1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAEA yajikuta katika njia panda dhidi ya Syria

Aboubakary Jumaa Liongo13 Oktoba 2010

Shirika la Nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa IAEA limesema kuwa Syria imekuwa ikiweka vikwazo dhidi ya shirika hilo kuichunguza kuhusiana na shashaka kuwa nchi hiyo inajihusiska na shughuli za atomiki

https://p.dw.com/p/Pdcc
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Yukiya AmanoPicha: AP

Hata hivyo shirika hilo limesema kuwa linashindwa kwa sasa kuchukua hatua yoyote ikiwa ni kuepuka kuibuka kwa mvutano mpya mnamo wakati ambapo kuna mvutano unaendelea wa mpango wa nyuklia wa Iran na shirika hilo.

Ni zaidi ya miaka miwili sasa tokea Syria ilipowaruhusu wataalam wa shirika hilo la nguvu za atomiki la Umoja wa Mataifa kukifanyia uchunguzi kinu chake cha Alzour kilichoko jangwani kubaini iwapo kulikuwa na harakati za kinyuklia.Kiwanda hicho kililipuliwa na Israel mwaka 2007.

Taarifa za kijasusi za Marekani zilisema kuwa Syria ilikuwa ikifanya urutubishaji wa nyuklia kama ilivyo kwa Korea Kaskazini kwa nia ya kuzalisha malighafi inayotumika kutengeneza bomu la nyuklia.Lakini Syria kama ilivyo kwa mshirika wake Iran imekuwa ikikanusha shutuma hizo.

Marekani ilipendekeza kuwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, lipewe mamlaka ya kuichunguza Syria mahali popote kwa kutoa taarifa ya muda mfupi.

Lakini hata hivyo  Syria bila shaka huenda ikagoma kutoa ushirikiano huo, na hapo Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la IAEA Yukiya Amano atakuwa hana budi kuchagua kati ya mawili, kuongeza mafuta katika moto unaowaka au kukubaliana na kile kidogo ambacho ofisi yake inachoweza kukifanya kuhusiana na msimamo wa Syria.

Mark Hibbs kutoka taasisi inayojihusisha masuala ya amani ya kimataifa anasema Syria inaibuka mshindi katika vita hii na shirika la IAEA.Anasema kuwa kwa kuhofia mkwaruzano mwengine, Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Amani hayuko tayari kuwasilisha ombi kwa serikali ya Syria kutaka kufanya ukaguzi maalum kuhusiana na shutuma zilizotolewa na Israel pamoja na mataifa ya magharibi kwamba nchi hiyo inajenga kwa siri kinu cha nyuklia.

Hibbs amesema kuwa huku wakati ukiwa unazidi kwenda, itakuwa rahisi kwa Syria kutumia mwanya huo kuficha shughuli zozote haramu za kinyuklia, kitu ambacho mataifa ya magharibi yamekibaini na kukitilia shaka.

DALILI ZA URANIUM

Katika taarifa yake ya hivi karibuni kuhusiana na Syria, Shirika la Atomiki la Umoja wa Mataifa limesema kuwa  nchi hiyo imewazuia wachunguzi wake kwenda katika maeneo ambayo ni muhimu kwa uchunguzi wao.

Mapema mwaka huu shirika hilo liliupa uzito wasiwasi wa kuwepo kwa shughuli haramu za kinyuklia nchini humo kwa kusema kuwa wakaguzi wake katika uchunguzi wao waliyoufanya mwaka 2008 wamebaini kuwepo kwa madini ya Uranium katika maeneo yanayohusishwa na kuendelea kwa shughuli hizo za kinyuklia.

Katika mjadala wa wanachama 35 wa bodi ya shirika hilo mwezi uliyopita, Balozi wa Marekani Glyn Davies alisema kuwa nchi yake italiunga mkono shirika hilo kutumia njia zote kuendelea na uchunguzi wake huko Syria.

Lakini balozi wa Syria Mohammed Badi Khattab alisema kuwa hakuna haja ya kurejea tena katika kiwanda cha Dair Alzour kwani ilikwishathibitika kuwa hakihusiani na shughuli zozote za kijeshi.

Katika siku za nyuma Syria ilisema kuwa madini hayo ya Uranium yaliyokutwa kwenye kiwanda hicho, yalitokana na silaha ambazo Israel ilizitumia wakati ilipokishambulia kiwanda hicho, au labda zilidondoshwa kutoka angani, madai ambayo yanapingwa na mataifa ya magharibi.

Hata hivyo suala hilo la Syria limekuwa likigubikwa na mzozo wa mpango wa nyuklia wa Iran ambao mataifa ya magharibi yanadai ni hatua za nchi hiyo kutengeneza bomu la nyuklia, madai ambayo Iran inayapinga ikisema kuwa ni mpango kwa ajili ya matumizi ya kiraia.

Wanadiplomasia wanasema kuwa tofauti moja muhimu iliyopo kati ya suala la Iran na Syria, ni kwamba Iran bado inaendelea na urutubishaji wa madini hayo ya Uranium, wakati ambapo Syria kiwanda chake kilisambaratishwa na mashambulio ya Israel.

UKAGUZI MAALUM

Shannon Kile  kutoka taasisi inayojihusisha na utafiti wa masuala ya amani ya kimataifa yenye makao yake mjini Stockholm Sweden amesema ushahidi unaibua maswali mengi iwapo kama kweli Syria inakiuka makubaliano ya kimataifa kuhusiana na nishati ya nyuklia.Amesema kwa mtizamo wake jambo hilo linahitaji kufanyika kwa ukaguzi maalum.

Hatua yoyote ya aina hiyo huenda ikaikasirisha Syria ambayo uhusiano wake na Marekani imeimarika tokea kuingia madarakni kwa  Rais Barack Obama mwaka jana.

Iwapo Syria itakataa kufanyika kwa ukaguzi huo maalum, basi bodi ya shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki IAEA inaweza kupiga kura kulipeleka suala hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kama ilivyofanyika kwa suala la Iran miaka minne iliyopita.

Lakini hata hivyo Syria inaonekana kuwa huenda itaungwa mkono na baadhi ya nchi wanachama wa shirika hilo kutoka nchi zinazoendelea, lakini mataifa ya magharibi nayo yanategemewa kwa upande wao kuendelea na mbinyo zaidi.

Syria imewaruhusu wakaguzi wa shirika hilo la nguvu za atomiki la Umoja wa Mataifa kufanya ukaguzi katika kinu cha utafiti cha zamani mjini Damascus ambako wamekuwa wakiangalia iwapo kuna uhusiano wowote kati ya kinu hicho na kile cha Dair Alzour

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters

Mhariri:Mohammed Abdulrahman