1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakanusha madai ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
14 Juni 2019

Marekani inaamini kuwa Iran inahusika na kushambuliwa kwa meli za mafuta kwenye mlango wa bahari wa Hormuz katika Ghuba ya Oman. Kwa upande wake Iran imekanusha vikali lawama hizo.

https://p.dw.com/p/3KOoy
Golf von Oman Öltanker Front Altair
Picha: picture-alliance/AP Photo/ISNA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema madai yake yanatokana na tathmini iliyofanywa na idara ya ujasusi. Pompeo ameonya kwamba Marekani itayalinda majeshi yake, maslahi ya nchi yake na yale ya washirika wake katika Mashariki ya Kati.

Pompeo amesema Marekani italiwasilisha suala hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Martaifa leo hii.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike PompeoPicha: picture-alliance/A. Brandon

Wakati huo huo jeshi la Marekani limetoa mkanda wa video ulioonyesha wanaoaminika kuwa ni wanajeshi wa kikosi cha wanamapinduzi wa Iran wakiondoa bomu ambalo bado lilikuwa halijalipuka kutoka kwenye meli moja ya mafuta kati ya meli mbili zilizolengwa na mashambulizi kwenye mlango wa bahari wa Hormuz katika Ghuba ya Oman. Jeshi la marekani limedai kuwa kikosi hicho cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kilitaka kuondoa ushahidi kutoka kwenye eneo la tukio.

Iran imekanusha vikali kuwa inahusika na mashambulizi hayo, imesema madai hayo ya Marekani hayana msingi.

Juu ya madai hayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amehoji muda yalipofanyika ambao ulikuwa samamba na wakati ambapo Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe alipokutana na kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei mjini Tehran.

Iran mapema alikanusha kuhusika na mashambulio hayo kupitia ujumbe wake kwa Umoja wa Mataifa.

Ramani inayoonesha mahala pa tukio
Ramani inayoonesha mahala pa tukio

Japan ambayo inamiliki moja ya meli zilizoshambuliwa imesema mabaharia wa chombo hicho "Kokuka Courageous” waliona kitu kinaelekea haraka upande wao kabla ya kutokea mlipuko.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tokyo, Rais wa kampuni hiyo ya meli Yutaka Katada alisema chombo hicho kilikuwa na tani 25,000 za gesi aina ya Methanol kutoka Saudi Arabia na kilikuwa kinaelekea Singapore, na kwamba meli hiyo ilishambuliwa mara mbili lakini alikanusha kuwa ilishambuliwa kwa kombora aina ya Torpedo. Katada amefahamisha kwamba sasa melim hiyo ya mafuta inakokotwa kupelekwa katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Awali katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema dunia haitaki kushuhudia vita kwenye eneo la ghuba. Hata hivyo amelaani vikali kushambuliwa meli za mafuta. Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema matukio hayo ni ya kutia wasiwasi na yanaweza kuzidisha mivutano katika Mashariki ya Kati.

Vyanzo: /AFP/DPA