1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliofariki kuongezeka Ecuador

18 Aprili 2016

Timu ya waokozi kutoka nchi mbali mbali jirani ya Ecuador zinaendelea kutafuta waliofunikwa na vifusi kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililoitikisa Ecuador na kusababisha maafa makubwa na uharibifu

https://p.dw.com/p/1IXbm
Uharibifu uliosababishwa na tetemeko la ardhi katika mji wa Manta
Uharibifu uliosababishwa na tetemeko la ardhi katika mji wa MantaPicha: Getty Images/AFP/L. Acosta

Watu 272 wameuwawa kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililoitikisa Ecuador jumamosi usiku.Waokoaji bado wanaendelea kukabiliana na hali ngumu ya kuwaokoa walionusurika kutoka kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka. Rais Rafael Correa amesema idadi ya waliouwawa huenda ikaongezeka.

Tetemeko la ardhi lenye kipimo cha 7.8 richta limeitikisa nchi hiyo ndogo yenye utajiri wa mafuta ya Amerika kusini Jumamosi usiku na kuharibu mahoteli pamoja na makaazi ya watu katika mwambao wa pwani ya pacific eneo lenye umaarufu kwa watalii na kusababisha vile vile mitaa kadhaa kubakia vifusi baada ya majengo kuporomoka.Zaidi ya watu 2000 walijeruhiwa wakati wa tetemeko hilo lililoyatikisa majumba halikadhalika mitetemeko midogo kadhaa iliyofuatia.Rais Rafael Correa alietembelea maeneo yaliyoharibiwa vibaya na mkasa na kusema

Rais Raffael Correa
Rais Raffael CorreaPicha: picture-alliance/dpa/S. Lecocq

''Idadi rasmi ya waliopoteza maisha nchi nzima ni 272.Nimetembelea maeneo mbali mbali na nakhofia kwamba idadi hiyo itaongezeka kwasababu tunaendelea kuondoa vifusi na tunatumai kuwapata manusura.Saa kadhaa za mwanzo ni muhimu sana.Zaidi ya saa 24 zimemalizika tangu lilipopiga tetemeko la ardhi hata hivyo kuna ishara ya watu kuwepo hai katika vifusi vingi na hilo ndilo suala muhimu zaidi.Na baadae tutajaribu kuzitafuta maiti nyingi kadri itakavyowezekana.''

Maafisa wanasema katika mji mkuu Quito uharibifu pia ulitokea huku majengo kadhaa yakipata nyufa na nguvu za umeme kukatika ingawa mitambo muhimu ya mafuta ilionekana kunusurika. Hata hivyo katika mwambao wa pwani uharibifu mkubwa ulizifanya nchi jirani za Colombia pamoja na Mexico ambayo inauzoefu na mitetemeko ya ardhi pamoja na El Salvador zilituma haraka timu ya waokozi kusaidia hali ya mambo nchini Ecouador.Sambamba na hayo katika mji wa Portoviejo ulioko kilomita 15 kutoka pwani ya Ecoduour tetemeko hilo la ardhi liliporomosha kuta za gereza moja na kusababisha wafungwa 100 kutoroka ingawa baadhi yao walikamatwa tena na kurudishwa baadae katika gereza hilo lakini polisi ilikuwa mbioni kuwasaka wengine kwa mujibu wa ujumbe wa Twitter wa waziri wa sheria Ledy Zuninga.

Watu wakitembea Karibu na majumba yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi,Manta
Watu wakitembea Karibu na majumba yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi,MantaPicha: Reuters/P. Ochoa

Kwengineko katika mji huo wa Portviejo ulioharibiwa vibaya zaidi na tetemeko hilo inaarifiwa kwamba harufu ya miili iliyoanza kuharibika imeanza kuhanikiza kwenye anga ya eneo hilo huku waokoaji wakijitahidi kwa nguvu zote kutafuta walionusurika.Mfanyakazi mmoja wa shughuli za uokozi aliyekuwa akichimba kifusi kwa ajili ya kutafuta manusura amesema kwamba tayari wameziondoa maiti tatu kutoka kwenye kifusi hicho ingawa wanaamini kuna watu wengine kati 10 na 11 waliosalia ndani ya kifusi hicho cha hoteli ya ghorofa sita ikijulikana kama El-Gato iliyoporomoka.Rais Correa alitembelea eneo lililofikwa na mkasa siku ya Jumapili baada ya kukatiza ziara ya kiserikali ya kwenda Vatican.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

MhaririJosephat Charo