1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ingali mapema kuiamini Korea Kaskazini - Moon Jae-in

Mohammed Khelef
7 Machi 2018

Licha ya matumaini kwamba sasa mahusiano kati ya Korea mbili yanaimarika kufuatia kauli ya Korea Kaskazini kuwa tayari kuachana na nyuklia, Korea Kusini inasema bado ingali mapema mno kujenga imani.

https://p.dw.com/p/2tp9D
Nordkorea Kim Jong Un spricht mit südkoreanischer Delegation
Picha: Reuters/Yonhap

Huku kukiwa na matumaini ya kuimarika kwa mahusiano kati ya nchi yake na Korea Kaskazini, Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini ametoa tahadhari kwamba bado ingali mapema mno kujenga imani na ishara ya Korea Kaskazini kujiondoa kwenye mpango wake wa nyuklia, licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kuipokea kwa mikono miwili ahadi hiyo.

Mapema Rais Trump alilipokea tangazo linalochukuliwa kuwa la kufungua njia kutoka utawala wa Korea Kaskazini, kwamba unataka kuzungumza na Marekani na usingelikuwa na haja ya kuwa na silaha za kinyuklia endapo ingelihakikishiwa usalama wake.

Trump alisema tamko hilo ni jema na linaonekana kutoka moyoni.

Hata hivyo, Rais Moon aliwaambia viongozi wa chama chake kwamba bado wako kwenye hatua za awali za mazungumzo na hivyo ingali mapema mno kujenga matumaini. 

"Mazungumzo baina ya Korea mbili tu hayatoshi pekee kufikia amani," alisema akisisitiza umuhimu wa nchi yake kuendelea na mahusiano ya karibu na mshirika wake mkuu wa usalama, Marekani, na kuongeza kwamba hakutakuwa na nafuu ya vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini kwa sababu ya mazungumzo baina ya Korea hizo mbili.

Japan yaonesha wasiwasi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Yoshihide Suga, asema nchi yake bado inaendelea kuishinikiza Korea Kaskazini´.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Yoshihide Suga, asema nchi yake bado inaendelea kuishinikiza Korea Kaskazini´.Picha: Yoshikazu Tsuno/AFP/Getty Images

Kauli kama hii pia imesikika kutoka upande wa Japan, ambako Waziri wa Mambo ya Nje, Yoshihide Suga, amesema mbali ya nchi yake kutaka maelezo ya kina juu ya mazungumzo kati ya Korea Kusini na Kaskazini, bado shinikizo dhidi ya Korea Kaskazini litaendelea.

"Japan inawasiliana na Korea Kusini kwenye viwango vingi, lakini narejea kauli ya Makamu wa Rais wa Marekani kwamba lolote linawezekana, hadi pale Korea Kaskazini itakapoonesha hatua za kweli za kuachana na silaha za nyuklia. Japan, Marekani na Korea Kusini zitashirikiana na mataifa mengine, kwa kutumia njia zote, kuishinikiza Korea Kaskazini kwa kiwango cha juu kabisa hadi iachane na programu zake za nyuklia na makombora," aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatano (7 Februari).

Maendeleo ya sasa kwenye mahusiano kati ya Korea mbili yanafuatia miezi kadhaa ya vitisho, uhasama na matusi kati ya Rais Trump wa Marekani na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, kabla ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi kuibua matumaini mapya ya kidiplomasia.

Moon atakutana na mwenzake wa Kim mwezi ujao katika eneo lisilofanyika harakati za kijeshi upande wa kusini. Hii ni kwa mujibu wa serikali ya Korea Kusini, mara tu baada ya ujumbe wake kurejea kutoka ziara yake ya kihistoria mjini Pyongyang.

Ujumbe huo ulirudi na salamu za Kim Jong Un kwamba nchi yake itasitisha urushaji wa makombora na majaribio ya nyuklia wakati mazungumzo baina yao yakiendelea.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf