1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC inatarajia kutoa uamizi kuhusu kukamatwa kwa Gaddafi

27 Juni 2011

Mahakama ya Kimatiafa ya Uhalifu wa Kivita,( ICC), leo hii ipo katika mchakato wa kuamua kama itatoa waranti ya kukamatwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.

https://p.dw.com/p/11k85
Kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: dapd

Mwezi Mei, mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo, Luis Moreno Ocampo, aliomba ridhaa ya kumkamata Gaddafi na wasaidizi wake wawili kwa uhalifu wa kibinadamu dhidi ya mahasimu wake.

Waandamanaji wanaoipinga serikali ya Libya, wamemtaka kiongozi hiyo ambae alitumia nguvu za kijeshi dhidi yao tangu kuanza kwa vuguvuvugu la kisiasa nchini humo katikati ya Februari kuondoka madarakani.

Mtangazaji wa televisheni ya Al Arabiya ameripoti kwamba Ocampo amewasilisha katika mahakama hiyo vielelezo 1,200, zikiwemo video na ushahidi mwingine kutoka kwa watu waliofungwa na kuteswa.

Aidha Imeripotiwa kwamba nyaraka zote hizo zinamoneshea kidole Gaddafi, mwanawe Saif al- Islam pamoja na Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Libya, Abdullah al-Senussi.

Wakati hatima hiyo ikisubiriwa huko mjini The Hague, nchini Uholanzi, mjini New York nchini Marekani, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafanya mjadala kuhusu hali ilivyo nchini Libya wakati mapambano yakiwa yanaendelea.

Hapo jana viongozi wa Afrika waliukaribisha uamuzi wa Gaddafi kujiweka kando katika mazungumzo ya kumaliza mgogoro wa nchi hiyo, ambao unaingia mwezi wa tano sasa, kati ya wanajeshi watiifu kwa Gaddafi na Waasi.

Libyen Kämpfe Rebellen
Mpiganaji muasi nchini LibyaPicha: AP

Milio ya makombora ya maroketi na silaaha nyingine nzito imesikika huko maeneo ya milimani ya Nafusa, kusini mashariki mwa mji wa Tripoli.

Jopo la upatanishi la Umoja wa Afrika, AU, kuhusu Libya, katika mkutano wa uliofanyika mjini Pretoria nchini Afrika Kusini, limesema Gaddafi hatoshiriki katika mazungumzo ya amani.

Hata hivyo, afisa mmoja nchini Afrika Kusini, ambae alizungumza kwa mashariti ya kutotajwa jina lake na Shirika la Habari la Ufaraansa, AFP, amesema walimtaka Gaddafi kutangaza hadharini uamuzi huo, lakini hakufanya hivyo.

Lakini awali katika ufunguzi wa mkutano huo, rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alishutumu tena NATO kwa kuvuka kikomo cha azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nchini Libya.

Katika ufunguzi wa mkutano huo nchini Afrika Kusini, Zuma alisema lengo halikuwa kufanikisha mabadiliko ya kiutawala au mauwaji ya viongozi.

Katika hatua nyingine, mawaziri watatu wa serikali ya Libya hivi sasa wapo nchini Tunisia kwa shabaha ya kufanya mazungumzo na vyama mbalimbali vya kimataifa yenye shabaha ya kumaliza mgogoro wa nchi hiyo.

Shirika la habari nchini Tunisia, TAP, limemtaja Waziri wa Afya, Mohammed Hijazi, na wa Ustawi wa Jamii, Ibrahim Sherif, wamewasili jana katika eneo la kitalii la Jeba, mahala ambapo mkutano huo unaendelea.

Mawaziri hao wanaungana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Abdelati al-Obeid,. ambae amekuwepo nchini Tunisia tangu jumatano iliyopita akizungumza na vyama mbalimbali.

Mwandishi: Sudi Mnette/DPA

Mhariri.Miraji Othman