1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya vifo kutokana na UKIMWI imepungua- Umoja wa Mataifa

Kalyango Siraj30 Julai 2008

UKIMWI uliua millioni 25 miaka 27 iliopita

https://p.dw.com/p/EmY9
Wanaharakati wa UKIMWI nchini Kenya wakitaka kupatikana kwa madawa ya ugonjwa huo yenye bei nafuuPicha: AP

Wakati matayarisho kwa ajili ya mkutano wa dunia kuhusu Ukimwi utakaofanyika mwishoni mwa juma nchini Mexico yakiwa mbioni tathmini mpya ya Umoja wa mataifa kuhusu UKIMWI zinaonyesha kama kuna kitu kama utulivu fulani kuhusiana na ugonjwa huo jambo ambalo ni changamoto kwa mikakati ya kuutokomeza.

Mkutano huo wa sita wa kimataifa kuhusu Ukimwi utafanyika mjini Mexico City kuanzia jumapili hii na utawakusanya pamoja wadau takriban 22,000 wakiwemo wanasayansi,wanaharakati pamoja na watunga sera.

Mkutano huo unaofanyika kila baada ya miaka miwili na huu wa Mexico ni wa 17 na wa kwanza kufanyika Latin Amerika.

Unakwenda sambamba na tathmin mpya ya Umoja wa Mataifa kuwa Ukimwi ambao umesababisha vifo vya takriban watu millioni 25 katika kipindi cha miaka 27 na kuwaacha wengine millioni 33 wakiwa wameambukizwa na virusi vya HIV,sasa unaonyesha alama za kutulia.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ukimwi la UNAIDS linasema kuwa takwim mpya za maambukizi zinaonyesha kidogo kupanda ingawa mataifa mengine baado katika hali inayoweza kusemwa kuwa yanabanwa na ugonjwa huo. Hata hivyo, mambukizi kwa ujumla, ukichukuliwa kwa kiwango cha asilimia dhidi ya idadi ya watu duniani,imebaki palepale bila kupanda wala kushuka.

Vifo kutokana na ukimwi katika mwaka wa 2007 vilipungua kwa kiasi cha millioni mbili,hii ikiwa upungufu wa asili mia 10 kwa kipindi cha miaka miwili.Wataalamu wanasema hali hiyo imetokana na kuwa takriban watu millioni tatu ambao ni maskani tena waliathirika vibaya waliweza kupata dawa ambayo imeweza kubadili hali ya kinga yao.

Licha ya mafanikio hayo lakini baado hali si nzuri sehemu zote.Wataalamu wengi wanasema kuwa viwango vya uambukizaji vinapanda katika mataifa mengi.

Wakati hayo yakiendelea taarifa za ukimwi kutoka Kenya zasema kuwa asili mia nane ya wakenya walio na virusi vya Ukimwi hawajui kuwa wako navyo.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliotolewa jumanne mjini Nairobi unaonyesha kuwa kila wakenya wanne kati ya watano waishio na virusi vya ukimwi hawajui hali yao huku theluthi mbili ya watu millioni 37 walioko Kenya hawajapima kuona ikiwa wanavirusi au la.

Uchunguzi wa ishara za Ukimwi nchini Kenya unasema kuwa asili mia 57 ya watu waliyona HIV walisema kuwa hawajapima ukimwi huku asili mia 26 walisema kuwa hawana virusi vya Ukimwi lakini baade walipopimwa walipatikana kuwa navyo.

Mkuu wa mpango wa taifa wa kudhibiti Ukimwi nchini humo, Ibrahim Mohamed, amenukuliwa na vyombo vya habari kusema kuwa asili mia 16 ya watu walioulizwa hawakutaka kujua matokeo ya uchunguzi wao wakiogopa.

Uchunguzi huo umeonyesha kuwa takriban watu wa makamo wakenya millioni 1 karibu Unusu wanaishi na Ukimwi.

Uchunguzi huu ambao ulifanyika kati ya miezi ya Agosti na Disemba mwaka wa 2007 ndio wa kwanza kufanyika tangu mwaka wa 2003.

Watoto hawakuchunguzwa katika zoezi hilo.