1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF yasema uchumi wa dunia umeshuka

Isaac Gamba
9 Oktoba 2018

Shirika la fedha la kimataifa IMF limesema vita vya kibiashara vilivyosababishwa na hatua ya Marekani kutangaza viwango vya ushuru pamoja na madeni makubwa vimeshusha uchumi wa dunia.

https://p.dw.com/p/36DQ4
Indonesien IWF stellt Weltwirtschaftsbericht auf Bali vor
Picha: picture-alliance/dpa/F. Lisnawat

Ikitangaza utafiti wake wa hivi karibuni hii leo  kuhusiana na hali ya uchumi duniani  katika kuelekea mkutano wa kilele utakaofanyika Bali Indonesia,  IMF imesema kukua kwa uchumi duniani kwa mwaka huu kutasalia katika kiwango cha asilimia 3.7 na kusalia katika kiwango hicho hapo mwakani.  Utafiti huo unaonesha kuwa kiwango hicho ni cha chini kulinganisha  na asilimia 3.9 iliyotangazwa April.

 Uchumi unaonekana kuporomoka  na kuwa katika kiwango cha asilimia 3.7 alisema mchumi mkuu wa IMF  Maury Obstfeld wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kutangazwa kwa ripoti hiyo.

Aidha IMF pia inasema kiwango cha kukua kwa uchumi wa mataifa ya China na Marekani  yaliyo na uchumi mkubwa duniani nacho pia kimeshuka.

Uchumi wa China sasa unakadiriwa kukua kwa kiwango cha asilimia 6.2 kwa mwaka 2019 kiwango ambacho ni cha chini  kulinganisha na asilimia 6.4 iliyokadiriwa Julai huku IMF ikionya    uchumi wa China uko hatarini kuporomoka kwa asilimia moja kamili mwakani kama vita hivi vya kibiashara vitaendelea hali inayoleta hofu na kupunguza imani kwa wafanyabiashara na hivyo kuathiri masoko.

Kwa mujibu wa IMF utafiti huo hauhusishi athari ya viwango vingine vya ushuru dhidi ya China vinavyotarajiwa kutangazwa na Marekani   pamoja na hatua zitakazo chukuliwa na China kibiashara dhidi ya Marekani .

 

BREXIT moja pia ya sababu

Christine Lagarde in Marokko
Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Christine LagardePicha: Getty Images/AFP

Shirika hilo limesema kushindwa kuidhinishwa kisheria mikataba ya kibiashara  kati ya Marekani , Mexico na Canada pamoja na mchakato wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya  kuwa moja ya sababu ambazo zinachangia hali hiyo.

Viwango vya kodi vilivyotangazwa na Marekani dhidi ya China  vinavyohusiana zaidi na  magari pamoja na vipuri vya magari vinaweza  kuvuruga biashara na hasa iwapo kuatakua na uamuzi wa kujibu hatua hiyo ya Marekani.

Mivutano ya kibiashara kidunia nayo pia inatajwa kuathiri kukua kwa uchumi kanda ya ulaya  katika kipindi cha mwaka 2018/2019.

Aidha IMF imesema kushuka kwa viwango vya uzalishaji kuna weza kukaiathiri Ujerumani kwa kiwango kikubwa mnamo wakati kiwango cha kukua kwa uchumi wa Ujerumani  kwa mwaka 2018 na 2019 kikikadiriwa kuwa asilimia 1.9 ambacho ni kiwango cha chini na hiyo ikitajwa kusababishwa na kushuka kwa mauzo ya nje pamoja na uzalishaji viwandani.

Mwandishi :Isaac Gamba/DPAE/RTRE/DW

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman