1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hungary yaanza kujenga uzio kwenye mpaka na Croatia

18 Septemba 2015

Hungary imesema uzio mpya umeanza kujengwa kwenye mpaka wake na Croatia, saa chache tu baada Croatia kufunga mpaka wake na Serbia baada ya kuzidiwa na idadi kubwa ya wakimzi katika siku zilizopita.

https://p.dw.com/p/1GYWh
Ungarn Grenze Polizeieinsatz gegen Flüchtlinge
Picha: picture-alliance/dpa/S. Ujvari

Akizungumza kwenye radio ya taifa siku ya Ijumaa, waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban alisema uzio huo ungekamilishwa ifikapo mwisho wa Ijumaa, katika eneo la urefu wa kilomita 41, ambako Hungary na Croatia hazitenganishwi na mto. Lakini haikubainika wazi, iwapo hatimaye uzio huo utamaliza urefu wote wa mpaka huo wenye kilomita 329.

Uzio wa kwanza uliojengwa na Hungary kuzuwia wakimbizi una urefu wa juu wa futi 11.4, na ulikamilishwa mapema wiki hii kwenye mpaka wake wa kilomita 175 na Serbia. Tangu kukamilishwa kwa uzio huo, Hungary imewazuwia wakimbizi wote waliojaribu kuingia nchini humo, na iliwahukumu adhabu kali wote waliojaribu kuvuka kinyume na sheria.

Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban.
Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban.Picha: T. Charlier/AFP/Getty Images

Hatua hizo mpya kali zilisababisha makabiliano kati ya polisi na wandamanaji siku ya Jumatano, wakati maafisa walipotumia gesi ya kutoa machazi na maji dhidi ya kundi la waandamanaji na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa.

Vizuwizi hivyo vya Hungary viliwalaazimu wahamiaji kubadili njia na kuanza kupitia Croatia ambako polisi imesema leo kuwa tangu siku ya Jumanne, watu 13,000 wameingia nchini humo kinyume na sheria wakitokea Serbia.

Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad amekosoa hatua hizo zinazochukuliwa na Hungary, na kuzitaja kuwa za ubaguzi na zenye mwelekeo wa chuki dhidi ya Waislamu na wageni.

Wakati huo huo, Croatia imekata kuwachukuwa wahamiaji waliokamatwa na Slovenia jana jioni, wakiwemo 150 walioshushwa kwenye treni inayofanya safari za kimataifa, hatua iliyosababisha kulaumiana kati ya viongozi wamataifa hayo mawili.

Waziri mkuu wa Croatia alisema Umoja wa Ulaya laazima ufahamu kuwa nchi yake siyo mahala pa kukusanyia wakimbizi na kutangaza kile alichokiita "Plan B" ambayo itahusisha kutosajiliwa tena kwa wakimbizi wanaoingia nchini humo.

Hollande kuhimiza ufadhili kwa Uturuki

Rais wa Ufaransa Franocois Hollande, alisema jana baada ya mkutano na waziri mkuu wa Italia kuwa Umoja wa Ulaya laazima ushirikiane na Uturuki kuhakikisha kwamba wakimbizi walioko nchini humo wanabakia na kufanya kazi huko, na kupatiwa rasilimali zote wanazozihitaji kusubiri hadi hali itakapotengama nchini Syria.

Wakimbizi wakiwa kwenye treni kwenye mji Dobova, mpakani mwa Croatia na Slovenia.
Wakimbizi wakiwa kwenye treni kwenye mji Dobova, mpakani mwa Croatia na Slovenia.Picha: Getty Images/AFP/J. Makovec

Uturuki ilisema Ijumaa kuwa tayari imetumia kiasi cha dola bilioni 7.6 kuwahudumia wakimbizi wapatao milioni 2.2 tangu ulipoanza mgogoro wa kivita nchini Syria. Naibu waziri mkuu wa nchi hiyo, Numan Kurtulmus alitoa matamshi hayo wakati waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, akijiandaa kufanya ziara nchini Uturuki kujadili mzozo wa Syria.

Naibu wa kansela na waziri wa uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel, amesema katika mahojiano na gazeti la kila siku la Bild, kwamba mataifa yasiyoshiriki maadili ya pamoja ya hisia za wengine na mshikamano wasitegemee kupokea fedha kutoka jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

Gabriel amesema wakati Ujerumani ikijenga shule, kambi na makaazi kwa ajili ya familia za wakimbizi, mataifa mengine yalikuwa yanatandaza tu senyenge kwenye mipaka yake na kufunga milango yake, matamshi ambayo yalionekana kuelekezwa kwa Hungary, ambako polisi wameonekana wakiwashambulia wakimbizi kwa gesi za kutoka machozi na maji ya kuwasha.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe

Mhariri: Daniel Gakuba