1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na Syria zakosolewa na El Baradei

A.Meyer-Feist - (P.Martin)4 Machi 2009

Mwaka huu 2009, Shirika la Atomu la Umoja wa Mataifa IAEA litakuwa na mkurugenzi mkuu mpya. Bado haijulikani nani atakaemrithi Mkurugenzi Mkuu wa hivi sasa Mohammed el Baradei.

https://p.dw.com/p/H5lS
Mohamed ElBaradei (L), Director General of the International Atomic Energy Agency (IAEA), speaks next to Ernest Petric, Chair of the Board of Governors for 2006-2007 during the IAEA board of governors meeting in Vienna, Austria 10 September 2007. EPA/HELMUT FOHRINGER +++(c) dpa - Report+++
Mohammed El Baradei,Mkurugenzi Mkuu wa IAEA.Picha: picture-alliance /dpa

Ingawa El Baradei hatogombea wadhifa huo kwa muhula wa nne, hata hivyo anajaribu kusuluhisha mgogoro wa mradi wa nyuklia wa Iran kwa njia ya amani.Kuna tuhuma na mashaka,lakini hakuna uhakika kuwa uranium iliyorutubushwa na Iran inatosha kutengeneza bomu la atomu. Mohammed el Baradei hawezi kuthibitisha hilo. Hata hivyo mkurugenzi mkuu huyo wa shirika la atomu la Umoja wa Mataifa ana wasiwasi mkubwa. Anasema, mradi Iran inawazuia wakaguzi wa IAEA kufanya kazi zao na haitoi hati zinazohusika na mradi huo, basi itakuwa shida kutathmini iwapo mradi wake wa nyuklia ni kwa matumizi ya kiraia au kijeshi. El Baradei akaongezea:

"Inasikitisha kuwa shirika hili halikuweza kufanya maendeleo yo yote katika masuala mengine yaliyobaki.Hiyo inasababisha wasiwasi kuhusu kipeo kilichofikiwa katika mradi wa nyuklia wa Iran kuweza kutengeneza silaha."

Kwa hivyo El Baradei kwa mara nyingine tena ameihimiza Iran kuchukua hatua zinazohitajika haraka iwezekanavyo,kurejesha imani kwamba lengo la mradi wake wa nyuklia ni kwa maslahi ya amani.Hadi hivi sasa maazimio manne yamepitishwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran bila ya kufanikiwa. Maazimio hayo yanatoa mwito kwa Iran kusitisha urutubishaji wa uranium-hiyo ni hatua muhimu na njia ndefu ya kutengeneza silaha za nyuklia.

Ujerumani,Ufaransa na Uingereza zinatishia kuchukua hatua mpya dhidi ya Iran,lakini hiyo itakuwa vigumu. Kwani serikali mpya ya Marekani haitaki kuchochea zaidi mgogoro huo,badala yake inataka kufanya majadiliano na Tehran. Umoja wa Mataifa pia unaamini kuwa vikwazo vya kiuchumi viliopi hivi sasa vinatosha kuishinikiza Iran kusitisha harakati za kurutubisha uranium. Vikwazo hivyo vimeathiri uchumi wa Iran uliodhoofika kwa sababu ya mzozo wa fedha kote duniani na kuporomoka kwa bei za mafuta. Uchumi wa Iran unategemea sana pato la mafuta ambalo huchangia sehemu kubwa ya bajeti ya taifa.

Syria nayo ikituhumiwa kuwa na mradi wa nyuklia,inashinikizwa kushirikiana na wakaguzi wa miradi ya atomu wa IAEA na kuwasilisha nyaraka zote zinazohusika na mradi huo. Hadi sasa,Damascus inakanusha kuwa na mpango kama huo. Lakini wataalamu wa atomu waliochunguza vifusi vya mtambo uliobomolewa na ndege za kijeshi za Israel miaka miwili iliyopita katika kambi ya kijeshi ya Al-Kibar nchini Syria, wamekuta chembe za uranium na hivyo kuashiria harakati za kinyuklia. Syria inangojewa kutoa maelezo yake.