepusha mauaji ya halaiki kwa kutuma majeshi kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi katika nchi hizo za Afrika.

Mwandishi:Caro Robi/ap/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman