1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliouawa Mogadishu yafikia 300

Sylvia Mwehozi
16 Oktoba 2017

Idadi ya vifo vya watu waliofariki katika shambulizi la Jumamosi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu imefikia 300 huku wengine zaidi ya 300 wakijeruhiwa. Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo.

https://p.dw.com/p/2ltLv
Somalia Mehr als 260 Tote nach Doppel-Anschlag in Mogadischu
Picha: Reuters/F. Omar

Mkurugenzi wa huduma ya magari ya kusafirisha wagonjwa Dr. Abdulkadir Adam amesema kwamba watu zaid wamefariki kutokana na majereha katika saa chache zilizopita.

Shughuli ya mazishi imeanza huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka. Shambulizi hilo la mabomu ya kutegwa kwenye lori lililenga eneo lenye shughuli nyingi za kibiashara mjini Mogadishu pia limewajeruhi watu wengine 300. Serikali ya Somalia imelituhumu kundi la wanamgambo la al-Shabab lenye mafungamano na kundi la al-Qaeda ambalo hadi sasa halijatoa taarifa ya kuhusika kwake.

Maafisa wanasema watu zaidi ya 70 ambao wamejeruhiwa vibaya wamekimbizwa nchini Uturuki kwa ndege kwa ajili ya mataibabu wakati misaada ya kimataifa ikianza kuwasili. Hospitali zilizojaa mjini Mogadishu zinaendelea kuwahudumia majeruhi, ingawa afisa wa polisi Ibrahim Mohamed ameliambia shirika la habari la AFP kwamba majeruhi wengi wameuangua vibaya kiasi cha kutotambulika.

Somalia Mogadischu Bombenanschlag
Mwanaume mmoja akipita kando ya magari yaliyoharibiwa katika shambuliziPicha: Getty Images/AFP/M. Abdiwahab

Shambulizi hilo linatajwa kuwa baya zaidi kuwahi kushuhudiwa duniani na katika ukanda wa Afrika, kusini mwa jangwa la sahara katika miaka ya hivi karibuni, kubwa zaidi ya shambulizi katika chuo kikuu cha Garissa nchini Kenya 2015, pia zaidi ya mashambulizi ya 1998 katika balozi za Marekani nchini Tanzania na kenya.

Waziri wa habari  wa Somalia Abdirahman Osman amesema nchi nyingine ikiwemo Kenya na Ethiopia zimethibitisha kutuma usaidizi wa kimatibabu katika kile serikali ya Somalia ilichokiita ni "janga la kitaifa".

Mashambulizi ya al-Shabaab

Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo lakini kundi la wanamgambo wa kiislamu la al-Shabab mara nyingi limekuwa likiyalenga maeneo muhimu mjini Mogadishu katika jitihada zake za kuiangusha serikali ya Somalia ambayo inaungwa mkono kimataifa.

Mapema mwaka huu, liliapa kuongeza kasi ya mashambulizi baada ya utawala wa rais Donald Trump wa Marekani na rais mpya wa Somalia, kutangaza mikakati mipya ya kijeshi kukabiliana na kundi hilo.

Mwezi Februari mwaka huu bomu la kujitoa muhanga la kwenye gari liliwaua watu 36, muda mchache baada ya wapiganaji wa al-Shabaab kutishia "vita mbaya" dhidi ya rais mpya aliyechaguliwa anayejulikana pia kwa jina la Farmajo.

Maombolezo ya kitaifa

Somalia Mogadischu Bombenanschlag
Wanajeshi wa Somalia pamoja na raia wakiwasili eneo la tukio kuwaokoa majeruhiPicha: Getty Images/AFP/M. Abdiwahab

Rais wa nchi hiyo Mohamed Abdullahi Mohamed ametangaza siku tatu za maombolezo na kuungana na maelfu ya watu ambao waliitikia wito wa kuchangia damu katika hospitali. Pia ametembelea eneo lilikofanyika shambulizi na pia kukutana na wahanga wa tukio hilo. Farmajo amesema kupitia televisheni kuwa "tukio la leo ni shambulizi baya ambalo limetekelezwa na Al-Shabaab dhidi ya raia wasio na hatia na halikuilenga serikali ya Somalia mojakwamoja".

Meya wa mji wa Mogadisgu Tabid Abdi Mohamed pia amewatembelea waathirika na kusema kwamba hofu ya shambulizi hilo "halizungumziki". Mamia ya watu walipita katika mitaa ya Mogadishu jana Jumapili kulaani shambulizi hilo.

Jumuiya za kimataifa zalaani shambulizi

Marekani, Uingereza, Canada, Ufaransa, Uturuki na Umoja wa Afrika zimelaani shambulizi hilo. Msemaji wa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, Ibrahim Kalin amesema Uturukiimetuma ndege zilizo na vifaa vya matibabu, na kuongeza kwamba majeruhi watapelekwa Uturuki kwa ajili ya matibabau zaidi. Uturuki ni mfadhili na mwekezaji mkuu nchini Somalia.

Waziri wa mambo ya nje wa Qatari Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al-Thani ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba ubalozi wa nchi hiyo umeharibiwa vibaya katika shambulizi hilo na mmoja wa maafisa wake wa juu amejeruhiwa.

Mwanidshi: Sylvia Mwehozi/AP/AFP

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman