1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran kutosalimu amri kwa Marekani

Lilian Mtono
2 Novemba 2017

Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Khamenei amemueleza rais wa Urusi Vladimir Putin kwamba mataifa yao yanatakiwa kuimarisha mashirikiano na kuitenga Marekani, na kusaidia kuleta utulivu katika eneo la Mashariki ya kati

https://p.dw.com/p/2mt40
Teheran, Russlands Präsident Wladimir Putin trifft sich mit Ayatollah Ali Khamenei
Picha: Reuters

Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Khamenei amemueleza rais wa Urusi Vladimir Putin anayezuru nchi yake kwamba mataifa hayo yanatakiwa kuimarisha mashirikiano na kuitenga Marekani, ikiwa ni pamoja na kusaidia juhudi za kuleta utulivu katika eneo la Mashariki ya kati. Taarifa hii ni kulingana na kituo cha televisheni ya serikali. Taarifa hii ni kulingana na kituo cha televisheni ya serikali. 

Kiongozi huyo mkuu wa Iran amesema kwamba Marekani ni adui namba moja wa Iran, na kamwe nchi yake haitakubali kusalimu amri kutokana na shinikizo la Marekani kuhusiana na mkataba wa kimataifa wa nyuklia. Khamenei amesema hayo kupitia hotuba yake kwenye televisheni leo hii. 

Iran na Urusi ni washirika wakuu wa rais wa Syria, Bashar al Assad, wakati Marekani, Uturuki na mataifa mengi ya Kiarabu yakiunga mkono makundi ya waasi yanaopambana ili kumuondoa Assad madarakani.

Rais Putin alikutana na viongozi wa kisiasa wa Iran ikiwa ni sehemu ya juhudi ya kulinda mahusiano yaliyoanza kuimarishwa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump hivi karibuni kutishia kujiondoa kwenye makubaliano ya kimataifa ya kupambana na nyuklia yaliyofikiwa kati ya mataifa 6 yenye nguvu duniani na Iran mwaka 2015.

Kiongozi wa Iran Khamenei alinukuliwa na kituo hicho cha televisheni akisema "mahusiano yetu yanaweza kuitenga Marekani. Kushindwa kwa Marekani inayowaunga mkono magaidi nchini Syria, ni suala lililo wazi, lakini Wamarekani wameendeleza hila zao."

Washington, US-Präsident Donald Trump spricht während einer Kabinettssitzung im Weißen Haus
Rais wa Marekani Donald Trump aliutaja mkataba huo wa nyuklia kuwa ni mbaya zaidi na kuonyesha nia ya kujitoa.Picha: Reuters/K.Lamarque

Rais wa Iran, Hassan Rouhani ametilia msisitizo matamshi ya Khamenei, akisema Iran na Urusi kwa pamoja wanaweza kukabiliana na "ugaidi wa kikanda".

Amesema, jukumu lao kubwa kwa kushirikiana na Syria ni kuhakikisha kunakuwepo na amani na utulivu wa kikanda.

Tangu Urusi iliapoingilia kati kijeshi katika vita vya Syria mwaka 2015, huku ikiungwa mkono na jeshi la Iran, Assad amefanikiwa kurejesha maeneo mengi yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi pamoja na eneo kubwa la katikati na Mashariki mwa Syria kutoka kwa wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Urusi hivi sasa inajaribu kujijenga kupitia mafanikio hayo kwa kuanzisha hatua mpya za kidiplomasi, ikiwa ni pamoja na mipango yake ya kufanya kongamano litakalokutanisha pande zinazohasimiana nchini Syria, mipango ambayo ilifikiwa Novemba 18 mjni Sochi, ingawa upande wa upinzani mkuu ulikataa kushiriki.

Hapo jana, rais Vladimir Putin, Rouhani wa Irani na Rais wa Arzebaijan Ilham Aliyev walikubaliana katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya wakuu hao kukutana mjini Tehran na kukubaliana kwamba mataifa yote yaliyoingia mktaba huo, ikiwa ni pamoja na Marekani yanatakiwa kuzingatia utekelezaji wake, taarifa hiyo ikiwa ni kulingana na shirika la habari la serikali ya Urusi, TASS.

Mazungumzo hayo pia yalilenga kuimarisha mahusiano ya kibiashara miongoni mwa mataifa hayo. Iran imesema inataka kuonyesha kwamba hakuna haja ya kupata kibali cha Marekani katika kuendeleza mahusiano hayo ya kikanda.

Mwandishi: Lilian Mtono/ECA/dpa/rtre.

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman