1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliouawa kufuatia shambulio Kenya yaongezeka

17 Januari 2019

Idadi ya waliofariki dunia kufuatia shambulio la kigaidi lililotekelezwa mjini Nairobi, nchini Kenya imefikia watu 21. Familia kadhaa za waliofariki dunia zimeanza kuzika mili ya wapendwa wao leo.

https://p.dw.com/p/3BhMS
Nairobi Angriff auf Hotel in Kenias Hauptstadt
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Maafisa wa usalama nchini Kenya wameanza tena kufanya upekuzi katika hoteli ya DusitD2 leo, iliyoshambuliwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al Shabaab, wakiwa na mbwa wa kunusa na wataalamu wa mabomu, huku kukiwa na taarifa kuhusu mmoja wa washambuliaji. Afisa mmoja wa polisi, ambaye hakutaka kutajwa jina, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wana uhakika hakuna watu waliokwama kwenye hoteli hiyo au majengo yaliyoizunguka baada ya operesheni ya saa ishirini ambapo raia 700 waliokolewa.

Watu wawili wanaodaiwa kuhusika katika utekelezwaji wa shambulio hilo wamekamatwa. Kulingana na Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi nchini Kenya Joseph Boinett, miili mingine sita ilipatikana katika eneo la tukio, na afisa mmoja wa polisi alifariki dunia kutokna na majeraha aliyoyapata alipokuwa akitibiwa hospitalini, ´´Kufuatia uchunguzi wa Mkuu wa Idara ya Upelelezi, tumewakamata watu wawili ambao tuna sababu nzito za kuamini kwamba walihusika katika shambulio hilo na wanazuiliwa ili kuwasaidia polisi katika uchunguzi wao.´´

Kenia Nairobi Explosion und Schüsse in Hotel und Bürogebäude
Picha: Getty Images/AFP/L. Tato

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limesema watu kumi na tisa ambao wanaaminika walikuwa katika jengo lililoshambuliwa hawajulikani waliko.

Akilihutubia taifa kuhusiana na tukio hilo, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema jana Jumatano kwamba Kenya itaendelea kuwasaka wote waliohusika katika shambulio hilo, na kuwahakikishia Wakenya kwamba wataendeleza mikakati kuhakikisha taifa hilo pamoja na wananchi wako salama,´´Tutamtafuta kila mmoja aliyehusika katika kufadhili, kupanga na kutekeleza kitendo hicho kiovu. Tutawatafuta bila kuchoka, popote watakapokuwa, hadi watakapowajibishwa. Namhakikishia kila Mkenya pamoja na wageni kwamba muko salama hapa Kenya.´´

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
Picha: Reuters/T. Mukoya

Maafisa wa polisi wanasema miongoni mwa raia waliouawa, kumi na sita ni Wakenya, mmoja wa Uingereza, mmoja wa Marekani na watatu wenye asili ya Africa lakini uraia wao haujabainika. Kundi la Al Shabaab lilidai kuhusika na kusema walifanya hivyo kama ulipizaji kisasi kufuatia uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

Ikumbukwe shambulio sawa na hilo lilitekelezwa mwaka 2013 katika Duka kuu la Westgate ambapo watu 67 waliuawa, na shambulio jingine katika Chuo Kikuu cha Moi mjini Garissa mwaka 2015 ambapo watu 147 waliuawa, wengi wakiwa wanafunzi.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE/RTRE

Mhariri: Iddi Sessanga