1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya Wairan wazilaani Marekani na Israel

Saumu Mwasimba
11 Februari 2019

Maelfu ya Wairan wamemiminika katika miji mbali mbali kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 40 tangu mapinduzi ya Kiislamu yaliyouondowa utawala wa Shah Mohammed Reza uliokuwa ukiungwa mkono na Marekani.

https://p.dw.com/p/3D7BN
Iran Teheran - U.S. Flaggen werden während dem 40. Jahrestag der Revolution verbrannt
Picha: Reuters/Tasnim/M. Madadi

((Nchini Iran mamia kwa maelfu ya Wairan wamekusanyika kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 40 tangu kuanguka utawala wa Shah   katika mapinduzi ya kiislamu yaliyoongozwa na Ulamaa wa Kishia Ayatollah Ruhollah Khomeini, Februari 11 mwaka 1979.

Televisheni ya taifa nchini Iran imeonesha mikusanyiko mikubwa ya watu waliobeba bendera ya nchi yao na kuimba kwa sauti kuzilaani Israel na Marekani.Umma huo wa watu unasema kifo kwa Israen na kifo kwa Marekani hizi zikiwa ni nyimbo ambazozimekuwa ni alama ya mapinduzi ya kiislamu ya Iran. Bango moja limeandikwa kwa maneno yanayosema fedheha kubwa kwa Marekani mapinduzi yameingia mwaka wake wa 40. Kituo cha Televisheni ya taifa kimeripoti kwamba rais wa Iran Hassan Rouhani amesema nchi yake imejitolea kutanua nguvu zake za kijeshi na mpango wake wa makombora licha ya kuongezeka shinikizo kutoka nchi hasimu zinazotaka kuzuia harakati zake hizo.

Rouhani asisitiza nguvu za kijeshi

Iran Hassan Rohani
Picha: Irna

Katika hotuba yake rais Rouhani amenukuliwa akisema katu hawatomuomba mtu yoyote idhini ya kutengeneza makombora aina mbali mbali na Iran itaendelea kufuata njia yake na nguvu zake za kijeshi. Hotuba hiyo ya rais Rouhani ameitowa katika uwanaj wa uhuru wa Azadi ulioko mjini Tehran ambako mamia kwa maelfu ya watu walikusanyika kuadhimisha kumbukumbu ya mapinduzi ya Kiislamu. Umati  mkubwa umejitokeza katika mikusanyiko iliyodhaminiwa na serikali wakati Iran ikikabiliwa na hali ya mfumko wa bei,upungufu wa chakula pamoja na bei ya bidhaa kuongezeka,hali ambayo ilichochea wimbi la maandamano.

Mwaka 2018 rais wa Marekani Donald Trump alijiondowa katika mpango wa Nuklia wa Iran uliofikiwa 2015 pamoja na nchi zenye nguvu na kuvirudisha tena vikwazo dhidi ya serikali ya mjini Tehran na kusababisha pigo kubwa la kiuchumi kwa nchi jamhuri hiyo ya umma wa kiislamu . Maafisa wa Iran wanasema hatua ya Marekani imekuja kusababisha  vita vya kiuchumi. Wanajeshi,wanafunzi,viongozi wa kidini pamoja na wanawake waliobeba watoto walimiminika kwenye mitaa ya miji mbali mbali wengi wakibeba picha zinazomuonesha Ulamaa wa Kishia,Khomeini pamoja na kiongozi mkuu wa sasa wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.

Iran Teheran - 40. Jahrestag der Revolution
Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Salemi

Ikumbukwe kwamba tarehe kama ya leo mwaka 1979,jeshi la Iran lilisalimu amri baada ya siku kadhaa za mapambano mitaani na kuwaruhusu wanamapinduzi kudhibiti maeneo yote nchini wakati serikali ya Shah Mohammed Reza Pahlavi ikijiuzulu.Na siku hiyo Ayatollah Ruhollah Khomeini aliitangaza Iran kuwa Jamhuri ya kiislamu. Nchi yenye nguvu katika ukanda huo Saudi Arabia na nchi nyingine za kiarabu zimekuwa zikiitazama Iran kwa jicho la wasiwasi mkubwa tangu mapinduzi ya kiislamu yaliyouangusha utawala wa Shah uliokuwa ukiungwa mkono na Marekani,huku nchi hizo zikiwa na hofu kwamba Khomeini angewashawishi wanamgambo wa kiislamu kote katika kanda hiyo. Iran na Saudi Arabia ziko kwenye vita vya kiuhasama kila mmoja akiunga mkono upande wake nchini Iraq,Yemen na Syria.

Mwandishi:Yusuf Saumu/Reuters/AFPE

Mhariri: Josephat Charo