1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Irak na mkutano wa Sham el Sheikh

4 Mei 2007

Waziri mkuu al Maliki wa Irak amezitaka nchi jirani kushirikiana na serikali yake kumaliza machafuko nchini Irak.Isitoshe, amedai kufutiwa Iraq madeni yake .

https://p.dw.com/p/CB4J
Waziri wa nje wa Uingereza huko Sham el Sheikh
Waziri wa nje wa Uingereza huko Sham el SheikhPicha: AP

Katika mkutano wa kimataifa ulioanza jana huko Sham el Sheikh,Misri, juu ya usalama nchini Irak,serikali ya Irak ya waziri mkuu al Maliki,imejitolea kufanya juhudi mpya ya kurejesha maskizano na suluhu nchini.

Kwa upande mwengine,serikali ya Baghdad imeomba kufutiwa madeni yake ilikuwa nayo wakati wa enzi za utawala wa Saddam Hussein.

Umoja wa Mataifa nao umeahidi kuchangia kwa nguvu zaidi kuliko ilivyofanya hadi sasa kupunguza maafa ya binadamu nchini Irak.

Katibu mkuu wa UM Ban Ki-Moon aliuwambia mkutano:

“Tusiache mkono Irak na matatizo yake iliyonayo.”

Huo ni mwito wa katibu mkuu Ban Ki Mooon kwa wajumbe huko Sham el Sheikh.Jamii ya kimataifa na hasa nchi jirani zinapaswa kushirikiana kuigeuza Irak kuwa nchi ya amani,ilioungana na iliostawi.

Mchango wa majirani wa Irak ndio shina la mkutano huu.Nchi jirani na Irak kama Syria na Iran zinatupia macho nchini Irak masilahi yao na hivyo zinachangia katika kutoleta hali ya utulivu.

Waziri wa nje wa Ujerumani,ambayo ni mweenyekiti wa sasa wa dola kuu 8 za kiviwanda-G-8 Walter Steinmeier asema:

“Inatupasa kusaka njia na mbinu kuzizindua nchi hizo mbili zitambue jukumu lao na kuzifanya zinyoshe njia bora itakayoleta hali bora ya usalama.”

Asema waziri wa nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.hii si mara ya kwanza kwa serikali ya Irak kushauriana na nchi jirani juu ya maswali ya usalama na kuijenga nchi upya,lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.Hivi sasa nchi za kiarabu binafsi zimejitolea kufuta madeni yao kwa Irak na usoni kabisa ni Saudi Arabia.Lakini fedha sio haza balaa linaloitatiza zaidi Irak,bali usalama:

Waziri mkuu wa Irak Nuri al-Maliki,kwahivyo, aliwataka majirani zake kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo na kuwazuwia wale aliowaita “wapiganaji wa kigeni” kuvuka mipaka yao na kuingia Irak.

“Tunazitaka nchi ziliopo katika eneo hili kuyazuwia makundi ya magaidi kuingia Irak na kuvizuwia kujipatia fedha au msaada tangu wa kisiasa hata kuwapigia debe katika vyombo vya habari.”

Wanaoshiriki katika mkutano huu huko Sham el Sheikh ni Iran,Syria,Saudi Arabia ,Marekani,Umoja wa Ulaya na UM pamoja na wajumbe wengine muhimu sana katika mgogoro wa Irak.

Al Maliki aliutaka ulimwengu kutoifikiria Irak ni medani ya vita ambako nchi mbali mbali zinamalizia ugomvi wao.

Siku ya kwanza jana ya mkutano huu,waziri wa nje wa Marekani Dr.Condoleeza Rice alikuwa na mkutano wa nadra kabisa na mahasimu wa kale wa Marekani-Syria na Iran.Hivyo, amegeuza sera ya Marekani ya kutozungumza na nchi hizo mbili ambazo Washington, inaziangalia ni wakorofi katika siasa za Marekani katika Ghuba na Mashariki ya kati.

Marekani mara kwa mara, ikizituhumu Syria na Iran, kupalilia ugomvi nchini Irak kati ya jamii kwa kugharimia wanamgambo wa kisuni na wa kishia wanaotoa changamoto kwa majeshi ya kigeni yaliopo Irak.Tangu Damascus hata Teheran, lakini zakanusha hayo.

Mkutano huu wa siku 2 huko Sham el Sheikh,Misri, unatarajiwa kumalizika leo kwa majirani kujitwika jukumu la kukomesha bahari ya damu ya miaka 4 nchini Irak.