1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yaamuru uchunguzi dhidi ya Myanmar kuanza

Mohammed Khelef
15 Novemba 2019

Waendesha mashitaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague (ICC) wamepata ruhusa ya kuanzisha uchunguzi juu ya ukatili waliotendewa Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa Myanmar.

https://p.dw.com/p/3T7bW
Bangladesch Rohingya Flüchtlinge Cox’s Bazar | Protest gegen Rückführung
Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Yasin

Huu huenda ukwa ushindi wa awali wa Warohingya na wanaharakati wa haki za binaadamu ulimwenguni na pigo jengine kwa utawala wa Myanmar chini ya mtu aliyewahi kuwa alama ya mapambano ya haki na demokrasia duniani, Aung San Suu Kyi.

"Kuna sababu za kimsingi kuamini kuwa vitendo vya ghasia zilizoratibiwa kwa makusudi viletendwa ambavyo vinaweza kulingana na uhalifu dhidi ya ubinaadamu" ilisema taarifa kwa vyombo vya habari kutokea makao makuu ya mahakama hiyo mjini The Hague, Uholanzi.

Makhsusi kabisa, taarifa hiyo inagusia matukio kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar, ambako Umoja wa Mataifa umeituhumu serikali kuu mjini Rangoon kwa kuwahamisha kwa nguvu Warohingya waliokimbilia nchi jirani Bangladesh kwa dhamira ya kufanya mauaji ya kimbari kuanzia mwanzoni mwa mwezi Agosti 2017. 

Uamuzi huo wa ICC uliotolewa Alhamis (Novemba 14) ulisadifiana na na uliotolewa nchini Argentina, ambapo mahakama ya juu ilikubali kupokea ombi la jamii ya Rohingya na wanaharakati wa haki za binaadamu wa Amerika Kusini dhidi ya utawala wa Myanmar unaoongozwa na mshindi wa zamani wa Tuzo ya Amani ya Nobel na sasa kiongozi wa kisiasa wa Mnyanmar,  Bibi Aung San Sun Kyi. 

Wakitumia kipengele cha sheria za kimataifa kinachoipa mahakama ya Argentina haki ya kusikiliza shauri lolote la uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu bila kujali ulikotendeka, mwanasheria mashuhuri wa Argentina Tomas Ojea na Rais wa Jamii ya Warohingya wa Mnyamar nchini Uingereza, Tun Khin, walifungua rasmi kesi yao mjini Buenos Aires.

Myanmar yakabiliwa na kesi kila mahala

Kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi (katikati), analaumiwa kwa kutokulinda haki za Warohingya.
Kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi (katikati), analaumiwa kwa kutokulinda haki za Warohingya.Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/AP Photo/K. Sasahara

"Hivi sasa kuna wanajeshi ambao bado wapo gerezani kwa uhalifu walioutenda Uhispania chini ya Franco na wengine waliotenda uhalifu kama huo kwengineko pia. Kwa hivyo, naamini kesi hii italeta matokeo mazuri na tutasonga mbele," Tun Khin aliwaambia waandishi wa habari akiongeza kwamba kama walivyoshitakiwa na kufungwa wahalifu wengine ulimwenguni licha ya kwamba walitenda uhalifu huo katika mataifa ya mbali, anatazamia kuwa haki pia itatendeka kwao.

Haya yanajiri katika wakati ambapo kunaonekana kukiongezeka shinikizo la kisheria dhidi ya Myanmar katika majukwaa ya kimataifa. Kesi tafauti ilifunguliwa na Gambia siku ya Jumatatu kwenye Mahakama ya Haki ya Kimataifa, ICJ, iliyoko pia mjini The Hague. 

"Hii ni fursa kwa makosa ya kimbari yaliyotendwa dhidi ya Warohingya angalau kusikilizwa mahakamani, jambo ambalo Warohingya hawawezi kulipata ndani ya Myanmar wala kwenye kiwango cha kimataifa. Kwa hivyo, kwa njia hii wanasaka haki na ukweli kwa ajili yao ufahamike," alisema Wakili Ojea, licha ya kwamba sheria za Argentina hazihusiani na mashitaka ya mauaji ya kimbari.

Mchakato mwengine wa kisheria ulianza mwaka jana baada ya ICC kuwataka waendesha mashitaka kuanzisha uchunguzi wa awali nchini Bangladesh ambako takribani wakimbizi 700,000 wa Kirohingya wamekimbilia.

dpa, reuters