1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF: Yaonya ongezeko la deni la Afrika licha ya uchumi kukua

Grace Kabogo
9 Mei 2018

Shirika la Fedha Duniani limesema uchumi wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara umekuwa kwa asilimia 3.4 kwa 2018 kutoka asilimia 2.8 mwaka uliopita, ingawa madeni katika nchi hizo maskini duniani bado ni tatizo kubwa.

https://p.dw.com/p/2xRqr
Logo IMF Internationaler Währungsfond

Shirika la Fedha Duniani limesema kuwa uchumi wa mataifa ya kusini mwa Jangwa la Sahara umekuwa kwa asilimia 3.4 kwa mwaka huu kutoka asilimia 2.8 mwaka uliopita, ingawa madeni katika nchi hizo maskini duniani bado ni tatizo kubwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Fedha Duniani, IMF nchi zilizoongoza kukua kiuchumi ni pamoja na Benin, Burkina Faso, Ethiopia, Ghana, Cote d'Ivoire, Rwanda, Senegal na Tanzania. Uchumi wa nchi hizo ulikua kwa asilimia sita au zaidi kwa mwaka 2017 na zitaendelea kushikilia kiwango hicho kwa muda mrefu. Mkurugenzi wa IMF barani Afrika, Abebe Aemro Selassie amesema Ethiopia imeongoza kwa kupata asilimia 10.9 ya pato la ndani la taifa kwa mwaka 2017 na inategemea kufurahia asilimia 8.5 kwa mwaka huu.

Ripoti hiyo imetolewa wakati ambapo nchi za Afrika bado zinaendelea kushika nafasi ya juu kwa kuwa na deni kubwa. Aemro Selassie amesema wito wanaoutoa kwa sasa ni nchi hizo kuyafanyia marekebisho mapato ya serikali. Amesema nchi zinazouza mafuta kwa wingi na nyingine zinazotegemea uchumi kutokana na rasilimali zinataka uchumi wao ukue kwa kasi ili kupunguza mizigo yao ya madeni.

Akizungumza na DW, mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Tanzania, Profesa Honest Prosper Ngowi anafafanua kuwa serikali za Afrika zimekuwa zikikopa sana kwa sababu ya kuwekeza katika miundombinu kama vile barabara, reli na viwanja vya ndege. Amesema ukopaji unachangiwa na makusanyo ya ndani ya kodi kutokidhi mahitaji.

Elfenbeinküste - Hafen von Abidjan
Makontena katika bandari ya Abidjan, Cote d'Ivoire,Picha: picture-alliance/N. Zorkot

IMF imesema kiasi ya nchi 40 zenye kipato cha chini kwa sasa zina mzigo mkubwa wa madeni. Mwaka uliopita, serikali za Afrika ziliuza Dola bilioni 7.5 katika dhamana za serikali, ikiwa ni mara 10 zaidi ya mwaka 2016 na tayari zimetangaza mpango wa kuuza zaidi ya Dola bilioni 11 katika deni la nusu ya kwanza ya mwaka huu 2018.

Takwimu za IMF zinaonesha kuwa deni la fedha za kigeni limeongezeka kwa asilimia 40 kutoka mwaka 2010 na 2013 hadi 2017 na sasa limeongezeka kwa karibu asilimia 60 ya deni jumla la umma la  bara hilo. Wakati huo huo, malipo ya wastani ya riba yameongezeka kutoka asilimia 4 ya matumizi kwa mwaka 2013 hadi asilimia 12 mwaka 2017.

Nchi sita za Chad, Eritrea, Msumbiji, Jamhuri ya Kongo, Sudan Kusini na Zimbabwe ziliwekwa katika kundi la nchi zenye deni kubwa mwishoni mwa mwaka uliopita. Na viwango vya IMF kwa ajili ya Zambia na Ethiopia vilibadilika kutoka wastani hadi kuwa katika ''hatari kubwa ya mzigo wa madeni.''

IMF imekiri kuwa mahitaji ya Afrika kwa kiasi kikubwa yataendelea kutegemea uwekezaji mkubwa wa kujenga miundombinu na maendeleo ya jamii. Lakini kwa kufanya hivyo, wakati inaepuka hatari ya kunasa kwenye madeni, bara hilo ambalo kwa sasa linapata mapato ya chini kabisa ya pato la ndani la taifa duniani, litahitaji kujitegemea zaidi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf