1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yaitaka Sudan kuruhusu wachunguzi kuwafikia mashahidi

Saumu Mwasimba
11 Desemba 2020

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya kushughulikia kesi za jinai ICC ameitolea mwito serikali ya Sudan kutekeleza wajibu wake kivitendo katika suala la kutafuta haki kwenye jimbo la Darfur.

https://p.dw.com/p/3maUn
Niederlande Den Haag | ICC | Internationaler Strafgerichtshof
Picha: Everett Collection/picture alliance

Mwendesha mashtaka wa ICC Fatou Bensouda ameitaka serikali ya Sudan kuonesha kwa vitendo uwajibikaji wake katika suala la haki kwa watu wa jimbo la Darfur, kwa kuanza na hatua ya kuwaruhusu bila ya vipigamizi,wachunguzi wa mahakama hiyo kuwafikia mashahidi, maeneo ulikofanyika uhalifu pamoja na ushahidi mwingine katika eneo hilo kubwa la magharibi mwa Sudan.

Katika maelezo yake mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa aliyoyatowa kwa njia ya vidio,Fatou Bensouda amesema kwamba hatilii shaka uaminifu wa maafisa wa ngazi za juu kutoka serikali ya mpito ya Sudan lakini amesisitiza kwamba suala la wachunguzi kuruhusiwa kuingia Darfur ndilo hasa wanalolitarajia wahanga,na ndicho kitu ambacho Sudan kwa uungaji mkono wa baraza la usalama inachopaswa kukisimamia.

Soma zaidi: Wasudan warejea nyumbani kuijenga nchi baada ya Bashir

Mgogoro katika jimbo la Darfur ulizuka baada ya waasi kutoka jamii ya wasudan weusi wenye asili ya kutoka nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara na Afrika ya kati,kuanzisha uasi mwaka 2003 wakilalamikia ukandamizaji wanaofanyiwa na serikali ya Sudan mjini Khartoum iliyohodhiwa na waarabu.

Serikali ya rais wa wakati huo Omar al-Bashir ilijibu uasi huo kwa kuanzisha kampeini kubwa ya mashambulizi ya anga ya mabomu na kupeleka wanamgambo waliofahamika kama Janjaweed katika eneo hilo. Inaarifiwa kwamba wanamgambo hao walifanya mauaji ya watu wengi pamoja na ubakaji.

Maelfu ya watu wameuawa na mamia ya wengine kuachwa bila makaazi rasmi

Niederlande Den Haag |  Fatou Bensouda Chefanklägerin Internationaler Strafgerichtshof (ICC)
Mwendesha mashtaka wa ICC Fatou BensoudaPicha: picture-alliance/AA/A. Asiran

Zaidi ya watu 300,000 waliuwawa na wengine milioni 2 na laki 7 waliachwa bila makaazi.

Mahakama hiyo ya ICC iliyoko mjini The Hague Uholanzi ilimshtaki al Bashir kwa makosa ya uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki akituhumiwa kwamba ndiye aliyepanga kampeini ya mashambulizi katika jimbo la Darfur. Rais huyo wa zamani wa Sudan sasa yuko jela tangu jeshi lilipomuondowa madarakani kufuatia shinikizo kubwa la waandamanaji mnamo mwaka 2019.

Maafisa wengine wawili waandamizi waliokuweko katika utawala wa Bashir,waliotuhumiwa na mahakama hiyo ya ICC  kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, nao pia wanashikiliwa mjini Khartoum.

Maafisa hao ni Abdel-Rahim Muhammad Hussein, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani na ulinzi katika kipindi kirefu cha mgogoro huo pamoja na Ahmed Haroun, aliyekuwa kiongozi wa ngazi ya  juu wa masuala ya usalama na baadae akawa kiongozi wa chama tawala cha rais Bashir.

ICC yamtia hatiani Ntaganda

Fatou Bensouda amesema ofisi yake bado haijapokea uthibitisho wowote kutoka serikali ya Sudan kuhusu hatua inazokusudia kuchukua juu ya washukiwa hao wanaoshikiliwa.

Kwa mantiki hiyo ameliomba baraza na serikali ya Sudan kuongeza juhudi ya mazungumzo na ofisi yake kuhusiana na waranti za kuwakamata watuhumiwa hao. Ikumbukwe pia kwamba kiongozi wa kundi la Janjaweed Ali Kushayb ambaye jina lake halisi ni Ali Muhammad Ali  Abd-Al Rahman alijisalimisha mwenyewe kwa mamlaka huko Jamhuri ya Afrika ya kati nchi jirani na Sudan mnamo mwezi Juni na kusafirishwa moja kwa moja hadi The Hague.