1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: iko tayari kurutubisha Uranium yake nchini Russia

Miraji Othman2 Oktoba 2009

Mazungumzo baina ya Iran na madola makuu yamekwenda vizuri

https://p.dw.com/p/JwFY
Saeed Jalili, mkuu wa washauri wa Iran kuhusu masuala ya nishati yake ya kinyukliyaPicha: AP

Maofisa wa vyeo vya juu wa Iran na wa kutoka Umoja wa Ulaya watakutana mnamo siku chache zijazo kuzungumzia juu ya duru ijaya ya mazungumzo kuhusu mabishano ya nishati ya kinyukliya baina ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu na madola makuu. Shirika la habari la Iran, Fars, lilisema mazungumzo hayo yatakuwa baina ya manaibu wa mshauri mkuu wa Iran kuhusu masuala ya nyukliya, Saeed Jalili, na mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana. Katika mazungumzo ya jana baina ya Saeed Jalili na Javier Solana huko Geneva, ilikubaliwa kwamba pande hizo mbili zikutane tena mwezi huu, na pia Iran ilikubali kuwaruhusu wakaguzi wa Umoja wa Mataifa waende Iran kuki kinu chake kipya cha pili cha kurutubisha madini ya Uranium ambacho walikiweka siri...

Mazungumzo ya jana ya huko Geneva baina ya Iran na madola matano yalio na viti vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani yalitajwa kwamba ni ya kutia moyo. Baada ya majadiliano hayo, yaliodumu saa nane, mwandiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, alichomoza nje mbele ya waandishi wa habari, akionekana mwenye kupumua kidogo. Na kinyume na ilivokuwa mwaka mmoja uliopita, mara hii aliweza kutangaza matukeo mazuri. Alisema Iran katika wakati ujao itafungua milango yake wazi kwa waangalizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Kinyukliya wakitembelee kinu kipya, karibu na mji wa Qom. Pia inasemakana kwamba, kimsingi, Iran imekubali kusafirisha sehemu kubwa ya mirundiko ya madini yake ya uranium yaliosafishwa hadi Russia, ambako huko yatasafishwa zaidi kuwa nishati kwa ajili ya kinu kidogo. Chini ya mpango huo, Iran itasafirisha sehemu kubwa ya madini yake ya uranium yaliosafishwa kwa kiwango cha chini, kiwango cha asilimia 3.5, hadi Russia ambako huko itasafishwa zaidi kufikia usafi wa asilimia 19.5. Hicho bado ni kiwango cha chini kuweza kutengeneza silaha za kinyukliya. Baadae mafundi wa Kifaransa wataitumia Uranium hiyo kutenegenza nishati kwa mfumo wa vyuma vitakavorejeshwa Iran kutumika katika vinu vitakavyotoa nishati ya kinyukliya. Iran inadai kwamba itaishiwa na nishati si muda mrefu kutoka sasa. Javier Solana alisema:

Insert: O-Ton Solana...

" Iran imetuambia kwamba itashirikiana kikamilifu na wakala wa kimataifa wa nishati ya kinyukliya kuhusu kinu chake cha atomiki karibu na mji wa Qom. Karibuni itawaalika mabingwa wa kinyukliya wakitemebelee kinu hicho. Tunataraji kwamba jambo hilo litafanyika mnamo wiki zijazo."

Javier Solana EU Außenbeauftragter
Mkuu wa masuala ya ngambo wa Umoja wa Ulaya, Javier SolanaPicha: picture-alliance/ dpa

Mazungumzo hayo ya Geneva yaonesha yamepunguza mivutano baina ya Iran na madola makuu, na Rais Barack Obama wa Marekani, akizungumzia juu ya hatua hiyo ya jana ya Iran, alisema mazungumzo hayo yalikuwa mwanzo mzuri, lakini alisema Iran lazima pia iwaachilie bila ya vizuizi wakaguzi wa kimataifa mnamo wiki mbili zijazo, akionya kwamba pindi Iran itashindwa kufanya hivyo, basi Marekani itakuwa tayari kuweka mbinyo zaidi.

Lakini wachunguzi wanasema mpango huo uliokubaliwa jana Geneva ni hatua madhubuti ya kujishikiza katika kujenga hali ya kuaminiana baina ya pande mbili hizo zilizokuwa zinabishana.

Pia imetangazwa kwamba mkuu wa Wakala wa Umoja wa Mataifa juu ya Nishati ya Kinyukliya, Mohamed el-Baradei, atakwenda Iran kesho.

Kutokana na Javier Solana ni kwamba nchi za Magharibi katika mazungumzo ya jana ya Geneva zilikariri kwamba ziko tayari kutoa msaada wa kiufundi na kifedha kwa Iran kuweza kutengeneza nishati ya kinyukliya kwa matumizi ya amani, lakini kwa sharti kwamba Iran isimamishe shughuli zake za kurutubisha madini yake ya Uranium. La kutia moyo mara hii ni kwamba Iran sasa imekubali masuala hayo ya nsihati yake ya kinyukliya yazungumziwe.

Suala la kuzidihswa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran kutoka nchi za Magharibi lilikuwa haliko katika mazungumzo ya jana ya huko Geneva.

Mwandishi: Miraji Othman / AFP,AP

Mhariri: Mohammed Abdulrahman