1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yamtia hatiani Lubanga

Saumu Ramadhani Yusuf14 Machi 2012

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imemtia hatiani mbabe wa kivita wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Thomas Lubanga, ambaye pamoja na mengine anatuhumiwa kuhusika katika kuwaingiza jeshini watoto wadogo.

https://p.dw.com/p/14K3F
Thomas Lubanga
Thomas LubangaPicha: dapd

Mahakama ya ICC imetoa uamuzi uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu ndani na nje ya Kongo. Hatimaye Thomas Lubanga Dyilo, aliyekuwa kiongozi wa waasi wa chama cha UPC kilichokuwa kikiendesha kundi la PFLC linalodaiwa kuhusika katika ubakaji utesaji na mauaji ya raia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, amekutwa na hatia.

Lubanga anatuhumiwa kuwaingiza jeshini maelfu ya watoto wadogo wengine wakiwa chini ya umri wa miaka 8 wakati wa vita kwenye jimbo la Ituri. Makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema Lubanga alitenda mengi maovu zaidi ya kuwatumia watoto jeshini katika vita vyake kaskazini mwa jimbo la hilo katika mwaka 2002 hadi mwaka 2003.

Wachambuzi wa mambo wanasema uamuzi wa kumtia hatiani mtuhumiwa huyo umetoa ujumbe mzito utakaowatisha wakiukaji wengine wa haki za binadamu katika taifa hilo. Kabla ya hukumu hii kutolewa, Mwendesha Mashtaka wa ICC, Luis Moreno Ocampo, alishasema kwamba alikuwa na ushihidi wa kutosha unaoonyesha jinsi Lubanga alivyohusika katika kuwaingiza jeshini watoto.

Mahakama ya ICC pia inashughulikia kesi zinazowakabili watuhumiwa wengine wawili raia wa Kongo huku mtuhumiwa mwengine wa tatu anayetakiwa na mahakama hiyo, Bosco Ntaganda, bado akiwa huru.

Luis Moreno Ocampo
Luis Moreno OcampoPicha: AP

Lubanga anayetokea kabila la Hema alishtakiwa sambamba na wenzake wengine wawili wanaotuhumiwa kwa mashtaka mengine, Germain Katanga na Mathew Ngujdolo Chui, wote wanatuhumiwa kuliendesha kundi la waasi lililohusika kwenye mzozo wa Ituri uliosababisha mamilioni ya Wakongomani kupoteza maisha yao.

Bosco Ntaganda ambaye vile vile anatuhumiwa katika mzozo huo kama ilivyo Lubanga anasemekana kula na kunywa katika mikahawa na mahoteli ya kifahari ndani ya Jamhuri ya Kongo na kutembea bila wasiwasi huku akiwa ni jenerali katika jeshi la taifa la nchi hiyo pamoja na kuendesha biashara zake binafsi.

Itakumbukwa kwamba kama sehemu ya mchakato wa kuleta amani nchini Kongo, watu kadhaa wanaotuhumiwa kutenda uhalifu katika vita wamejumuishwa jeshini ingawa mfumo huo umewaacha wengi kupata hisia za kuwepo upendeleo wa kisheria. Kwa maana hiyo Ntaganda hayuko peke yake kati ya wale watuhumiwa walioachwa huru licha ya kudaiwa kuhusika na mauaji ya Ituri.

Nchi nane zilihusika katika vita vya Kongo zikihusika pia serikali za nchi jirani zilizokuwa zikiunga mkono makundi mbali mbali ya wapiganaji. Vita hivyo vikaonekana kuwa ni mapambano ya kuwania rasilimani ya Kongo kuanzia madini ya Cobalt, dhahabu na madini mengine na vito vya thamani.

Watetezi wa haki za binadamu wanaamini kama Ocampo angeweza kufuatilia kwa undani zaidi msururu wa kamandi ya vita hivyo, basi hapana shaka viongozi wa juu wa kisiasa katika nchi nyingi wangehusishwa na mzozo huo.

Mahakama ya ICC kwa upande mwingine inakosolewa kwa kuliandama bara la Afrika kutokana na kesi kadhaa zinazohusisha raia wa nchi za Kiafrika zinazoshughulikiwa na mahakama hiyo ya mjini The Hague nchini Uholanzi.

Majaji wa ICC
Majaji wa ICCPicha: AP

Hata hivyo, Theo Boutruche mmoja wa maafisa wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu, Amnesty International, nchini Kongo anasema kutokuwepo hofu ya watu kuadhibiwa ndio chanzo kikubwa kinachochea mzozo na kwa hivyo serikali inabidi kuweka usawa wa watu kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa wanataka kuona amani ya kudumu katika taifa hilo la Afrika ya Kati lenye wakaazi milioni 71.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef