1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yaombwa kufanya uchunguzi dhidi ya Venezuela

Isaac Gamba
27 Septemba 2018

Mataifa sita yametoa mwito kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu- ICC kuchunguza tuhuma zinazoihusisha Venezuela na uhalifu dhidi ya ubinadamu .

https://p.dw.com/p/35Z0l
Nicolas Maduro
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Franklin II

Hotuba ya Maduro katika mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa imekuja ikiwa ni saa kadhaa

baada ya Argentina, Chile, Colombia, Peru, Paraguayi na Canada kutoa  mwito kwa mahakama ya ICC kuifanyia uchunguzi Venezuela kuhusiana na tuhuma dhidi ya nchi hiyo za mauaji pamoja na ukatili mwingine dhidi ya ubinadamu.

Kuendelea kusalia na minon'gono kuhusiana na tuhuma hizi inaweza ikatafsiriwa kama ni sawa na kuidhinisha tuhuma za uhalifu dhidi ya utawala wa Venezuela, alisema waziri wa mamabo ya nje wa Paraguayi Andres Rodriguez Pedotti.

Nchi hizo sita zina matumaini kuwa hatua hiyo inaongeza mbinyo kwa Maduro ili akomeshe ghasia  na mgogoro ambao umesababisha  zaidi ya watu milioni mbili kulazimika kuikimbia nchi hiyo na kusababisha pia mfumuko wa bei nchini humo kuongezeka kwa kiwango cha juu.

Hata hivyo maafisa wa Venezuela  wamekua wakipinga ukosoaji wa kimataifa  wakisema wakosoaji wanachochewa na mabepari wanaoongozwa na Marekani  ili kuhalalisha uvamizi dhidi ya taifa hilo.

Akizungumza katika hadhara hiyo ya Umoja wa Mataifa Maduro amelalamika kuwa Marekani  inaishambulia Venezuela  kupitia vikwazo pamoja na njia nyingine huku pia ikiyashawishi mataifa mengine   kuwa na mahusiano mabovu ya kidiplomasia na Venezuela.

Maduro alisema Marekani  inataka kuendelea kutoa amri kwa ulimwengu kama vile dunia ni mali yake lakini hata hivyo Venezuela haita salimu amri.

 

Maduro yuko tayari kuzungmza na Trump

Pressekonferenz Donald Trump
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: picture alliance/Zumapress

Ama kwa upande mwingine kiongozi huyo wa Venezuela amesema yuko tayari kuzungumza na rais wa Marekani Donald Trump.Canada ni miongoni mwa nchi ambazo zimetoa mwito Venezuela ichunguzwe na mahakama  ya ICC mnamo wakati  mwendesha mashitaka mkuu  wa mahakama hiyo  , Fatou Bensouda akiwa tayari  ameanzisha uchunguzi wa awali kuhusiana na madai kuwa vikosi vya serikali ya Venezuela  tangu mwaka 2017 mara kadhaa vilitumia nguvu  ya ziada  kuwatawanya  na kuwadhibiti waandamanaji na pia kuwadhalilisha  baadhi ya wafuasi wa upinzani  waliotiwa mbaroni.

Ni juu sasa  ya mwendesha mashitaka kuamua la kufanya kuhusiana na wito uliotolewa na mataifa hayo sita licha ya mwendesha mashitaka  kutotoa ufafanuzi mara moja juu ya pendekezo hilo.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch  ni moja ya mashirika yaliyopongeza hatua iliyopendekezwa na mataifa hayo sita ambayo imejikita katika ripoti mbili  ikiwa ni pamoja na ripoti ya tume ya shirika la Umoja wa Mataifa  linalohusika na haki za binadamu  iliyofichua tuhuma  kadhaa zikiwemo za mauaji na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu.

Mwandishi : Isaac Gamba/APE

Mhariri: Bruce Amani