1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yamkuta na hatia mbabe wa kivita wa kundi la LRA

4 Februari 2021

Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya uhalifu wa kivita ICC imememkuta na hatia mbabe wa zamani wa kivita wa kundi la LRA Dominic Ongwen kwa makosa makosa ya kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

https://p.dw.com/p/3orkU
Niederlande Dominic Ongwen
Dominic OngwenPicha: picture alliance picture alliance/dpa/M. Kooren dpa/P. Dejong

 Akisoma hukumu hiyo mjini The Hague, jaji Bertram Schmitt amesema "hatia yake imepatikana bila ya kuwa na mashaka yoyote"   

Hukumu iliyotolewa leo inafuatia kesi ya zaidi ya miaka 4 iliyoanza mwaka 2016 ikimtuhumu Ongwen kuwa na dhima katika uhalifu mkubwa na wa kutisha uliofanywa na kundi la waasi la Lord Resistance Army, LRA.

Ongwen alikabiliwa na mashtaka 70 kwa matendo ya kikatili yaliyofanywa mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kundi la waasi la LRA ambalo kiongozi wake Joseph Kony alianzisha uasi mkubwa uliolenga kuunda taifa jipya chini ya misingi ya amri kumi za Mungu kama zilivyotatwa kwenye Biblia takatifu.

LRA inatuhumiwa kwa uhalifu mkubwa 

Dominic Ongwen Gerichtsprozess 26.01.2015 Den Haag
Ongwen akifuatilia shauri lake mjini The Hague.Picha: picture-alliance/epa/P. Dejong

Kesi dhidi ya Ongwen ilijikita zaidi kwenye uhalifu uliotendwa baina ya mwaka 2002-2005 kipindi ambacho waendehsa mashtaka wanasema LRA ilifanya mauaji, ubakaji, utumwa wa ngono, ndoa za kulazimisha, utesaji, uporaji na kuwasajili watoto chini ya umri wa miaka 15 kama wapiganaji.

Kesi hiyo ni ya kwanza kwenye mahakama ya ICC ikihusisha mtuhumiwa ambaye pia ni muhanga wa uhalifu ule ule wa kivita uliofanywa  na LRA, kwa sababu Ongwen mwenyewe alitekwa nyara na waasi akiwa mtoto alipokuwa njiani kwenda shule.

Ongwen aliyepachiwa jina la utani la "siafu mweupe" pia ni mpiganaji wa kwanza wa kundi la LRA kukabiliwa na mashtaka kwenye mahakama ya ICC au kwengineko kuhusiana na madhila na umwagaji damu uliyofanywa na kundi hilo katika mataifa manne ya Afrika.

Mbabe huyo wa kivita mwenyewe alijitetea "kwa jina la mwenyezi Mungu" kuwa hana hatia na mawakili wake walisema mara kadhaa kwamba mashtaka dhidi yake sharti yaondolewe kwa sababu Ongwen aliathiriwa kisaikolojia kwa kuchukuliwa mateka na waasi alipokuwa mtoto.

Adhabu yake kutolewa miezi inayokuja 

Likiongozwa na Kony, ambaye bado anatafutwa, kundi la LRA lilisababisha mashaka na uharibifu mkubwa kwa raia wa uganda wakati likipambana na utawala wa rais Yoweri Museveni kutoka kambi zake za siri kaskazini mwa nchi hiyo na kwenye misitu ya Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Sudan Joseph Kony mutmaßlicher Kriegsverbrecher und der Anführer der Lord’s Resistance Army
Kiongozi wa LRA, Joseph KonyPicha: Stuart Price/AP Photo/dpa/picture alliance

Baada ya kukamatwa kwa nguvu na waasi wa LRA akiwa mtoto, Ongwen alilitumikia kundi hilo hadi kufikia ngazi ya kamanda, akiongoza moja ya vikosi vinne vya operesheni za LRA.

Ingawa mawakili wake wametumia hoja kwamba mateso aliyopitia Ongwen ndiyo chanzo cha uhalifu aliotenda, waendesha mashtaka waliwasihi majaji kupuuza utetezi huo wakisema mbabe huyo wa kivita alitenda makosa akiwa mtu mzima na hawezi kukwepa lawama za kile alichokifanya.

Licha ya majaji kumkuta na hatia mbabe huyo wa kivita, adhabu atakayotumikia itatangazwa miezi inayokuja na inaweza kuwa kifungo cha maisha jela.