1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICG yataka kusogezwa mbele uchaguzi nchini Kenya

Lilian Mtono
24 Oktoba 2017

Shirika la kimataifa linaloshughulikia  mizozo, ICG limemtaka mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati kutolea ufafanuzi kauli kwamba kwamba ni vigumu kwa uchaguzi mpya wa urais utakaofanyika Oktoba 26 kuwa huru na wa haki.

https://p.dw.com/p/2mQP0
Kenia Wahlen IEBCWafula Chebukati in Nairobi
Picha: Reuters/B. Ratner

Shirika la kimataifa linaloshughulikia  mizozo - International Crisis Group, ICG limemtaka mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya, Wafula Chebukati kutolea ufafanuzi kauli aliyotoa kwenye mkutano wa waandishi wa habari Oktoba 18 kwamba ni vigumu kwa uchaguzi mpya wa urais utakaofanyika Oktoba 26 kuwa huru na wa haki, kutokana na mazingira yalivyo kwa sasa. Limemtaka mwenyekiti huyo kuiomba mahakama ya juu kuongeza siku kati ya 30 hadi 45, ili kuruhusu kupangwa kwa tarehe mpya ya uchaguzi bila ya kukiukwa kwa katiba.

Shirika hilo limeangazia maamuzi ya mahakama kuu ya Januari mwaka 2012 iliposogeza mbele uchaguzi kwa miezi sita, hatua ambayo ilisaidia kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na haki.

Shirika hilo limesema, mahakama ya juu inatakiwa kulipatia upendeleo suala hili la kuongezwa kwa siku za kuandaa uchaguzi, baada ya mwenyekiti wa tume ya IEBC, kukiri mwenyewe kwamba tume yake haiwezi kuthibitisha iwapo kutafanyika uchaguzi wa haki ndani ya muda uliopangwa.

Kutokana na kwamba ni taasisi za bunge ama mahakama ya juu zenye uwezo wa kuruhusu kuahirishwa, na kwa kuzingatia kwamba bunge litahitaji sio chini ya wiki mbili kupitisha muswada wa kuongeza siku 60 ili kufanyika uchaguzi mpya, mwito huo katika wakati kama huu unaweza tu kutolewa na mahakama.

Kenia Wahl Annullierung Uhuru Kenyatta
Mahakama itatakiwa kueleza wazi kwamba Uhuru Kenyatta atasalia mamlakani hadi uchaguzi mpya utakapofanyikaPicha: Reuters/T. Mukoya

Shirika hilo limesema iwapo mahakama itakubali kusogeza mbele uchaguzi, itatakiwa kueleza wazi kwamba Rais Uhuru Kenyatta atasalia madarakani hadi pale uchaguzi mpya utakapofanyika. Katiba haielezi kuhusu nani atashika madaraka wakati ambapo uchaguzi unafanyika baada ya siku 60, baada ya kufutwa kwa uchaguzi wa awali.

Kulingana na ICG, kufanyika upya kwa uchaguzi wa urais unaotarajiwa Oktoba 26 kumeibua kitisho kipya cha mzozo wa kisiasa nchini Kenya. Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametangaza hatashiriki, mmoja wa makamishna wa tume ya IEBC Dr. Roselyn Akombe hivi karibuni amejiuzulu na kuondoka nchini humo, huku mwenyekiti wa IEBC akiashiria kwamba hawezi kuhakikisha kutafanyika uchaguzi wa haki ndani ya muda uliopangwa.

Wasiwasi wa kutokea kwa machafuko mabaya kati ya wafuasi wa vyama viwili vikuu, ama kati ya vikosi vya usalama dhidi ya makundi yanayotaka kuzuia uchaguzi pia unazidi kuongezeka. Kuendelea kwa mchakato wa kuandaa uchaguzi huku kukiwa na wasiwasi kama huu kunaweza kuongeza mgawanyiko na kuendeleza uadui ambao tayari uligharimu maisha ya wengi na uchumi wa nchi hiyo.

Kenya ilikuwa ikiangaliwa kwa jicho ala matumaini miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki panapohusika na suala zima la Demokrasia . Lakini matukio ya  baada ya uchaguzi wa rais Agosti 8 yamesababisha maswali kadhaa  na hasa baada ya mahakama ya juu kubatilisha  matokeo ya uchaguzi hu yaliompa ushindi rais Uhuru Kenyatta. Mahakama ilisema katika uamuzi wake Septemba mosi kwamba uchaguzi huo ulikuwa na dosari kubwa na kuamuru urudiwe. Kutokana na utata uliopo tangu wakati huo, linalosub iriwa  ni ikiwa uchaguzi huo mpya utafanyika kama ilivyopangwa na tume Oktoba 26.

Mwandishi: Lilian Mtono/ https://www.crisisgroup.org/africa/horn-africa/kenya/b132-election-delay-can-help-avert-kenyas-crisis

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman