1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huwezi kumpa demokrasia mtu kama vile unavompa mgonjwa dawa ya kifua.

11 Septemba 2007

Mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11. mwaka 2001 yalisababisha mshangao na fazaa, hasa kwa Ulimwengu wote wa nchi za Magharibi. Yale mafungamno yalioahidiwa na wanasiasa kupambana na ugaidi zamani yamesahauliwa. Na hasa tangu pale Marekani ilipoanza kuendesha vita katika Iraq pamezuka mabishano makali katika miji mikuu ya nchi hizo za Magharibi juu ya vipi kuing’oa mizizi ya siasa kali za ugaidi wa Kiislamu.

https://p.dw.com/p/CH8H
Rais George Bush wa Marekani akiweka shada la mauwa katika Uwanja palipokuweko Kituo cha Biashara Duniani, New York, kilichoshambuliwa na magaidi wa al-Qaida miaka sita iliopita.
Rais George Bush wa Marekani akiweka shada la mauwa katika Uwanja palipokuweko Kituo cha Biashara Duniani, New York, kilichoshambuliwa na magaidi wa al-Qaida miaka sita iliopita.Picha: AP

Demokrasia haiwezi kupewa mfumo wa kijamii unaokosa jambo hilo kama vile unavompa mtu dawa ya kifua pale anaposhikwa na mafua. Rais George Bush wa Marekani aliamini baada ya mashambulio ya Septemba 11, mwaka 2001 kwamba ataweza kuziongoza kwa haraka baadhi ya nchi za Kiislamu kuelekea mfumo wa kisiasa kama ule wa nchi za Magharibi. Na ikiwezekana kufanya hivyo, hata kwa kutumia nguvu. Miaka sita baada ya kujaribu kufanya hivyo, yaonesha jambo hilo limeshindwa. Haipiti siku ambako hakuna mtu asiye na hatia kuripuliwi kwa bomu huko Iraq. Hakuna siku inapita ambapo hakutokei mapigano ya kumwaga damu huko Afghanistan. Bado Marekani inajaribu kutafuta jibu mujarabu kwa mashambulio ya Setemba 11.

Na juu ya mkorofi wa hayo mashambulio ya kigaidi, Osama Ben laden? Hata kama hasimu huyo mkubwa akipatikana, hiyo haitokuwa mwisho wa mtandao wa al-Qaida. Ben Laden alisomea uchumi, na jambo hilo linahusiana sana na kujifunza namna ya kuunda jumiya. Mtandao wake wa kigaidi zamani umeshaingia katika nchi kadhaa, kutoka Bosnia hadi Yemen na Pakistan na hadi kufikia Indonesia. Al-Qaida imejizatiti katika hali zote, ina fedha nyingi na watu wengi. Mtandano huo wa kigaidi hauna makao makuu, hivyo inakuwa taabu kupambana nao.

Al-Qaida inajidai kuzungumza kwa niaba ya Waislamu wote wa dunia. Jee watu wanaweza kukingwa na ugonjwa wa itikadi kali za kidini? Na ikiwa ndio, basi kwa namna gani? Japokuwa, watekelezaji wa mashambulio ya Septemba 11 na washukiwa waliokamatwa karibuni hapa Ujerumani hawo hawamo katika hao watu wa kukingwa. Itikadi kali za kidini zinapamba moto pale watu wanapolazimishwa waishi katika umaskini na kutokuwa na mustakbali. Itikadi kali za kidini zinapata nguvu pale watu wanapokuwa na ukosefu wa elimu. Majeshi ya Kimarekani hayapigani dhidi ya umaskini au ujinga katika nchi za Kiislamu, hayashughulikii hata kidogo juu ya usalama. Na Huko Iraq, Afghanistan na katika nchi nyingine za Kiislamu, hisia za kuipinga Marekani zinazidi kupata nguvu.

Kwa kuishambulia Marekani, Bin Laden ameanzisha mabadiliko. Wenye dhamana za kisiasa kote duniani wanatambua wazi kwamba nchi nyingi za Kiislamu zimeelemewa na mizigo. Nchi hizo hazimudu kuwapatia nafasi za kazi na mkate makundi ya vijana wake wengi. Chumi katika nchi zenye mila za Kiislamu sio zenye kuendeleza mashindano ya kibiashara, tawala katika nchi hizo zinakula rushwa na fisadi. Wengi wa watawala wa nchi hizo wanahisi watakula hasara kutokana na mashindano yanayozidi kuwa makali. Ni nchi chache za Kiislamu zinazoogolea katika fedha zinazotokana na kusafirisha mafuta ngambo. Na hata katika nchi hizo watu wanazidi kutoridhika na hali ya kisiasa na ya kijamii.

Dunia inazidi kuwa ngumu kutokana na utanda wazi tunoushuhudia hivi sasa, angalu hivyo ndivyo inavosemwa na vyombo vya habari. Watu zaidi na zaidi wana hamu ya kupata majibu rahisi juu ya matokeo ya dunia ambayo huwezi kuyafikiria na ambayo hayatoi picha ilio wazi. Watu wanaoangalia mambo na kuyapa tu majina mawili, nyeupe au nyeusi, pamoja na wale wenye kupayuka, miongoni mwao wakiwemo viongozi wa kidini, wanafuatwa na makundi ya watu. Kwa bahati mbaya, mamilioni ya watu wanawaamini. Kazi ya kuwafahamisha wat ni ngumu na inachukuwa wakati. Wanasisa wengi, akiwemo pia George Bush, wanafikiri kwamba kutumia nguvu watafikia mafanikio ya haraka. Ukweli unaoonesha, lakini, kwamba demokrasia huwezi kuiamarisha kwa mgonjwa kama vile kuamrisha kunywa dawa au kupiga chanjo.