1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 32,658 waliuawa na magaidi mwaka 2014

17 Novemba 2015

Taasisi ya maswala ya Uchumi na Amani imesema idadi ya watu waliouawa ulimwenguni kwenye mashambulizi ya kigaidi ni zaidi ya asilimia 80 mwaka uliopita, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuwahi kunakiliwa .

https://p.dw.com/p/1H7NF
Abdelhamid Abaaoud IS Islamischer Staat Flagge Koran
Picha: picture-alliance/dpa/Dabiq

Ripoti hiyo inayohusu ugaidi ulimwenguni inaarifu kuwa watu elfu 32,658 waliuawa na magaidi mwaka 2014,idadi ambayo ni ya juu zaidi kuliko mwaka uliotangulia ambapo watu 18,111 waliuawa.

Utafiti huo unatazama ugaidi kama matumizi mabaya ya nguvu na shirika lolote lisilo la serikali kwa kuafikia lengo la kisiasa, kiuchumi, kidini au kijamii kwa kusababisha hofu, kushurutisha au kitisha.

Kundi la Boko Haram nchini Nigeria na Dola la kiislamu la IS yalihusika katika vifo vya zaidi ya nusu ya idadi hiyo ya watu kulingana na ripoti hiyo ambayo inatathmini mashambulizi, vifo na madhara yanayotokana na uvamizi wa kigaidi katika mataifa 162.

Ugaidi Umeongezeka

Mwenyekiti mtendaji wa taasisi hiyo ya Uchumi na amani iliyoiandaa ripoti hiyo Steve Killelea amesema ugaidi unaongezeka kwa kasi.

Utafiti huo umebaini kuwa ugaidi umejikita sana huku mauaji hayo ya kigaidi katika mataifa ya Afghanistan, Iraq, Nigeria, Pakistan na Syria yakifikia asilimia 78 mwaka jana.

Iraq ndio iliathirika zaidi ambapo vifo 9,929 vilitokana na ugaidi, pia nchi hiyo ilikumbwa na mashambulizi mengi na vifo vingi vinavyotokana na ugaidi kuliko taifa lolote lile.

Taifa lingine lililoshuhudia kuongezeka kwa ugaidi ni Nigeria, ambayo ilishuhudia zaidi ya asilimia 300 kwa kusababisha mauwaji ya watu 7,512.

Frankreich Attentat Stade de France
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Ena

Utafiti huo unasema kuwa mataifa ya magharibi hayako hatarini kukumbwa na mashambulizi ambayo yanaweza kusababishwa na ukereketwa wa kisiasa, utaifa au ubaguzi wa rangi na ushindani wa kidini badala ya imani kali ya kiislamu.

Uingereza ndio imekumbwa na visa vingi vya kigaidi miongoni mwa mataifa ya magharibi, hususan kutokana na wanamgambo wa Ireland ya Kaskazini.

Hata hivyo mashambulizi ya wiki iliyopita mjini Paris yaliyowauwa watu 129 ambayo Dola la kiislamu imekiri kuyatekeleza yanaonesha jinsi ugaidi ulivyokithiri.

Mwenyekiti huyo amesema mashambulizi ya Paris yamefikia kilele barani Ulaya. Amesema mashambulizi hayo yanabainisha jinsi Dola la kiislamu linavyoweza kufanya mauaji Ulaya kwa kutumia mbinu za hali ya juu.

Wapiganaji wa kigeni kutoka Syria ni Kitisho

Ameonya kuwa wapiganaji wa kigeni ambao wamesafiri hadi Iraq na Syria wanaokadiriwa kufikia kati ya 25000 na 30000 tangu 2011 huenda wakawa hatari. Amesema wapiganaji hao wanaorudi kutoka Syria wamepata mafunzo ya kijeshi. Ameongeza kuwa mbinu inazotumia kundi la ISIS zinabadilika kwa kuwalenga raia. Ni vigumu kuona kitisho cha kundi hilo kikitoweka katika miaka miwili ijayo. Utafiti huo aidha umekadiria kuwa gharama ya ugaidi inafikia dola bilioni 52.9 hiki kikiwa ni kiwango cha juu zaidi tangu mwaka 2000.

Utafiti huu umefanywa huku polisi nchini Uingereza wakitangaza leo kuwa wamewakamata watu wawili kwa makosa ya ugaidi waliojaribu kuondoka nchini humo. Ingawa wanasema kukamatwa kwao hakuhusiani na mashambulizi ya Paris.

Mwandishi:Bernard Maranga/AFP

Mhariri:Josephat Charo