1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran iko tayari kwa mazungumzo ya heshima na Marekani

Yusra Buwayhid
2 Juni 2019

Rais Hassan Rouhani amesema Iran haipingi mazungumzo na Washington, lakini haitokubali kushinikizwa. Mvutano umeongezeka sana katika wiki kadhaa zilizopita kati ya Marekani na Iran.

https://p.dw.com/p/3JcHi
Iran Teheran - Hassan Rouhani hält Ansprache zum "Army Day"
Picha: Getty Images/AFP

Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema jana kwamba nchi yake iko tayari kwa mazungumzo na Marekani iwapo itaonyesha heshima na kufuata sheria za kimataifa. Lakini kiongozi huyo amesema Iran haitokubali kushinikizwa na Marekani kwenda kwenye meza ya mazungumzo.

"Tuko tayari kwa mazungumzo iwapo upande mwingine utakaa kwa heshima katika meza ya mazungumzo na kufuata kanuni za kimataifa, lakini sio kutoa amri ya majadiliano," Rouhani amesema kulingana na Fars.

Mivutano kati ya Iran na Marekani imeongezeka kwa kasi kubwa katika miezi ya hivi karibuni. Marekani inasema Iran ni kitisho kwake na washirika wake bila ya kutoa ufafanuzi zaidi.

Mara kwa mara Rouhani amekuwa akikataa kukaa katika meza ya mazungumzo mpaka pale Marekani itakapoviondoa vikwazo vya kibiashara ilivyoiwekea Iran, pamoja na kurudi katika makubaliano ya nyuklia yaliyosainiwa mwaka 2015 kati ya Marekani, Iran na mataifa mengine yenye nguvu duniani.

Mvutano kati ya nchi hizo mbili ulianza baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano hayo mwaka jana na kuiwekea vikwazo zaidi Iran.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema makubaliano ya kinyuklia ya mwaka 2015 hayakuwa na nguvu ya kutosha, na anataka kuilazimisha Iran kujadili makubaliano mapya.

Bildkombo Donald Trump und Ali Khamenei
Rais wa Marekani Donald Trump (kushoto) na Kiongozi wa kidini Iran Ali Khamenei (kulia)Picha: Imago/UPI//Imago/Russian Look

Na tangu mwezi Mei, Marekani pia imeongeza uwepo wake wa kijeshi katika kanda ya Mashariki ya Kati kwa kile inachodai "kitisho" cha Iran.

Hatutaki mabadiliko ya uongozi

Siku ya Jumatatu Trump alisema kwamba Marekani haitaki mabadiliko ya kiserikali nchini Iran, na kutaja pia uwezekano wa kufanyika mazungumzo kati yao.

"Iran ina nafasi ya kuwa taifa kubwa kwa uongozi huo huo uliko madarakani...Hatutaki mabadiliko ya uongozi - Nataka hilo kuliweka wazi," amesema Trump.

Kiongozi wa kidini nchini Iran, Ayatollah Khamenei, ameyafananisha mazungumzo na serikali ya Trump na sumu kwa vile amesema serikali hiyo haina msimamo kwa lolote, akimaanisha hatua ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya kinyuklia.

Katika hotuba yake ya Jumamosi mbele ya kundi la wanariadha, Rouhani alizungumzia matamshi hayo ya hivi karibuni ya Trump, na kusema kwamba ni tofauti na ya mwaka jana yaliyokuwa yakisisitiza mabadiliko ya uongozi Iran.

"Adui yule yule aliyetangaza nia ya kuitokomeza Jamhuri ya Kiislam ya Iran mwaka jana, amesema wazi kwamba hataki kubadilisha chochote katika mfumo wetu," alisema Rouhani. "Kama tutabaki na matumaini katika vita na Marekani, basi tutashinda."

(rtre,afp)