1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC kuwataja watu sita waliofadhili ghasia za uchaguzi Kenya

15 Desemba 2010

Louis Moreno Ocampo atayatoa majina hayo katika mkutano wa waandishi habari, huko The Hague mwendo wa saa sita mchana saa za hapa Ulaya.

https://p.dw.com/p/QYmW
Luis Moreno Ocampo, kutoa taarifa muhimu kuhusu Kenya, saa sita mchana.Picha: AP

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Uhalifu, ICC ilio na makao yake mjini The Hague Uholanzi leo mchana atawataja watu sita, washukiwa wakuu wanaodaiwa walihusika na kufadhili machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya. Louis Moreno Ocampo baadaye ataitaka mahakama hiyo iwatolee watuhumiwa hao wito wa kufika mahakamani. Ocampo pia ametoa masharti kadhaa ikiwemo, baada ya kutajwa majina yao, watu hao sita watatakiwa kuwasiliana mara kwa mara na mahakama hiyo ya ICC.

Bwana Ocampo alisema iwapo washukiwa hao watakiuka masharti hayo, basi ataitaka mahakama hiyo ya ICC kutoa waranti wa kuwakamata. Mwezi Machi mwaka huu, Mahakama hiyo ya uhalifu ya ICC iliidhinisha uchunguzi uanzishwe kuhusiana na ghasia hizo za uchaguzi nchini Kenya baada ya kiongozi wa upinzani wakati huo Raila Odinga kudai kuwa Rais Mwai Kibaki alifanya hila katika uchaguzi huo uliomrejesha tena madarakani.