1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India miaka 60 ya uhuru

15 Agosti 2007

India ilijipatia uhuru siku kama leo,1947 chini ya Jawhalal Nehru. Miaka 60 baadae, India inastawi kiuchumi lakini ufukara umeselelea.

https://p.dw.com/p/CH9a
India miaka 60 ya uhuru
India miaka 60 ya uhuruPicha: picture-alliance/dpa

India inaadhimisha leo miaka 60 ya uhuru,lakini waziri wake mkuu Manmohan Singh, ameonya wahindi wasijiamini kupita kiasi kuwa kila kitu kiko sawa kutokana na kustawi hivi sasa kwa uchumi wake.Alionya kwamba mitihani migumu inaikabili India.

India,dola kubwa kabisa la kidemokrasia duniani,linakumbuka na kuadhimisha siku ya leo, 1947 pale kiongozi wake Jawahalal Nehru alipotangaza uhuru na kukomesha enzi ya miaka 200 ya utawala wa Uingereza huko Barahindi.

Kabla ya tangazo hilo,masaa 24 kabla,marehemu mahtima Gandhi aliepinga kugawanywa Barahindi chini ya misingi ya kidini,alimuona Mohammed Ali Jinah na chama chake cha Muslim League-kitangaza kuundwa kwa dola la Pakistan katika sehemu ya Barahindi.

Katika hotuba yake hii leo ,waziri mkuu Manmohan singh alipongeza demokrasia ya India kuwa ndio matunda bora kabisa ya uhuru.Alisema na ninamnukulu,

“Mafanikio ya demokrasia ya dola lisiloegemea dini katika taifa la wakaazi bilioni 1 wenye mila na utamaduni tofauti,yanawavutia wengi.”

Lakini, “Mazuri kabisa bado hayajaja bali yako njiani” aliongeza Manmohan Singh.Hapo akichukuliwa na mkondo wa matumaini mazuri kuwa India iko njiani kuibuka dola kuu duniani.”Tuna mwendo mrefu wa kwenda bado” alisema waziri mkuu huyo wa India.

Kuna upande mwengine wa sarafu:Licha ya kustawi mno kwa uchumi wa India unaokua hadi 9%,waziri mkuu alitaja ufukara ulienea India aliouita “aibu kwa taifa” pamoja na madhila mengine yanayoikumba India kama utapiamloo,ukosefu wa kazi ,machafuko katika jamii na mfarakano wa kidini na madhehebu.

“matunda ya maendeleo ya uchumi wetu lazima yaonekane kwenye hali za maisha na katika jasho la umma wetu wanaoishi chini ya kiwango cha chni cha umasikini.”

Alisema rais mpya wa India alietawazwa kitini hivi majuzi.

Waziri mkuu Singh alipendekeza mapinduzi pia katika sekta ya kilimo na akaahidi kuanzisha mfuko wa kukidhi malipo ya uzeeni-pension- kwa wastaafu pamoja na kuendeleza mbele matibabu.Kiasi cha shule 6.000 mpya zitaanzishwa .

Baadhi ya maoni yake yaliungwamkono na wahindi waishio mijini katika uchunguzi wa maoni uliofanywa na gazeti mashuhuri la HINDUSTAN TIMES:

52% ya wakaazi 1,247 waliochangia maoni yao wakiwa kati ya umri wa miaka 16-25 walisema wanajivunia demokrasia iliopo India.

Shamra-shamra za kuadhimisha siku hii ya kuzaliwa India, ziligubikwa hatahivyo, na ulinzi mkali huku ndege za kivita ,vikosi vyenye silaha vikishika zamu majiani baada ya vitisho vya wapiganaji wa Al Qaeda na waasi wanaogombea kujitenga na India.

Katika mji mkuu New Delhi,kikosi cha askari-polisi na wanajeshi 70.000 kikipiga doria.

Uasi tangu katika jimbo la Kashmir hadi Assam,waziri mkuu Singh ameahidi hatua kali kupambana na chuki na siasa kali.