1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yapiga marufuku mikusanyiko mjini New Delhi

Admin.WagnerD18 Desemba 2019

Polisi ya India imetangaza marufuku ya mikusanyiko mikubwa kwenye ya maeneo ya mji mkuu New Delhi wakati ikiongeza juhudi za kudhibiti maandamano dhidi ya sheria ya uraia inayooneka kuwa ya kibaguzi dhidi ya waislamu. 

https://p.dw.com/p/3V1ie
Indien Assam | Protest gegen Staatsbürgerschaftsgesetz
Picha: Getty Images/AFP/B. Boro

Uamuzi huo wa kutangaza marufuku ya mikusanyiko katika baadhi ya wilaya zenye idadi kubwa ya waislam mjini New Delhi, ambako baadhi ya mafisa wa polisi walijeruhiwa wakati makabiliano na waandamanaji, unafuatia kukamatwa kwa mamia ya watu kwenye maeneo chungu nzima ya India.

Licha ya hatua hizo bado maandamano mapya yaliripotiwa leo kwenye majimbo ya Bengal Magharibi, Tamil Nadu, Telangana na Maharashtra huku mengine yakipangwa kufanyika huko Kerala, Pradesh na Gujarat.

Maandamano dhidi ya sheria mpya ya uraia ambayo itaharakisha mchakato wa wahamiaji wasio waislamu kutoka mataifa matatu jirani na India kupatiwa uraia wa nchi hiyo tayari yamesababisha vifo vya watu sita katika jimbo la kaskazini mashariki la Assam.

Siku moja tangu kutkea machafuko makubwa mjini New Delhi, polisi imesema mikusanyiko yote inayopindukia watu wanne imezuiwa.

Polisi ilifyetua gesi ya kutoa machozi baada ya maelfu ya waandamanaji kurusha mawe na kuyachoma moto mabasi mawili na kituo kimoja cha polisi katika wilaya ya Seelampur.

Pingamizi dhidi ya sheria hiyo kusikilizwa Januari, 2020

Indien Proteste gegen Staatsbürgerschaftsgesetz
Picha: Reuters/A. Abidi

Kiasi watu 21 ikiwemo polisi 12 walijeruhiwa wakati wa makabiliano hayo huku wengine sita wamekamatwa kwa makosa ya kuchoma moto mali  pamoja na kufanya vurugu.

Maandamano mapya yamefanyika baada ya mahakama ya juu ya India kutangaza leo, pingamizi zote zilizowekwa dhidi ya sheria mpya ya uraia yatasikilishwa mwezi Januari mwaka unaokuja.

Waliofungua pingamii hizo wanasema sheria hiyo mpya ni kinyume cha katiba na inapingana na tamaduni zinazotambua India kuwa taifa lisilo la kidini.

Modi hana mipango ya kusalimu amri

Indien Parlament PK Narendra Modi
Picha: Reuters/A. Hussain

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ameendelea kushupalia msimamo wake licha ya maandmaano ya umma na amesema sheria hiyo haitowadhuru raia wa India huku ikiwalinda waumini kihindu, Sikh na jamii nyingine za wachache zinazokabiliwa na unyanyasaji katika mataifa jirani yenye waumini wengi wa dini ya kiislamu.

Wakosoaji wake wanasema sehria hiyo ni sehemu ya mipango ya waziri mkuu Modi na serikali yake inayoongozwa na wahindu ya kuwatenga waislamu milioni 200 wa India.

Vyama vya upinzani vikiongozwa na rais wa Bunge Sonia Gandhi, walikutana jana na rais Ram Nath Kovind kumrai aishauri serikali ya waziri mkuu Modi kuondoa sheria hiyo.

Mamlaka za India zimechukua ya kuzima mtandao wa intaneti na kutumia vikosi vya usalama kuzuia maandmaano lakini waandmaanji wameapa kuendelea kupambana hadi sheria hiyo itakapofutwa.