1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huyu ndiye rais mpya wa Somalia

11 Septemba 2012

Wabunge wa Somalia wamemchagua Hassan Sheikh Muhamud kuwa rais mpya wa nchi hiyo baada ya miongo zaidi ya miwili ya kutokuwa na serikali kuu. Je, rais huyo mpya ni mtu wa aina gani?

https://p.dw.com/p/166ZL
Rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud
Rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh MohamudPicha: picture-alliance/dpa

Hassan Sheikh Mohamud ni mtu asiyejulikana sana nje ya Somalia. Mwanadiplomasia mmoja wa nchi za Magharibi amesema kuwa katika nchi hizo kiongozi huyo hajulikani sana.

Sheikh anatokea kwenye asasi za kiraia na ana uhusiano na Al-Islan, mshabaha wa jumuiya ya Udugu wa Kiislamu. Mwanadiplomasia huyo ameeleza kuwa ni katika muda wa siku mbili tu zilizopita, ndipo watu wa nje walipoanza kusikia mengi juu yake.

Katika medani za usomi na mashirika yasiyo ya kiserikali, Hassan Sheikh Mohamud anatambulika kuwa mwasisi mwenza wa taasisi ya maendeleo ya usimamizi na utawala, SIMAD na anaheshimika kama mtaalamu wa masuala ya elimu.

Taasisi ya SIMAD ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba nchi ya Somalia iliyoathirika vibaya sana na vita, inapata wasimamizi na watawala wa kutosha.

Historia ya Sheikh

Hassan Sheikh Mohamud alizaliwa mnamo mwaka wa 1955 katika mkoa wa kati nchini Somalia, Hiran. Na yeye, sawa na Rais wa hapo awali Sharif Sheikh Ahmed anatoka katika ukoo maarufu wa Haweyi ambao ni mkubwa kabisa katika jiji la Mogadishu.

Rais Sheikh akiwa katikati ya waliokuwa wagombea wengine wa urais wa Somalia.
Rais Sheikh akiwa katikati ya waliokuwa wagombea wengine wa urais wa Somalia.Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa tovuti ya chama chake cha kisiasa alichokiunda mwaka uliopita, rais huyo mpya anayo tajiriba ya miaka 20 katika masuala ya elimu na utatuaji wa migogoro.

Hassan Sheikh Mohamud alisoma kwenye Chuo Kikuu cha Taifa nchini Somalia kabla ya vita kuanza mnamo mwaka wa 1991 nchini humo. Baadaye alienda India kufanya masomo kwenye Chuo Kikuu cha Bhopal.

Harakati zake

Hakuna mtu hata mmoja aliyewaza japo kutokea mbali kwamba Hassan Sheikh Mohamud angeliibuka mshindi wa uchaguzi. Kinachofahamika kwa watu wachache ni kwamba Rais huyo mpya aliwahi kufanya kazi kwenye Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) mnamo miaka ya kwanza baada ya aliyekuwa Rais wa Somalia, Siad Barre kutimuliwa.

Kijana wa Kisomali na bendera ya nchi yake.
Kijana wa Kisomali na bendera ya nchi yake.Picha: dapd

Mnamo mwaka wa 2009 Hassan Sheikh Mohamud alishiriki katika kuandika ripoti kwa ajili ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambapo alisisitisa umuhimu wa dhima ya Wasomali wanaoishi katika nchi za nje. Muhamud alihoji kwamba watu hao wanapaswa kutoa mchango wao katika ujenzi wa amani wa Somalia.

Tofati na wanasiasa wengi wa Somalia, rais mpya wa nchi hiyo hayumo katika jumuiya ya Wasomali waliotoka nje ya nchi yao. Hakuwahi kuwa waziri na ni hivi karibuni tu alipoingia katika ubunge.

Katika Ilani ya chama chake amesema kuwa anakusudia kuijenga Somalia isiyokuwa na siasa za kiukoo na jamii isiyokuwa na hofu ya wala migogoro ya ndani. Watu wanaomjua wamesema siasa zake ni za mrengo wa wastani, kwani aliwahi kufanya mazungumzo hata na al-Shabaab waliyoiruhusu taasisi yake ya SIMAD iendelee kufanya shughuli zake .

Chama chake cha kisiasa kinamwelezea rais huyo mpya wa Somalia kuwa mjenzi wa jamii ya kiraia nchini Somalia. Lakini kwa wanadiplomasia wa nchi za Magharibi, Hassan Sheikh Mohamud ni rais mpya asiyekuwa na uzoefu wa kisiasa na mtu asiyejulikana sana.

Mwandishi: Mtullya Abdu/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef